Sunday, February 19, 2017

KAMATI YA UONGOZI NA MIPANGO YARIDHISHWA NA UJENZI NYUMBA ZA WALIMU KITURA SEKONDARI

Na Dustan Ndunguru,   
Mbinga.

WAJUMBE Kamati ya uongozi na mipango katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Kampuni ya Sinani Building Contactors katika kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu shule ya sekondari Kitura iliyopo wilayani humo, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 168.7.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose Nchimbi alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo alisema kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake utasaidia kuondoa tatizo la walimu kukosa nyumba za kuishi na kuondokana na adha ya kupanga uraiani.

Nchimbi alisema kuwa mradi huo unagharimu fedha nyingi hivyo ni vyema ujenzi wake unapaswa kuwa wa viwango vinavyokubalika na kwamba kamwe halmashauri hiyo, haitawavumiliwa makandarasi ambao wamekuwa na tabia ya kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi na kusababisha kuzua malalamiko yasiyokuwa ya lazima.


Alisema wahandisi wanapaswa pia kuwa makini pale wanaposhauri na kusimamia mradi kwani wengine wamekuwa wakikosa uaminifu ambapo hushirikiana na makandarasi hao kuhujumu, jambo ambalo halipaswi kupewa nafasi na kwamba wakati umefika sasa kwa wale wenye tabia hiyo kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao kwani serikali hii ya awamu ya tano haina muda wa kuwavumilia.

“Nimekuja hapa kukagua ujenzi wa nyumba hizi za walimu kimsingi tumeridhishwa na viwango vya ujenzi wa jingo hili sasa niwaombe kamilisheni kwa wakati, ili hatimaye walimu waweze kuhamia hapa na kuanza kuishi katika nyumba hizi”, alisema Nchimbi.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Zena Mijinga pamoja na kupongeza kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika utekelezaji wa mradi huo alishauri kwamba viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani na mtendaji wanapaswa wahakikishe wanatembelea eneo hilo mara kwa mara ili kujiridhisha na kazi hiyo ya ujenzi unaoendelea kufanyika hapo ili iweze kwenda sambamba na malengo husika.


Zena alisema kuwa serikali itaendelea kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi mara kwa mara kwa lengo la kujionea na kujiridhisha kama kweli inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika huku akiitaka kampuni hiyo ya Sinani ihakikishe inaendelea kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na maelekezo iliyopewa.

No comments: