Sunday, September 21, 2014

CHUO KIKUU CHA SAYANSI SONGEA CHA PONGEZWA KWA JITIHADA ZAKE


Na Mwandishi wetu,

Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amekipongeza chuo kikuu cha sayansi ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani humo, kwa jitihada zake za kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma na kukuza elimu ya juu hapa nchini.

Mwambungu alitoa pongezi hizo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya tano ya chuo hicho mjini hapa, kwa wahitimu 119 wa shahada na stashahada ambapo alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho, kumesaidia kulipunguzia taifa tatizo la ukosefu wa wataalam wa sayansi hususan katika ukanda wa kusini na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha sayansi ya kilimo na teknolojia katika sekta ya kilimo, ni jambo jema kwa ustawi wa nchi na uti wa mgongo na mwajiri mkubwa kwa wananchi huku akiwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Alieleza kuwa katika maisha ya sasa hakuna njia fupi ya kufikia mafanikio katika maisha  zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa, na kwamba changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora,  huku akiwataka kuboresha mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto hizo.


Vilevile Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliwataka wanafunzi wa chuo hicho cha Mtakatifu Joseph, kuombea amani hususan katika kipindi hiki kigumu ambacho Taifa linaingia kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya, na kwamba wajiepushe na wale wenye tabia ya kuhamasisha uvunjifu wa amani bila sababu za msingi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya chuo hicho Askofu John Ndimbo, alisema anajisikia fahari kuona chuo hicho kinazalisha wataalam wengi wa sayansi kanda wa kusini, huku akisema kuwa elimu ni tunu kubwa ya maendeleo katika ulimwengu wa sasa wa karne hii ya sayansi na tekinolojia.

Ndimbo alitoa rai kwa uongozi wa chuo na wanafunzi kuhakikisha wanafuata taratibu, sheria na miongozo ya wizara ya elimu badala ya kuzalisha migogoro isiyokuwa na faida yoyote kwa madai kwamba, gharama ya kutuliza ni kubwa pamoja na kupoteza rasilimali muda.

No comments: