Sunday, February 5, 2017

WATUMISHI SABA WA HALMASHAURI AMBAO NI WAJUMBE BODI YA KURUGENZI SACCOS MBINGA WABURUTWA MAHAKAMANI WAKIDAIWA KULA NJAMA NA KUJIPATIA MILIONI 500

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

HATIMAYE Watumishi saba wanaotoka katika Halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo wakituhumiwa kula njama na kutenda kosa la kujipatia mkopo wa shilingi milioni 500 kutoka benki ya CRDB kinyume na taratibu husika.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa serikali mkoani hapa, Shaban Mwegole mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Simon Kobero alidai kuwa washtakiwa hao pia wanakabiliwa na makosa kumi, wakidaiwa kughushi nyaraka mbalimbali na kufanikiwa kufanya wizi katika sehemu ya fedha hizo jambo ambalo limesababisha hasara kubwa kwa chama hicho kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.

Mwendesha mashtaka huyo aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa kufanya makosa hayo na kufunguliwa kesi Jinai namba 1 ya mwaka 2017 kuwa ni, Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo na Zackaria Lingowe ambao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.


Aidha Mwegole aliendelea kudai Mahakamani hapo kuwa shtaka la Kwanza linamkabili Emmanuel Mwasaga akiwa Mwenyekiti wa bodi ya ushirika huo anadaiwa kwamba Novemba 7 mwaka 2015, alitumia mbinu za kuweza kupata mkopo huo kwa kutoa cheti cha udanganyifu cha SACCOS hiyo chenye kuonyesha ukomo wa madeni ili waweze kupewa fedha hizo kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi.

Mwegole alisema kuwa Mwasaga kwa kushirikiana na Wajumbe wenzake wa bodi wanakabiliwa na kosa la pili ambapo katika mwaka huo, walitumia muhtasari wa Novemba 23 mwaka 2015 wa vikao vya bodi kughushi nyaraka na kuweza kujipatia mkopo huo kinyume na sheria za ushirika.

Vilevile alisema kuwa shtaka la tatu ni kwamba Wajumbe hao wa bodi wanadaiwa kuiba fedha za chama hicho cha ushirika shilingi milioni 137,236,250 katika kipindi hicho cha Novemba 7 mwaka 2015 baada ya kufanikiwa kujipatia mkopo huo kutoka benki ya CRDB.

Shtaka la nne mnamo mwaka 2014 hadi 2015 kwa nyakati tofauti walitenda kosa la wizi wa uaminifu, wakiwa wote saba Wajumbe wa bodi hiyo waliiba tena shilingi milioni 65 za Mbinga Kurugenzi SACCOS na kujinufaisha wao binafsi.

Katika shtaka la tano Mwasaga akiwa Mwenyekiti wa bodi anatuhumiwa pia kuiba shilingi milioni 3,931,124 kutoka katika SACCOS hiyo, ambazo alikopeshwa kwa kuaminiwa kama mkopo ili baadaye aweze kulipa kupitia mshahara wake jambo ambalo hajalitekeleza mpaka sasa.

Mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba katika shtaka la sita, alimtaja Alex Kalilo akiwa mjumbe wa bodi naye anadaiwa kuiba shilingi milioni 3,813,541 na shtaka la saba Mhadisa Meshack akiwa naye mjumbe wa bodi hiyo aliiba shilingi milioni 1,615,000 fedha ambazo waliaminiwa kama mkopo ili waweze kukatwa kupitia mshahara wao.

Pia Mwanasheria huyo wa serikali Mwegole aliongeza kuwa katika kosa la nane shilingi milioni 5,550,000 zilichotwa na Stella Mhagama, ambapo katika shtaka la tisa shilingi milioni 107,500,000 ziliibwa na Jamima Challe huku shtaka la kumi shilingi milioni 9,835,000 ziliibwa na Lucas Nchimbi.

Hata hivyo kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Februari 8 mwaka huu kutokana na upelelezi bado haujakamilika ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walikana mashtaka, wapo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waaminifu kila mmoja kwa shilingi milioni 25 na hati za mali zisizohamishika zenye thamani ya shilingi milioni 50.

No comments: