Sunday, September 21, 2014

CHUO KIKUU CHA SAYANSI SONGEA CHA PONGEZWA KWA JITIHADA ZAKE


Na Mwandishi wetu,

Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amekipongeza chuo kikuu cha sayansi ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani humo, kwa jitihada zake za kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma na kukuza elimu ya juu hapa nchini.

Mwambungu alitoa pongezi hizo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya tano ya chuo hicho mjini hapa, kwa wahitimu 119 wa shahada na stashahada ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho, kumesaidia kulipunguzia taifa tatizo la ukosefu wa wataalam wa sayansi hususan katika ukanda wa kusini na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha sayansi ya kilimo na teknolojia katika sekta ya kilimo, ni jambo jema kwa ustawi wa nchi na uti wa mgongo na mwajiri mkubwa kwa wananchi huku akiwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Alieleza kuwa katika maisha ya sasa hakuna njia fupi ya kufikia mafanikio katika maisha  zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa, na kwamba changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora,  huku akiwataka kuboresha mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto hizo.

Friday, September 19, 2014

MKUU WA MKOA RUVUMA AKUTANA NA MADEREVA PIKIPIKI, ASISITIZA AMANI NA UTULIVU


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akizungumza na waendesha pikipiki (Maarufu kama  Boda Boda) leo katika ukumbi wa Songea Club uliopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma. Mwambungu amewataka madereva Boda boda kuepusha ajali za barabarani kwa kufuata sheria, na kutotumiwa na vyama vya kisiasa.

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

BAADA ya siku chache kupita kufuatia tukio la nani amefanya kitendo kiovu cha kurusha bomu la kienyeji katika mtaa wa Msufini Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, na kujeruhi baadhi ya askari Polisi mjini hapa, Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu amekutana na waendesha pikipiki wa manispaa hiyo na kuwataka  kujenga ushirikiano ili kuweza kulinda amani ya nchi dhidi ya maadui ambao hawalitakii mema taifa hili.

Mwambungu amekutana leo na madereva hao maarufu kwa jina la “Boda boda” katika ukumbi wa Songea Club uliopo mjini Songea, akisisitiza kujenga ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuweza kupata ukweli wa tukio hilo na kuwafanya wakazi wa mji huo, watu wengine (wageni) wanaoingia na kutoka kuondoa hofu na kuishi katika hali ya usalama.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa jamii ihakikishe kwamba amani utulivu vinatawala miongoni mwao, na pale wanapoona kuna sintofahamu ni vyema watoe taarifa katika vyombo husika vya usalama ili kuweza kubaini uhalifu unaofanyika na hatua ziweze kuchukuliwa haraka dhidi ya wahalifu.

JESHI LA POLISI NCHINI LANYOSHEWA KIDOLE LATAKIWA KUACHA KUNYANYASA WAANDISHI WA HABARI

Rais Jakaya Kikwete wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

















Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

JESHI la Polisi nchini limetakiwa kuacha vitendo vya  kuwanyanyasa waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao ipasavyo, kufanya hivyo ni kutowatendea haki na kudhalilisha taaluma ya habari.

Sambamba na hilo Jeshi hilo limenyoshewa kidole kwamba limekuwa na historia ya kupiga na kuwafukuza waandishi wa habari, hasa pale wanapotafuta ukweli juu ya matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea miongoni mwa jamii.

Rai hiyo imetolewa na baadhi ya Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kufuatia tukio lililotokea jana makao makuu ya jeshi hilo baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe.

Thursday, September 18, 2014

JESHI LA POLISI NCHINI LATHIBITISHA BOMU WALILORUSHIWA ASKARI WAKE MJINI SONGEA LIMETENGENEZWA KIENYEJI

 Eneo la tukio mtaa wa Msufini mjini Songea mkoani Ruvuma, ambako bomu ambalo limetengenezwa kienyeji lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana Jeshi la Polisi likiwa limezungushia alama.
Askari Ramadhani Ally, akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea, akielezea kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi mkasa huo ulivyowakuta na askari wenzake wakati walipokuwa doria mtaa wa Msufini mjini hapa,  baada ya kurushiwa bomu ambalo limetengenezwa kienyeji na watu wasiojulikana mpaka sasa.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.


JESHI la polisi nchini limethibitisha kuwa kitu kilichokuwa kinadaiwa kuwa ni bomu lililorushwa mjini Songea mkoani Ruvuma, na kuwajeruhi askari wa jeshi hilo mjini hapa kuwa ni la kutupwa kwa mkono.

Tukio hilo lilitokea  Septemba 16 mwaka huu majira ya saa 1.25 usiku katika eneo la Misufini na kuwajeruhi askari polisi watatu kati ya wanne waliokuwa doria na kwamba bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo kwa waandishi wa habari mjini hapa, Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai kamishina wa polisi Isaya Mngulu amesema bomu hilo lilirushwa na watu wasiojulikana na kuwajeruhi askari polisi watatu waliokuwa doria siku hiyo.

Mngulu alisema askari hao ni wa kituo kikuu cha polisi mjini Songea ambao aliwataja kuwa ni G.5515 PC John, G7351 PC Ramadhan na WP 10399 Felista ambapo baaada ya kujeruhiwa kwa bomu hilo, walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu.

KATIBU TAWALA MSAIDIZI MKOANI RUVUMA NA WENZAKE WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA WIZI WA SHILINGI MILIONI 800

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MWENYEKITI wa chama kikuu cha ushirika (SONAMCU) wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma, amefikishwa katika Mahakama ya mkoa huo akiwemo na Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo ambaye pia ni afisa ushirika wa mkoa huo, kwa tuhuma za kula njama, kugushi nyaraka na kuiba fedha shilingi milioni 889.

Imedaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali Hamimu Mkoleye mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa huo Joackimu Tiganga washtakiwa hao wote wawili wanalinganishwa na washitakiwa wengine 14 ambao walikwisha somewa mashitaka na kufanya idadi yao kuwa 16 ambapo wanadaiwa kuiba fedha hizo.

Mkoleye amewataja waliofikishwa mahakamani hapo kuwa ni Ally Athumani Bango (45) Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Namtumbo (SONAMCO) ambacho kinajishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku.

AHUKUMIWA KWENDA JELA BAADA YA KULAWITI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKAZI mmoja wa Mjimwema Songea mjini mkoani Ruvuma, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu mkazi wa mkoa huo adhabu ya kifungo cha maisha  kwenda gerezani kwa kosa la kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka tisa.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa huo, Joakimu Tiganga alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa John Mapunda (38) mkazi wa Mjimwema songea mjini bila halali alimlawiti msichana huyo.

DEREVA PIKIPIKI AKUTWA AMEFARIKI DUNIA BAADA KUCHOMWA KISU TUMBONI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MTU mmoja ambaye ni dereva wa pikipiki amekutwa amefariki dunia baada kuchomwa kisu tumboni na kupigwa na kitu kizito kichwani kisha mwili wake kufungwa kamba mikononi na miguuni hatimaye kuunganishwa kwenye mti na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea Septemba 16 mwaka huu majira ya mchana ambapo mwili wa marehemu huyo umetambuliwa kwa jina la Maulid Kuburi (21) mkazi wa kijiji cha Mpandangindo Songea vijijini mkoani Ruvuma.

Mwili wa marehemu huyo umekutwa na majeraha ambapo alichomwa kisu mara tatu tumboni kisha kufariki dunia.

ASKARI SONGEA WAJERUHIWA NA KITU KINACHODAIWA KUWA NI BOMU LA KURUSHWA NA MKONO



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ASKARI watatu  wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini  wakiwa wanapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu la kurusha kwa mkono.

Tukio hilo limetokea Septemba 16 mwaka huu majira ya jioni katika kata ya Msufini mjini hapa, ambapo wamejeruhiwa.

Akizungumzia tukio hilo kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo ASP George Chiposi,  alisema kuwa watu watatu wasio fahamika ndio waliotupa kitu hicho kinacho sadikiwa kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono.

Bomu hilo alisema limetengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari  hao watatu waliokuwa doria.

Wednesday, September 10, 2014

SERIKALI YARUHUSU WAFANYABIASHARA KUUZA MAHINDI NJE YA NCHI



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

SERIKALI hapa nchini imeruhusu wafanyabiashara kuuza mahindi yao nje ya nchi popote pale, huku ikiwataka kuzingatia bei elekezi iliyowekwa ili kumfanya mkulima asiweze kupata hasara.

Sambamba na hilo mahindi ambayo yamehifadhiwa katika vituo husika vilivyopo mkoani humo, serikali itayanunua kwa kilo shilingi 500 na kwamba wakulima hawaruhusiwi kuingiza mahindi mengine katika vituo.

BASI LA SUPER FEO LAPATA AJALI LEO WATATU WAFARIKI DUNIA 25 WAJERUHIWA VIBAYA



 



Picha hizi zinaonesha basi lenye namba za usajili T 273 CDD mali ya kampuni ya Super Feo lililopata ajali katika kijiji cha Sanangula mkoani Ruvuma, ambalo lilikuwa likisafiri leo kutoka Songea mjini kwenda mkoani Mbeya.
 


Na Kassian Nyandindi,

Songea.

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 25 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini mkoani Ruvuma, kwenda  jijini Mbeya kumgonga mwendesha baiskeli na baadaye kupinduka.

Habari zilizopatikana leo mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 4:45 asubuhi, katika eneo la Sanangula nje kidogo ya Manispaa ya songea mkoani humo.

Kamanda Msikhela amefafanua kuwa ajali hiyo imetokea kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe, ambapo namba za gari yenye usajili T273 CDD aina ya Mitsubishi Rosa mali ya kampuni ya Super feo mjini Songea ambalo lilikuwa linatoka Songea kwenda Mbeya.

Tuesday, September 9, 2014

MKUU WA WILAYA MBINGA AWA MBOGO, AWASHUKIA WAFANYABIASHARA WA KAHAWA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewashukia wafanyabishara wenye tabia ya kutorosha kahawa wilayani humo kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja, na atakaye endelea kufanya hivyo pale atakapobainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kunyang’anywa kibali cha ununuzi wa zao hilo wilayani humo.

Alitoa onyo hilo wakati alipokuwa akifunga kikao cha wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma, kilichofanyika katika ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa.

WATAKIWA KUZALISHA MICHE YA KAHAWA KWA WINGI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKURUGENZI mkuu wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) Adolf  Kumburu ameziasa Halmashauri na taasisi mbalimbali hapa nchini ambako zao la kahawa linazalishwa, kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika kuzalisha miche bora ya kahawa ili kuweza kuwafikia wakulima walio wengi kiurahisi na kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.

Alisema pamoja na Taasisi ya utafiti wa kahawa nchini (TaCRI) kuzalisha miche hiyo na kuisambaza, bado haitoshelezi mahitaji, kutokana na uzalishaji kuwa mdogo hivyo ili kuondokana na tatizo hilo wakulima, halmashauri na taasisi zingine zinapaswa kushiriki katika kuanzisha bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa.