Friday, August 15, 2014

WAFANYABIASHARA WA MAHINDI RUVUMA WALIA NA SERIKALI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

BAADHI ya Wasafirishaji wa mazao ya nafaka mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuharakisha kulipa madeni yao ya usafirishaji wa mahindi kutoka kwenye vituo vya ununuzi na kuyafikisha kwenye kitengo cha hifadhi ya chakula (NFRA) Songea mkoani humo, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 kwa lengo la kunusuru kuuziwa mali zao na taasisi za kifedha ambako walikopa kwa ajili ya kuendeshea shughuli hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasafirishaji hao ambao ni wazawa hawakutaka majina yao yatajwe, walidai kwamba hali hiyo imewaathiri zaidi  waajiriwa waliopitia mgongo wa nyuma kufanya kazi ya usafirishaji wa zao hilo baada ya matajiri wao kuingia mkataba na NFRA.

Walisema kuwa tangu kufunguliwa kwa msimu huo Julai 15 mwaka jana wamekuwa wakiendesha shughuli hizo kwa kutegemea mikopo kutoka benki, na wengine kudaiwa na baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta ambako walikopa.


Walieleza kuwa endapo serikali haitalifanyia ufumbuzi wa haraka suala hilo shughuli ya usafirishaji wa mahindi kutoka katika vituo mbalimbali katika msimu wa mwaka huu, kuna uwezekano wa kazi hiyo kuwa ngumu kutokana na wasafirishaji hao kukosa mitaji ya kuendeshea kazi hiyo.

“Sisi tuna nia nzuri ya kufanya biashara na serikali yetu, katika kuhakikisha tunasafirisha mahindi toka kwenye vituo huko vijijini ambako miundo mbinu yake ya barabara sio mizuri na kuyapeleka kwenye kitengo cha hifadhi ya chakula Songea”,

“Lakini magari yetu yamekuwa yakiharibika mara kwa mara wakati tunafanya kazi hii, tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kutulipa mapema madeni tunayoidai ili magari yaweze kufanyiwa matengenezo na kulipa madeni tunayodaiwa ambako tulikopa”, walisema.

Kwa upande wake Meneja wa kanda kitengo cha hifadhi ya chakula (NFRA) Songea mkoani Ruvuma, Morgan Mwaipyana alikiri kuwepo kwa madai hayo huku akieleza kuwa serikali ipo mbioni kuhakikisha Wasafirishaji hao wanalipwa fedha zao mara baada ya taratibu husika kukamilika.

Mwaipyana alifafanua kuwa NFRA mpaka sasa haidaiwi na mtu yeyote zaidi ya wasafirishaji wa mazao kwa kuwa Serikali katika msimu wa mwaka 2013/2014 imeweza kulipa madeni ya wakulima na mawakala wote ambao waliuza mahindi yao katika kitengo hicho cha hifadhi ya chakula kilichopo mjini hapa.

Wadai hao walifanya kazi ya kusafirisha mahindi  hayo kutoka maeneo mbalimbali ambayo vituo vya ununuzi vilitengwa  katika wilaya ya Songea, Mbinga na Namtumbo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013.

No comments: