Sunday, February 26, 2017

WANANCHI WAHAKIKISHIWA UJENZI WA DARAJA MTO KITURA

Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma Ambrose Nchimbi amewahakikishia wananchi wa kata ya Kitura wilayani humo kwamba halmashauri hiyo itajenga daraja la mto Kitura ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa kata hiyo, sambamba na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto zingine ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri wilaya Mbinga, Gombo Samandito.
Nchimbi alisema hayo juzi wakati wa majumuisho ya ziara yake ya Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri hiyo, ilipotembelea kata hiyo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo ya wananchi ambapo Wajumbe waliweza kupata fursa ya kutembelea daraja la mto Kitura, zahanati, nyumba ya mganga, ofisi ya kata na kukagua ujenzi wa nyumba za walimu katika sekondari ya Kitura.

Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi hiyo ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa nyakati tofauti wilayani humo, sambamba na kubaini changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba wananchi amewaasa kutoa ushirikiano wa karibu kwa kueleza ukweli hasa pale wanapobaini mradi unatekelezwa chini ya kiwango.


Nchimbi alisema kuwa muda mrefu wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa barabara ya uhakika hususani ile inayotoka Mbinga kwenda Litembo hadi Nkiri, ambayo ipo chini ya Wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma (TANROADS) ambayo hivi sasa imesahaulika kutokana na kutofanyiwa matengenezo ya uhakika mara kwa mara na hivyo kuwa kero kubwa kwa wananchi.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Kitura, Areus Nguhi aliwashukuru Wajumbe wa Kamati ya uongozi na mipango kwa uamuzi wake wa kuitembelea kata hiyo na kuona changamoto mbalimbali zilizopo, ambazo wananchi wamekuwa wakikabiliana nazo na kwamba yeye atahakikisha anatekeleza maagizo yote muhimu ambayo yameelekezwa na Wajumbe hao ili kutatua kero ambazo zimekuwa kwa muda mrefu zikiwakabili wananchi wa kata hiyo.

Nguhi alisema kuwa wananchi wake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika kuchangia nguvu zao kwenye shughuli za maendeleo hivyo aliiomba halmashauri kuhakikisha inapeleka vifaa vya viwandani kwa wakati, ili kukamilisha ujenzi wa majengo ambayo nguvu hizo zimetumika na hivyo kuyanusuru yasiweze kubomoka hasa katika kipindi hiki cha masika ambacho mvua nyingi hunyesha.


No comments: