Saturday, August 2, 2014

WATU SITA WAFARIKI DUNIA NA 18 WAJERUHIWA VIBAYA KATIKA AJALI YA BASI MBINGA


Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela akimtaka hali mmoja kati ya majeruhi Joseph Matembo aliyelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, ambaye amevunjika mikono na miguu katika ajali ya gari aina ya basi lenye namba za usajili T 759 BVR aina ya Nissan Civillian wakati akisafiri kutoka Mbinga mjini kwenda wilaya mpya ya Nyasa mkoani humo. Majeruhi 18 wamelazwa katika hospitali hiyo na hali zao ni mbaya.



Gari hilo lililopata ajali likionekana katika picha tofauti likiwa limetumbukia katika korongo kijiji cha Burma kata ya Nyoni wilayani Mbinga, baada ya dereva kuikosa kona kali wakati alipokuwa kwenye mwendo kasi. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.   
  
WATU sita ambao ni abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi kutoka Mbinga mjini kwenda makao makuu ya wilaya mpya ya Nyasa, mkoani Ruvuma wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya baada ya gari hilo walilokuwa wamepanda, kuacha njia na kutumbukia kwenye korongo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela, alisema gari hilo lenye  namba za usajili T 759 BVR aina ya Nissan Civillian mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini hapa (jina halijapatikana) lilipata ajali Agosti Mosi mwaka huu, majira ya saa 10:30 jioni katika kijiji cha Burma kata ya Nyoni wilayani Mbinga.

Mihayo alifafanua kuwa ajali hiyo ilisababishwa na gari kuwa katika mwendo kasi, ambapo dereva aliyekuwa akiliendesha alishindwa kulimudu kwenye kona kali na hatimaye lilitumbukia katika shimo kubwa (korongo) na kusababisha mauaji na majeruhi hao.

“Mpaka sasa dereva aliyekuwa akiliendesha gari hili bado jina lake halifahamiki kutokana na kukimbia kusikojulikana, Jeshi la polisi tunafanya jitihada ya kumtafuta ili aweze kupatikana na baadaye tupate maelezo yakinifu juu ya tukio hili”, alisema Mihayo. 


Aliwataja walimu wa shule ya msingi waliofariki dunia kuwa ni Esther Kumburu wa shule Kilimani wilayani Mbinga na Efigenia Kayombe ambaye ni mwalimu wa shule ya Linda iliyopo Mbambabay wilayani Nyasa.

Vilevile kulikuwa na Ernest Ndunguru mkazi wa kijiji cha Mikalanga wilayani Mbinga, Anna Chitete kijiji cha Kilosa wilayani Nyasa na mmoja ambaye alifahamika kwa jina moja la Mbunda mkazi wa kitongoji cha Lusonga Mbinga mjini, na kwamba maiti moja ambaye ni wa kiume bado hajatambuliwa jina lake mpaka sasa.

Aidha Kamanda Mihayo alieleza kuwa maiti zote zimehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, na kwamba majeruhi bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo lakini hali zao bado ni mbaya.

Hata hivyo alitoa wito kwa madereva wote mkoani Ruvuma, kuacha kuendesha vyombo vya moto barabarani kwa mwendo kasi, ikiwemo vile ambavyo vimekuwa vikibeba abiria kwani kufanya hivyo kuna hatarisha maisha ya watu wanaosafiri, kutoka sehemu moja kwenda nyingine.




No comments: