Friday, September 19, 2014

MKUU WA MKOA RUVUMA AKUTANA NA MADEREVA PIKIPIKI, ASISITIZA AMANI NA UTULIVU


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akizungumza na waendesha pikipiki (Maarufu kama  Boda Boda) leo katika ukumbi wa Songea Club uliopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma. Mwambungu amewataka madereva Boda boda kuepusha ajali za barabarani kwa kufuata sheria, na kutotumiwa na vyama vya kisiasa.

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

BAADA ya siku chache kupita kufuatia tukio la nani amefanya kitendo kiovu cha kurusha bomu la kienyeji katika mtaa wa Msufini Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, na kujeruhi baadhi ya askari Polisi mjini hapa, Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu amekutana na waendesha pikipiki wa manispaa hiyo na kuwataka  kujenga ushirikiano ili kuweza kulinda amani ya nchi dhidi ya maadui ambao hawalitakii mema taifa hili.

Mwambungu amekutana leo na madereva hao maarufu kwa jina la “Boda boda” katika ukumbi wa Songea Club uliopo mjini Songea, akisisitiza kujenga ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuweza kupata ukweli wa tukio hilo na kuwafanya wakazi wa mji huo, watu wengine (wageni) wanaoingia na kutoka kuondoa hofu na kuishi katika hali ya usalama.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa jamii ihakikishe kwamba amani utulivu vinatawala miongoni mwao, na pale wanapoona kuna sintofahamu ni vyema watoe taarifa katika vyombo husika vya usalama ili kuweza kubaini uhalifu unaofanyika na hatua ziweze kuchukuliwa haraka dhidi ya wahalifu.


“Ni kweli leo nimezungumza nao, ni kawaida yangu kukutana nao jambo kuu nimesisitiza kujenga ushirikiano na  amani, na waache kutumiwa katika mambo ya kisiasa, siku zote amani ndio msingi mkuu”, alisema Mwambungu.

Mwambungu aliongeza kuwa hivi sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo, na kwamba mpaka sasa hakuna mtu aliyepatikana ambaye anahusika kutenda unyama huo.

Pamoja na mambo mengine tukio la kurushwa kwa bomu hilo, lilitokea Septemba 16 mwaka huu majira ya 1:25 usiku katika mtaa wa Msufini katika Manispaa ya Songea na kuwajeruhi askari Polisi watatu kati ya w anne waliokuwa doria huku Jeshi la Polisi nchini likithibitisha kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Askari waliojeruhiwa ni G 5515 PC John, G 7351 PC Ramadhan na WP 10399 Felista ambapo baada ya kujeruhiwa kwa bomu hilo, walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu zaidi.

PC John aliyepata majeraha kiasi alipatiwa matibabu siku hiyo na kuruhusiwa, huku askari wawili PC Ramadhan na WP Felista wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

No comments: