Monday, February 13, 2017

MGOGORO SOKO KUU SONGEA WAFANYABIASHARA WAFUNGA SAFARI DODOMA KUMUONA WAZIRI MKUU

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wametuma ujumbe wa wafanyabiashara wenzao watano na wazee watano kwenda Dodoma kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa lengo la kupeleka kilio chao baada ya Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema kudaiwa kuwafungia vibanda vyao vya biashara, tangu Februari 11 mwaka huu kwa madai kwamba wanadaiwa shilingi milioni 100 na halmashauri hiyo jambo ambalo wamekana na kueleza kuwa sio la kweli.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Masoko katika Manispaa ya Songea (UWABIMASO) Leonard Chiunga alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa dharura na wafanyabiashara hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chama cha walimu Songea uliopo mjini hapa ambao ulihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania mkoa wa Ruvuma, Issaya Mwilamba.

Chiunga alisema kuwa tokea maduka hayo yalipofungwa wateja ambao wamekuwa wakienda kwa ajili ya kupata mahitaji kwenye maduka hayo wanashindwa kupata mahitaji husika, jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwao hivyo wanaziomba mamlaka za juu zione umuhimu wa kuchukua hatua haraka kuyafungua ili hata wafanyabiashara hao nao wasiweze kupata hasara kutokana na kuyafunga huko.


Alifafanua kuwa Mkuu wa wilaya, Mgema akiwa ameongozana na Kamati yake ya ulinzi na usalama majira ya saa tatu asubuhi ndiyo aliweza kuchukua jukumu la kuyafunga maduka hayo ambayo ni 275 yaliyopo kwenye vibanda vya Soko kuu lililopo mjini hapa, kwa madai kuwa wafanyabiashara wanatakiwa waingie mikataba upya na halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lazima na pango la vibanda hivyo inabidi lipande kwa asilimia mia moja jambo ambalo alidai kuwa ni kinyume na makubaliano ya vikao mbalimbali vilivyofanyika.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa mnamo Januari 27 mwaka huu kilifanyika kikao katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ambako waliazimia kuwa halmashauri ya Manispaa hiyo ni lazima ijiridhishe kwa kukaa pamoja na wafanyabiashara hao na kujadili jambo hilo kabla haijachukua maamuzi magumu kama hayo bila kuwashirikisha walengwa.

Alisema kwamba wafanyabiashara wameshangazwa kuona Mkuu wa wilaya hiyo, Mgema kuchukua uamuzi wa kufunga vibanda hivyo vya wafanyabiashara kwa kutumia nguvu wakati jambo hilo bado lipo kwenye vikao vya mazungumzo na kwamba Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge aliahidi kuumaliza mgogoro huo.

Kadhalika alieleza kuwa kufuatia kuendelea kufukuta kwa mgogoro huo viongozi wa wafanyabiashara hao wameunda Kamati ya usuluhishi ambayo ina Wajumbe kumi, wakiwemo wazee watano wa halmashauri ya Manispaa ya Songea ambao wameondoka Februari 12 mwaka huu majira ya asubuhi kwenda Dodoma kumuona Waziri Mkuu, Majaliwa ili aweze kuwasaidia kumaliza tatizo hilo ambalo linaonekana viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwakandamiza wafanyabiashara hao wakitaka wasaini mikataba ambayo sio rafiki kwao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoani Ruvuma, Issaya Mwilamba alisema kuwa kitendo cha uongozi wa wilaya ya Songea kwa kushirikisha na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwenda kufunga vibanda hivyo kwa kutumia nguvu ni kosa hivyo wanaiomba serikali iingilie kati ili waweze kumaliza mgogoro huo.

Mwilamba alisema kuwa kwa muda mrefu sasa halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa na migogoro mingi isiyokuwa na mwisho ambayo imekuwa ikiendekezwa kwa kufuata majungu jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Vilevile Mkuu wa wilaya ya Songea, Mgema alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na mgogoro huo alithibitisha kuvifunga vibanda vya maduka hayo vinavyozunguka Soko kuu mjini hapa, huku akiongeza kuwa bado anafanya kwanza mazungumzo na wahusika ili aweze kumaliza tatizo hilo.


Mkuu wa mkoa Ruvuma Dkt. Mahenge naye alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa tayari alikwisha anza kuufanyia kazi mgogoro huo na kwamba hivi sasa yupo Dodoma kikazi, ambapo atakaporudi atahakikisha jambo hilo linakwisha.

No comments: