Tuesday, September 9, 2014

WATAKIWA KUZALISHA MICHE YA KAHAWA KWA WINGI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKURUGENZI mkuu wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB) Adolf  Kumburu ameziasa Halmashauri na taasisi mbalimbali hapa nchini ambako zao la kahawa linazalishwa, kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika kuzalisha miche bora ya kahawa ili kuweza kuwafikia wakulima walio wengi kiurahisi na kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.

Alisema pamoja na Taasisi ya utafiti wa kahawa nchini (TaCRI) kuzalisha miche hiyo na kuisambaza, bado haitoshelezi mahitaji, kutokana na uzalishaji kuwa mdogo hivyo ili kuondokana na tatizo hilo wakulima, halmashauri na taasisi zingine zinapaswa kushiriki katika kuanzisha bustani mama za kuzalishia miche ya kahawa.


Alifafanua kuwa wakulima  walio wengi tayari walishajengewa uwezo na wataalamu wa TaCRI namna ya kuzalisha miche, hivyo hawana budi kutumia utaalamu husika waliopewa katika kuifanya kazi hiyo ili kuondokana na tatizo la upatikanaji wa miche hiyo.

Kumburu aliyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa.  

Aidha alieleza kuwa malengo ya nchi katika kuongeza uzalishaji wa kahawa ni kufikia tani 80,000 mwaka 2016 na tani 100,000 mwaka 2021 ambapo katika kufanikisha hilo ni lazima elimu ya kutosha iwafikie wakulima sambamba na matumizi ya pembejeo (mbolea) za kutosha katika mashamba yao.

“Makisio ya uzalishaji wa kahawa mwaka huu ni tani 61,800 mara nyingi malengo ya uzalishaji hatufikii kutokana na changamoto kubwa ya matumizi madogo ya pembejeo za kilimo hasa mbolea”, alisema Kumburu.

Kwa upande wa masoko Mkurugenzi huyo alisema asilimia 85 hadi 90 ya wakulima wadogo wadogo, wanatumia soko la mnada na kwamba asilimia kumi inayobakia wakulima hao hupeleka kahawa yao moja kwa moja katika soko la nje.

Pamoja na mambo mengine aliongeza kwamba ili kahawa iweze kupata bei nzuri katika soko la ndani au nje, akulima wanapaswa kuzingatia suala la ubora ikiwemo kuzingatia kanuni za kilimo bora cha zao la kahawa.

Kumburu alisema katika Afrika, Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa kahawa ambapo huzalisha magunia milioni moja kwa msimu mmoja wa kilimo cha zao hilo, ambapo nchi inayoongoza ni Ethiopia ambayo inazalisha magunia milioni 5 ikifuatiwa na Uganda inayozalisha magunia milioni 3 na nchi ya tatu ni Ivory Coast huzalisha magunia milioni 1.5.

No comments: