Friday, August 15, 2014

ASKOFU MKUU DAMIAN DALLU AWAASA WAUMINI WAKE

Watoto wa shirika la kipapa (mtoto Yesu) parokia ya Mbangamao Jimbo la Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakisherehekea siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya uinjilishaji wa parokia hiyo. Sherehe hizo zilifanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo.

Askofu mkuu Damian Dallu wakati akitoa mahubiri katika maadhimisho hayo kwa waumini wa kanisa Katoliki (hawapo pichani) Parokia ya Mbangamao Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na Julius Konala)

Na Julius Konala,
Mbinga.

ASKOFU mkuu Damian Dallu, wa Jimbo kuu Katoliki la Songea mkoani Ruvuma ameipongeza Parokia ya Mbangamao iliyopo katika Jimbo la Mbinga mkoani humo, kwa mchango wake mkubwa wa kusukuma maendeleo hususani katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964 chini ya Paroko wake wa kwanza mzalendo Hayati Askofu Maurus Komba.

Askofu Dallu ametoa pongezi hizo wakati akiwahubiria mamia ya Waumini wa kanisa hilo kwenye maadhimisho ya Ibada ya misa takatifu ya shukrani, Jubilei ya miaka 50 ya parokia hiyo iliyofanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu, mapadre, watawa, waumini pamoja na viongozi wa serikali.

Alisema Parokia hiyo kupitia Shirika la Wavisenti imefanikiwa kupanua wigo mkubwa wa kutoa huduma kwa jamii, ikiwemo kuongeza idadi ya shule za msingi hadi kufikia 15, shule za sekondari tatu na ujenzi wa shule za chekechea kwa kila kigango.

Vilevile ameeleza kuwa wameweza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo ikiwemo pamoja na parokia hiyo kuzaa parokia mpya ya Mpepai iliyopo wilayani humo na kufanya ukarabati wa zahanati, shule za msingi na ujenzi wa sekondari. 


Hata hivyo amewaomba waumini wa kanisa Katoliki kuliombea Taifa ili liweze kuendesha mchakato wa uundaji wa katiba mpya, uchaguzi ujao wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa Wabunge na Rais katika hali ya amani na utulivu tuliyoachiwa na muasisi wa taifa hili Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Waumini hao wameaswa kujenga utamaduni wa kulitegemeza kanisa kwa kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa makanisa, uanzishaji wa vigango, parokia kulipa zaka kwa wakati ikiwemo michango mbalimbali na kuwasaidia Mapadre badala ya kutegemea wafadhili toka nchi za nje. 

Akizungumzia kwa upande wa kiroho Askofu Dallu amesema kuwa katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uinjilishaji Parokia hiyo, pia imefanikiwa kuongeza idadi ya vigango toka sita na kufikia tisa, ikiwemo pia ongezeko la idadi ya waumini pamoja na ukomavu wa imani.

Pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa mapadre kujenga mazoea ya kutembelea jumuiya ndogondogo kwa ajili ya kuhamasisha wapagani kurudi kundini, waumini wanaoishi uchumba kufunga ndoa, pamoja na kuweka utaratibu wa kutengeneza bajeti ya miezi mitatu katika parokia zao ikiwa ni lengo la kuimarisha na kurahisisha utendaji wao wa kazi za kila siku.

Kwa upande wake uongozi wa Parokia ya Mbangamao wilayani Mbinga umesema wamejiwekea mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza pato la Parokia hiyo ikiwemo kuanzisha shamba la Mahindi, kahawa, miti, ufugaji wa kuku pamoja na kuhakikisha wanapunguza tatizo la watu kuishi katika hali ya upagani na uchumba.



No comments: