Wednesday, September 10, 2014

BASI LA SUPER FEO LAPATA AJALI LEO WATATU WAFARIKI DUNIA 25 WAJERUHIWA VIBAYA



 



Picha hizi zinaonesha basi lenye namba za usajili T 273 CDD mali ya kampuni ya Super Feo lililopata ajali katika kijiji cha Sanangula mkoani Ruvuma, ambalo lilikuwa likisafiri leo kutoka Songea mjini kwenda mkoani Mbeya.
 


Na Kassian Nyandindi,

Songea.

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 25 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Songea mjini mkoani Ruvuma, kwenda  jijini Mbeya kumgonga mwendesha baiskeli na baadaye kupinduka.

Habari zilizopatikana leo mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 4:45 asubuhi, katika eneo la Sanangula nje kidogo ya Manispaa ya songea mkoani humo.

Kamanda Msikhela amefafanua kuwa ajali hiyo imetokea kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe, ambapo namba za gari yenye usajili T273 CDD aina ya Mitsubishi Rosa mali ya kampuni ya Super feo mjini Songea ambalo lilikuwa linatoka Songea kwenda Mbeya.


Ameeleza kuwa basi hilo lilikuwa kwenye mwendo kasi ambapo mbele yake kulikuwa na mwendesha baiskeli, hivyo dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina la Steven Mbigi (45) baada ya kumkwepa mwendesha baiskeli huyo na kugonga mti na kupinduka kisha  kusababisha watu wawili kufariki dunia papo hapo.

Alisema kuwa mwendesha baiskeli licha ya kujaribu kumkwepa, alijeruhiwa vibaya hivyo pamoja na majeruhi wengine wamekimbizwa katika hospitali ya mkoa huo kwa matibabu, ambako alifariki dunia akiwa chumba cha mahututi wakati madaktari wakiendelea kumpa matibabu.

Kamanda Msikhela alisema kuwa maiti ya watu wawili pamoja na majeruhi 24 bado hayajafahamika majina yao, lakini maiti zote mbili zimehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya mkoa mjini Songea.

Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa majeruhi wote majina yao bado hayajatambulika na kwamba wamelazwa katika hospitali hiyo ambako wanaendelea kupata matibabu.

Msikhela alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi  ambapo dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo, anadaiwa kutokomea kusikojulikana  mara tu baada ya ajali hiyo kutokea na  Polisi inaendelea kumsaka.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya mkoa Dokta Benedict Ngaiza amethibitisha kupokea majeruhi 25 ambao mmoja kati ya majeruhi hao aliyejulikana kwa jina la Aron Edward ambaye alikuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) alifariki dunia wakati akiendelea kupata matibabu.



No comments: