Sunday, August 3, 2014

DEREVA ALIYETOKOMEA KUSIKOJULIKANA BAADA YA KUSABABISHA AJALI AJISALIMISHA MIKONONI MWA POLISI

Gari hili lenye namba za usajili T 759 BVR aina ya Nissan Civillian ndilo lililopata ajali na kuua watu sita, 18 kujeruhiwa vibaya likiwa limetumbukia kwenye korongo katika kijiji cha Burma kata ya Nyoni wilayani Mbinga, wakati linaelekea wilaya ya Nyasa. (Picha na Gwiji la matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
 
DEREVA aliyetokomea kusikojulikana ambaye alisababisha ajali ya gari kutumbukia katika korongo, watu sita kufariki dunia na 18 kujeruhiwa vibaya, waliokuwa wakisafiri kwa basi kutoka Mbinga mjini kwenda wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, amejitokeza na kujisalimisha mikononi mwa Jeshi la Polisi akiwa katika hali mbaya.
 
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela amemtaja dereva huyo kuwa ni Paul Nchimbi (31) mkazi wa kijiji cha Liparamba wilayani Nyasa, ambapo wakati anajisalimisha mwili wake umejaa majeraha.
 
Mihayo alifafanua kuwa baada ya dereva huyo kupatikana kwa hiari yake na kuripoti katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga amepelekwa kwa ajili ya kupewa matibabu, hospitali ya wilaya hiyo huku akiwa chini ya ulinzi mkali.
 
Alisema atakapomaliza kupatiwa matibabu na kupona, jeshi hilo litafanya mahojiano naye ili kuweza kujua chanzo cha tukio hilo ambalo limesababisha baadhi ya Watanzania, waliokuwa wakisafiri katika basi alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T 759 BVR aina ya Nissan Civillian mali ya Dismas Ndomba mkazi wa kijiji cha Kingirikiti wilayani wilayani humo, kupata ajali katika kijiji cha Burma majira ya saa 10:30 jioni Agosti Mosi mwaka huu.    
 
Pamoja na mambo mengine Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mbinga Elisha Robert, alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi alisema majeruhi wote ambao wamelazwa katika hospitali hiyo wanaendelea vizuri isipokuwa  wagonjwa wanne wamesafirishwa kwenda hospitali ya Peramiho, iliyopo wilaya ya Songea mkoani humo kutokana na kuwa katika hali mbaya.
 
“Vilevile tumesafirisha wagonjwa wengine wawili wameenda kupatiwa matibabu hospitali ya misheni Litembo iliyopo huku Mbinga hali zao sio nzuri wamevunjika nyonga, tukaona ni vyema wapelekwe kwanza huko kwa uchunguzi zaidi wa afya zao”, alisema Dokta Elisha.
 
Awali Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Bw. Mihayo alifafanua kuwa ajali hiyo ilisababishwa na gari kuwa katika mwendo kasi, ambapo dereva aliyekuwa akiliendesha alishindwa kulimudu kwenye kona kali na hatimaye lilitumbukia katika shimo kubwa (korongo) na kusababisha mauaji na majeruhi hao.
 

No comments: