Tuesday, August 12, 2014

WANASIASA WANYOSHEWA KIDOLE KWA KUWATUMIA VIJANA KATIKA USHABIKI WA MAMBO YA KISIASA

Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma, Josephat Ndulango. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

Songea.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma kimewanyoshea kidole wanasiasa ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa maslahi yao binafsi, kupitia mchakato huu wa kutengeneza katiba mpya unaoendelea huko Bungeni badala yake kimewataka waachane na ushabiki wa mambo ya kisiasa, na wawatumie vijana kwa maslahi ya taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha imeelezwa kuwa utengenezaji wa katiba mpya ni jukumu la Wabunge wa bunge maalum la katiba, hivyo kwa wale waliokimbia mapambano bungeni ni kutowatendea haki wananchi na ni dhambi ambayo itaendelea kuwatafuna kila siku maishani mwao, badala yake warudi bungeni ili kuweza kumaliza misuguano inayoendelea kufukuta na kuhatarisha ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.

Katibu wa CCM wilaya ya Songea mjini, Josephat Ndulango alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Majira mjini hapa, huku akieleza kuwa vyama vya upinzani ndio vimekuwa chagizo kwa kukataa kujenga maridhiano ya pamoja juu ya mchakato huo wa kuipata katiba mpya.

“Wajibu wao mkubwa ni kwenda bungeni na kutetea maslahi ya wananchi walio wengi wanapokimbia mapambano sio suluhu, umoja wa wananchi wa katiba (UKAWA) ni muhimu warudi bungeni kutengeneza katiba mpya”, alisema Ndulango.

Alisema yeye ana amini kuwa endapo watarudi bungeni na kujenga ushirikiano wa pamoja wataweza kutengeneza katiba ya Watanzania iliyo bora, ambayo itajali misingi ya haki na ubinadamu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ndulango alisema utengenezaji wa katiba hii ni faida ya miaka 50 ijayo kwa taifa letu, hivyo isipotengenezwa misingi imara huenda likawa ni tatizo au ombwe ambalo litaendelea kuwagawa watanzania kwa namna moja au nyingine.

“Vurugu na mifarakano ya hapa na pale kwa viongozi kulumbana kila kukicha haitakiwi, kwa nini tusifikie mahali tukajenga misingi iliyo bora na yenye kuleta tija kwa wananchi wetu?” , alihoji Ndulango.

Pia alizungumzia kipengele cha haki za vijana kilichopo katika rasimu ya pili ya katiba mpya, ambapo alieleza kuwa kimekuwa na mapungufu kwa kutoeleza bayana kijana ana umuhimu gani, ni vyema wabunge wa bunge maalum la katiba wakakiweka sawa kwa sababu jamii inatambua kuwa kijana ndio mhimili na msingi mkuu wa maendeleo ya taifa hili.

Sambamba na hilo Katibu huyo wa CCM vilevile amewataka viongozi wa chama hicho wilaya ya Songea mkoani hapa, kuepukana na makundi yasiyo ya lazima badala yake kupitia mikutano ya wananchi waeleze utekelezaji wa ilani ili kuweza kujenga misingi ya kukiimarisha chama, na wananchi waweze kutambua nini kimewafanyia.

Ndulango alisema Watendaji wa serikali katika maeneo mbalimbali wilayani humo baadhi yao wamekuwa kikwazo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hivyo wamesisitizwa kuacha kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi.

Hata hivyo aliwaasa wananchi kupitia mchakato huu wa kuipata katiba mpya waache mambo ya ushabiki wa kisiasa, hivyo waelekeze nguvu zao katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.


No comments: