Monday, February 13, 2017

WATANZANIA WASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA MALAWI

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

WANANCHI wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi ya Malawi wamehimizwa kuona umuhimu wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini humo, ikiwemo kufanya biashara kwa njia ambazo ni halali ili waweze kuinua uchumi wao.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassan Bendeyeko alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma wanayo fursa kubwa ya kuweza kufanya hivyo ili waweze kuondokana na umaskini.

Bendeyeko alisema kuwa hivi sasa ni wakati pekee wa kuchangamkia fursa hizo kwa kujenga ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Malawi, jambo ambalo litaweza kuleta tija katika shughuli zao za kukuza uchumi wa kila siku.


Alisema kuwa hivi karibuni alihudhuria mkutano wa ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Malawi ambao ulifanyika Jijini Lilongwe pamoja na mambo mengine waliyozungumza kwenye mkutano huo, walizungumzia pia uwepo wa fursa nyingi za kilimo, uvuvi, mifugo pamoja na biashara ambazo Watanzania kwa kufuata taratibu husika wanaweza wakafanya  shughuli za kibiashara kwa kushirikiana na wananchi wa Malawi.

Pia alifafanua kwamba upande wa nchi hiyo ya Malawi kando kando mwa ziwa Nyasa wamekuwa wakitumia fursa za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi ambazo Watanzania waishio mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma wakifanya hivyo wataweza kukuza uchumi wao.

Katibu tawala huyo alieleza pia wananchi wa Malawi wameonesha nia ya kutumia bandari ya Mtwara kwa kusafirisha bidhaa zao ambazo zitapitishwa kwenye barabara ya kutoka Mtwara hadi Malawi, kupitia bandari ya Mbamba bay hivyo wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuona umuhimu wa kutumia fursa hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Vilevile aliongeza kuwa akiwa nchini Malawi walifanikiwa kwenda Mzuzu kwenye gereza kuu ambako walikutana na Watanzania nane ambao walitoka Songea mkoani Ruvuma kwenda Malawi, kufanya utafiti wa madini ya Uranium ambapo walikamatwa wakidaiwa kuwa ni majasusi.

Kadhalika alisema kuwa Watanzania hao ambao kati yao wawili ni wanawake hali yao inaendelea vizuri na kwamba hivi sasa serikali ya Tanzania inafanya mazungumzo na serikali ya nchi ya Malawi kuona namna ya kuwaachia huru.

No comments: