Saturday, August 30, 2014

OFISA USHIRIKA MBINGA AONJA JOTO YA JIWE, WANACHAMA WAMKATAA WASEMA HAWANA IMANI NAYE


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

OFISA ushirika wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Raphael Luvanda amejikuta akiwa katika wakati mgumu kufuatia Wanachama wa chama cha kuweka na kukopa, Mbinga Lutheran SACCOS kilichopo wilayani humo kumjia juu na kumweleza kwamba hawana imani naye katika utendaji wa kazi zake, hivyo hawamtaki kumuona akifanya kazi za ukaguzi katika umoja huo.

Sambamba na hilo wanachama hao ambao walionekana kukerwa na tabia za Ofisa ushirika huyo walisema, sababu zao za msingi za kumkataa wamekuwa wakimtuhumu kwa muda mrefu kwamba anafanya kazi zake kwa mrengo wa kushoto kwa kutofuata taratibu husika.

Walieleza kuwa bodi husika itazifikisha tuhuma husika kwa mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga, ili ziweze kufanyiwa kazi huku wakitaka kuanzia sasa shughuli za ukaguzi zifanywe na ofisa ushirika mwingine kutoka katika halmashauri hiyo na sio vinginevyo.


Hali hiyo ya wanachama hao kumtuhumu Ofisa ushirika huyo ilijitokeza katika mkutano mkuu wa wanachama, liofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa.

Walisema katika hali ya kusikitisha Luvanda amekuwa na tabia za kupenda kuzua migogoro ya hapa na pale kati ya uongozi wa SACCOS hiyo na wanachama kwa ujumla.

Vilevile katika taarifa yake ya ukaguzi ya mwaka 2013 alishindwa kubainisha wizi wa fedha uliofanywa na aliyekuwa mhasibu wa ushirika huo, Ansilla Kapinga na kusababisha uongozi husika kutumia gharama kubwa kuleta wakaguzi wengine kutoka nje ya wilaya ya Mbinga.

Waliongeza kuwa amefikia hatua, hata vitabu na nyaraka muhimu za umoja huo amezuia ofisini kwake akitaa kuzirejesha, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko ya hapa na pale miongoni mwa wanachama na kufanya wakose imani naye.

“Kwa mwenendo huu hatutaweza kuvumilia suala hili, ni vyema Ofisa ushirika huyu afanye kazi zake kwa kufuata taratibu zilizowekwa na sio kujenga mipasuko ambayo inavuruga ushirika wetu”, walisema.

Walifafanua kuwa wanazo taarifa kwamba, Luvanda amekuwa hata akitoa taarifa za upotoshaji kwenye maeneo mengine ya mashirika ambayo yanatoa mikopo hapa wilayani, kwa lengo la kugonganisha viongozi husika na wanachama kwa maslahi yake binafsi.

Hata hivyo kwa upande wake Ofisa ushirika huyo alipopewa nafasi ya kujieleza aliishia kwa kuwaomba radhi wanachama hao, na kuondoka bila kutolea maelezo yakinifu yenye kufikia muafaka wa tuhuma ambazo alikuwa akinyoshewa kidole katika mkutano huo.


No comments: