Thursday, September 18, 2014

JESHI LA POLISI NCHINI LATHIBITISHA BOMU WALILORUSHIWA ASKARI WAKE MJINI SONGEA LIMETENGENEZWA KIENYEJI

 Eneo la tukio mtaa wa Msufini mjini Songea mkoani Ruvuma, ambako bomu ambalo limetengenezwa kienyeji lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana Jeshi la Polisi likiwa limezungushia alama.
Askari Ramadhani Ally, akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea, akielezea kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi mkasa huo ulivyowakuta na askari wenzake wakati walipokuwa doria mtaa wa Msufini mjini hapa,  baada ya kurushiwa bomu ambalo limetengenezwa kienyeji na watu wasiojulikana mpaka sasa.

Na Kassian Nyandindi,
Songea.


JESHI la polisi nchini limethibitisha kuwa kitu kilichokuwa kinadaiwa kuwa ni bomu lililorushwa mjini Songea mkoani Ruvuma, na kuwajeruhi askari wa jeshi hilo mjini hapa kuwa ni la kutupwa kwa mkono.

Tukio hilo lilitokea  Septemba 16 mwaka huu majira ya saa 1.25 usiku katika eneo la Misufini na kuwajeruhi askari polisi watatu kati ya wanne waliokuwa doria na kwamba bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo kwa waandishi wa habari mjini hapa, Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai kamishina wa polisi Isaya Mngulu amesema bomu hilo lilirushwa na watu wasiojulikana na kuwajeruhi askari polisi watatu waliokuwa doria siku hiyo.

Mngulu alisema askari hao ni wa kituo kikuu cha polisi mjini Songea ambao aliwataja kuwa ni G.5515 PC John, G7351 PC Ramadhan na WP 10399 Felista ambapo baaada ya kujeruhiwa kwa bomu hilo, walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu.

Alisema askari PC John aliyepata majeraha kiasi alipatiwa matibabu siku hiyo na kuruhusiwa, huku askari wawili PC Ramadhan na WP Felista wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri.

Vilevile alieleza kuwa jeshi la polisi makao makuu kwa kushirikiana na la polisi mkoani Ruvuma na vyombo mbali mbali vya ulinzi na usalama mkoani humo,  vinaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo pamoja na kutafuta taarifa za waliohusika na tukio hilo, ambalo mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana nalo.

Alisema linaamini kuwa wahusika waliofanya tukio hilo ni sehemu ya jamii inayoishi mjini Songea au yenye mahusiano na wenyeji wa Songea na mtu aliyetengeneza bomu hilo.

“Lazima kuna  mtu au watu walioshuhudia na wanaomjua aliyerusha bomu hili, nikiwa na maana kwamba hakuwa pekee yake kuna baadhi ya wananchi wanaweza kuwa wanawafahamu wahusika wa tukio hili, wasisite kushirikiana na jeshi la polisi kuwafichua ili kuendeleza ushirikiano mwema”, alisema Mngulu.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Kamishina wa polisi Isaya Mngulu ametoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na timu ya upelelezi kutoka makao makuu ya jeshi la polisi kwa ajili ya kuwapata wahusika wa tukio hilo ambalo limetokea kwa mara ya kwanza mkoani Ruvuma na lisipofanyiwa kazi ipasavyo linaweza kutoa mwanya kwa wahalifu wa aina hiyo, kuendeleza uhalifu huo kwa wananchi pamoja na jeshi la polisi.


No comments: