Monday, February 27, 2017

MANISPAA SONGEA YAGAWA MICHE YA MATUNDA BURE KWA WATUMISHI WAKE

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

KATIKA kuhakikisha kwamba mazingira yanaendelea kuboreshwa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, idara ya kilimo katika Manispaa hiyo imegawa bure miche bora ya matunda kwa watumishi wake wa idara mbalimbali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa uongozi wa Manispaa umefanya hivyo kwa lengo la kuwajenga watumishi wake, kuwa na tabia ya mara kwa mara kupenda kupanda miti ya matunda na miti mingine ya aina mbalimbali ili kusaidia kuhifadhi mazingira na watu kuweza kupata matunda.

Midelo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea, imenunua miche bora ya matunda 2000 yenye thamani ya shilingi milioni 5,000,000 kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).


Kwa upande wake Ofisa kilimo wa Manispaa hiyo, Zawadi Nguaro naye alieleza kuwa miche yote iliyonunuliwa ni ya matunda kati ya hiyo kuna miche aina tano za maembe na miche aina mbili za mapalachichi.

“Lengo letu la idara ni kuhakikisha watumishi wetu wanakuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza kila mwaka, ili kuhifadhi mazingira na kupata matunda bora ambayo ni muhimu kwa afya na kuwaongezea kipato”, alisema Nguaro.

Miongoni mwa watumishi waliofaidika na miche hiyo ni Katibu tawala wa wilaya ya Songea Pendo Ndumbaro na Madiwani wa Manispaa hiyo.

Pia Nguaro aliwaasa watumishi hao ambao walipewa miche hiyo kuhakikisha kwamba wanaitunza vizuri, ili iweze kukua na kuanza kuzaa matunda ambayo itakuwa ni faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.


No comments: