Tuesday, February 7, 2017

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMNYWESHA SUMU MWANAYE NA KUMSABABISHIA KIFO

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Suzana Mgaya (19) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wino tarafa ya Madaba wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, kwa tuhuma ya kumnywesha sumu mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliyejulikana kwa jina la Gerlad Kabelege na kusababisha afariki dunia huku yeye mwenyewe pia akinywa sumu hiyo kwa lengo la kutaka kujiua.

Taarifa zilizopatikana jana mjini Songea na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari 5 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji hicho cha Wino.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa Suzana Mgaya siku hiyo alikutwa akitoka povu mdomoni na puani jambo ambalo lilisababisha hofu kwa mashuhuda kuwa huenda amekunywa sumu.


Mwombeji alifafanua mashuhuda hao walimkuta Mgaya akiwa mahututi baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake ambao alikuwa ameufunga kwa ndani na kwamba juhudi za kuwaokoa zilifanyika kwa kuwatoa ndani ya nyumba hiyo kisha kuwapeleka kwenye zahanati ya kijiji cha Wino ambapo mtoto Gerlad alifariki wakati akipatiwa matibabu.

Akifafanua juu ya tukio hilo Kamanda Mwombeji alisema kuwa Mgaya baada ya kuonekana hali yake inaendelea kuwa mbaya alikimbizwa kwenye kituo cha afya cha Madaba ambako alipatiwa rufaa ya kwenda hospitali ya serikali ya mkoa huo iliyopo mjini hapa na kufikishwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na baadae aliweza kupata nafuu.

Alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo akiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba mara baada ya uchunguzi huo kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.


Kadhalika uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo baada ya kufariki dunia ulifanyika katika kituo cha afya cha Madaba na kuweza kubaini kuwa kitu alichokuwa amemnyeshwa inadaiwa kuwa ni sumu ambapo taarifa zitatolewa baadaye kuwa ilikuwa ni ya aina gani.

No comments: