Sunday, February 5, 2017

ATIWA MBARONI KWA TUHUMA YA KUMBAKA MWANAFUNZI

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Luhimba kata ya Mtyangimbole wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Allan Kihwili (48) ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita, ambaye anasoma shule ya msingi Ngembambili na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri.

Zubery Mwombeji.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 24 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika kijiji hicho wilayani hapa.

Mwombeji alifafanua kuwa inadaiwa siku ya tukio hilo mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa anapita jirani na nyumba ya mtuhumiwa huyo ghafla alimkamata na kumwingiza kwenye nyumba anayoishi kisha kumfanyia unyama huo.


Alibainisha kuwa mbinu aliyoitumia mtuhumiwa Kihwili ni kwamba alikuwa akimvizia mtoto huyo wakati anapita kwenye eneo la nyumba yake, akimtaka amuulize maswala ya shuleni anakosoma ndipo alipofanikiwa kumkamata na kumwingiza ndani ya nyumba yake hatimaye kumfanyia ukatili huo.


Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma alisema kwamba uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo kinaonesha kumekuwa na imani za ushirikina ambazo zilimfanya mtuhumiwa amfanyie kitendo cha kinyama msichana huyo, ambapo Jeshi hilo linaendelea kufanya upelelezi wa kina kuhusiana na tukio hilo ili mtuhumiwa aweze kufikishwa Mahakamani kujibu shitaka linalomkabili mbele yake.

No comments: