Thursday, February 23, 2017

SERIKALI YATOA UFAFANUZI JUU YA KUWAFUNGIA VIBANDA WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA



Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

SERIKALI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa ufafanuzi juu ya hatua iliyochukua ya kuwafungia vibanda Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea lililopo katika Manispaa hiyo kwamba, walifanya hivyo kutokana na wafanyabiashara hao kudaiwa shilingi milioni 150 za pango la vibanda vya biashara ambavyo wamepanga.

Ufafanuzi huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Kamando Mgema alipokuwa akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo.

Mgema alifafanua kuwa soko hilo lilianzishwa mwaka 1938 na kwamba ulipofika mwaka 1996 halmashauri hiyo ililazimika kuwaruhusu wafanyabiashara kukarabati vibanda hivyo vya soko ambavyo walikuwa wakifanyia biashara zao.

Alisema kuwa kila mfanyabiashara kwa wakati huo alikuwa akilipa pango la shilingi 8,000 kwa mwezi ambapo kiasi hicho kilikuwa kikiendelea kulipwa mpaka Agosti 20 mwaka 2002 wakati soko hilo lilipoungua na kuteketea kwa moto.


Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa baada ya kuungua moto soko hilo halmashauri ya Manispaa ilifanyajitihada mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma kwenye soko hilo, ambapo uongozi wa Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea, Hayati Dkt. Laurence Gama waliomba fedha toka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na kuweza kufanikiwa kujenga soko kuu la Songea.

Alisema waliochangia katika ujenzi huo ni Wizara ya fedha kupitia shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) ambalo lilitoa shilingi milioni 304,228,270 Mkopo kutoka bodi ya mikopo serikali za mitaa ilitoa shilingi milioni 125,000,000 Mchango wa halmashauri ya Manispaa shilingi milioni 50,000,000 Japan Food Aid shilingi milioni 133,944,060 na kuweza kufikia jumla ya shilingi milioni 613,172,330 ambazo zilifanya kazi ya ujenzi wa soko hilo.

Mgema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Songea alisema kuwa baada ya kupata fedha hizo ujenzi wa soko ulitekelezwa mara moja na kukamilika ambapo lilianza kutumika mwezi Mei mwaka 2004 na kwamba halmashauri hiyo kwa ujumla ilihusika na ujenzi huo kwa asilimia mia moja na kuweza kuingia mkataba wa kuwapangisha wafanyabiashara hao.

“Manispaa ilijiwekea utaratibu wa kupandisha pango kila baada ya  miaka mitatu kulingana na kuongezeka  kwa gharama za uendeshaji, mkataba wa mwisho kati ya Manispaa na wafanyabiashara hawa uliishia Juni 30 mwaka 2016 na kwamba kufikia mwezi Machi mwaka 2016 kabla ya mkataba kwisha muda wake kiliundwa kikosi kazi cha kupitia na kuhakiki wapangaji wote ili tuweze kujiridhisha ni nani anayetumia kibanda husika kutokana na kuwepo kwa taarifa kwamba baadhi ya wapangaji, wamewamilikisha wapangaji wengine kwa bei kubwa kuliko ile wanayolipa halmashauri na kusababisha kuwepo kwa msuguano mkubwa kati yao na uongozi wa Manispaa”, alisema Mgema.

Alieleza kuwa hadidu rejea zilizotumika na kikosi kazi hicho ziliweza kuwatambua wapangaji halali wa vibanda vyote 270 na kuainisha bei halisi ya sasa iliyopangwa na Manispaa na bei wanayopangishwa wapangaji halali kwa wapangaji wengine.

Pia aliongeza kuwa kufuatia kuwepo kwa hali hiyo wiki moja iliyopita serikali kwa kushirikiana na halmashauri hiyo baada ya kuona hivyo ililazimika kuvifunga vibanda vyote mpaka wafanyabiashara hao, walipe deni hilo wanalodaiwa ili halmashauri iweze kupunguza deni la mkopo iliochukua wakati wa kujenga soko hilo kutokana na kuteketea kwa moto.
 
Chiunga alisema halmashauri imepangisha pango kwa asilimia mia moja, wakati vibanda hivyo baada ya kuungua soko vilijengwa na wafanyabiashara wenyewe kwa makubaliano kwamba vikikamilika ujenzi wake nusu ya pango itakuwa inatolewa kwenda halmashauri na nusu nyingine inafidia ujenzi husika wa vibanda, hivyo ameiomba serikali iangalie namna ya kukaa pamoja na suluhisho sio kuendelea kuvifunga kwani wafanyabiashara wanaendelea kupata hasara.

No comments: