Monday, June 29, 2015

UVCCM NYASA YAWATAKA WANACHAMA WAKE KUJENGA USHIRIKIANO


Wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamekusanyika pamoja kumsikiliza Kamanda wao wa Umoja huo, Cassian Njowoka.

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Cassian Njowoka akiwa na wanachama wake wa umoja huo ambapo mbele yao kuna moja kati ya kikombe ambacho hukitoa zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mpira wa miguu katika timu mbalimbali, ambazo huendelea kushindana wilayani humo. Hapo tukio hilo lilifanyika jana katika kata ya Liuli wilayani Nyasa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

ZIARA ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, imeendelea kung’ara na kushika kasi katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kufuatia wanachama wa umoja huo kujitokeza kwa wingi katika kila eneo la mapokezi yanapofanyika.

Njowoka ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani humo, ikilenga kutembelea timu za mpira wa miguu na ambazo zinashiriki ligi kuu ya UVCCM wilayani humo, maarufu kwa jina la Njowoka Cup pamoja na kuongea na wanachama wa umoja huo.

Washiriki wa ligi hiyo amekuwa akiwapatia zawadi ya vifaa vya michezo kama vile kikombe kimoja cha ushindi, jezi seti tatu na mpira mmoja kwa mshindi wa kwanza, jezi seti mbili na mpira mmoja kwa mshindi wa pili na seti moja ya jezi kwa mshindi wa tatu.
Haya yote yanajiri kufuatia ahadi yake aliyoitoa hivi karibuni katika zoezi lake la kuwasimika makamanda wa UVCCM kwa kila kata za wilaya hiyo.

NJOWOKA AENDELEA KUFUNIKA NYASA

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Cassian Njowoka akipokelewa kwa shangwe na wanachama wa umoja huo kijiji cha Songambele kata ya Kihagara wilayani humo, wakati alipokuwa jana kwenye ziara yake ya kikazi kwa lengo la kuzungumza na wanachama hao.   

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Cassian Njowoka akizungumza jana na wanaumoja huo katika viwanja vya kijiji cha Songambele kata ya Kihagara wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, ambapo aliwataka wanachama wake kupenda kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili waweze kuondokana na umaskini.

Saturday, June 27, 2015

ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMBAKA MLEMAVU

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Na Sreven Augustino,
Songea.

NIRU Nyimbi (42) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mwombezi kilichopo kijiji cha Chandarua mkoani Ruvuma, anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mlemavu mwenye mtindio wa ubongo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, mtuhumiwa alinaswa akiwa anafanya unyama huo kijijini humo ambako imeelezwa kwamba, alikwenda kufanya kazi ya kibarua cha kufyatua tofari.

Mihayo Msikhela, Kamanda wa polisi wa mkoa huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo alifumaniwa na mama mzazi wa binti huyo aliyemtaja kwa jina la, Oresta Ndonde.

Mama huyo alifanikiwa kumkamata mtuhumiwa, baada ya kusikia sauti ya binti yake akiwa analia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata wakati anafanyiwa unyama huo.

VETA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Na Mwandishi wetu,
Songea.

ZAIDI ya vijana 60 mkoani Ruvuma, ambao hujishughulisha na kazi mbalimbali ya kuwahudumia wateja katika maeneo yao ya kazi, wamepata mafunzo ya kuwaongezea uelewa ambayo yametolewa na Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kanda ya nyanda za juu kusini, jambo ambalo litawasaidia kuleta ufanisi mzuri katika majukumu ya kazi zao za kila siku.

Kaimu Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu kusini, Suzan Magani alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao kukabiliana na changamoto mbalimbali mahali pa kazi, ambapo pia yanawaongezea uwezo wa namna ya kuwakaribisha na kuwahudumia wateja wao.

Magani alisema kuwa Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kutoa mafunzo ili kuweza kukidhi mahitaji ya sekta rasmi na isiyo rasmi, kwa lengo la kuwaongezea uwezo wadau waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na sio kwa kubahatisha, jambo ambalo linaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.

MFUGAJI ASHAMBULIWA NA SIMBA TUNDURU

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFUGAJI mwenye asili ya Mmang’ati, ambaye ametambuliwa kwa jina la Alex Poketi (22) amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, baada ya kujeruhiwa vibaya na simba wakati akiwa machungani.

Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa majeruhi huyo alipatwa na mkasa huo wakati akijitosa kuokoa maisha ya ng’ombe wake ambao walivamiwa na mnyama huyo mkali, kwa lengo la kutaka kuwafanya kitoweo.

Walisema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Mbuyuni kilichopo kando kando ya mto Ruvuma, eneo ambalo wafugaji hao wamekuwa wakichungia mifugo yao tangu mwaka 2007.

Katika eneo hilo imeelezwa kuwa, simba huyo alijitokeza ghafla na kuanza kushambulia ng’ombe hao aliokuwa akiwachunga ambapo Alex alijawa na jazba na kwenda kumrukia simba huyo kwa kumchoma mkuki, jambo ambalo lilimfanya mnyama huyo akimbie.

NYALANDU: VIONGOZI WASIOKUWA NA SIFA NI MIZIGO KWA CHAMA

Na Muhidin Amri,
Songea.

WAZIRI wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini ambao wanawania kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya urais, amewatahadharisha viongozi na wanachama wa CCM kuwa makini katika uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, ili kuepuka kuteua watu wasiokuwa na sifa ambao watakuwa mzigo kwa chama wakati utakapofika wa kuwanadi kwa wananchi.

Nyalandu alisema kuwa CCM imara itajengwa na viongozi imara waliopo madarakani, kwa kuzingatia hekima na kusimamia vizuri misingi ya haki na ukweli na kwamba pasipo kufanya hivyo wanaweza kukipeleka chama kubaya na kusababisha baadhi ya wanachama, kushindwa kukiamini tena.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwapata wadhamini kwa nafasi hiyo anayogombea.

Friday, June 26, 2015

NJOWOKA KUMALIZA KERO YA UJENZI ZAHANATI NKALACHI NYASA

Wananchi wa kijiji cha Nkalachi kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamemzunguka na kumsikiliza kwa makini Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama cha mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka wakati alipokuwa akiwahutubia.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Nkalachi kata ya Liuli wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali na wadau mbalimbali wasaidie vifaa vya kiwandani ili waweze kukamilisha ujenzi wa jengo la Zahanati ya kijiji hicho na hatimaye waondokane na kero ya kukosa huduma za matibabu.

Aidha walisema kuwa hivi sasa akina mama wajawazito na watoto wadogo wamekuwa wakifariki dunia, hasa pale wanapokuwa njiani kuelekea Hospitali ya Anglikana iliyopo wilayani humo, ambayo ipo mbali nao kwa ajili ya kutafuta matibabu.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wakazi wa kijiji hicho, mbele ya Kamanda wa Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM), Cassian Njowoka walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.

TASAF TUNDURU YAWATAKA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO


Baadhi ya Wataalamu kutoka katika kata mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika semina ya mpango wa TASAF kwa ajili ya kwenda kutoa elimu kwa wananchi vijijini.

Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameombwa kutoa ushirikiano wa kutosha juu ya hatua zote zinazotakiwa kutekelezwa pale unapofanyika upembuzi yakinifu katika matatizo yao, hasa yale yanayolenga uhifadhi wa udongo, uvunaji maji, udhibiti makorongo na kuotesha vitalu vya miti.

Aidha wametakiwa kuondokana na dhana potofu ambazo zinaenezwa na watu wasio na nia njema, kwa yale yanayofanywa katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiwa na lengo la kutaka kukwamisha maendeleo ya mpango huo, ili usiweze kuleta mafanikio katika jamii wilayani humo.

Hayo yalisemwa na Peter Lwanda ambaye ni mmoja kati ya watendaji wa mfuko huo, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa TASAF hapa nchini, Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo ya kuutambulisha juu ya kutoa ajira za muda, kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini kwenye kikao cha kazi kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya mlingoti mjini hapa.

Tuesday, June 23, 2015

NCHIMBI ATANGAZA RASMI KUTOGOMBEA JIMBO LA SONGEA MJINI

Dokta Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa CCM jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma.
Na Julius Konala,
Songea.

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Wananchi wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiangua kilio baada ya Mbunge wa jimbo hilo, Dokta Emmanuel Nchimbi kuwatamkia rasmi kuwa hatagombea tena nafasi ya kiti cha ubunge katika jimbo hilo. 

Tukio hilo lilitokea wakati Mbunge huyo, alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM kuanzia ngazi ya mashina hadi kata, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majimaji mjini hapa.

Dokta Nchimbi aliwaambia wanachama hao kuwa ameamua kuachia jimbo hilo, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka kumi jambo ambalo wanachama hao wa chama tawala, walilipokea kwa mshituko mkubwa.

HOSPITALI LITEMBO YAZINDUA SACCOS YAKE WANACHAMA WATAKIWA KUWEKA AKIBA

Katikati ni Meneja mkuu wa benki ya CRDB tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, Efrosina Mwanja akimpongeza kwa kupeana mkono na Mwenyekiti wa Chama cha ushirika Litembo SACCOS, Joseph Komba katika sherehe ya uzinduzi wa chama hicho iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Litembo iliyopo wilayani humo.


Vikundi mbalimbali vya ngoma za asili (kioda na mganda) navyo havikuwa mbali siku hiyo ya uzinduzi rasmi wa SACCOS hiyo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo, Litembo SACCOS wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuweka akiba kwa wingi jambo ambalo litawafanya waweze kukidhi mahitaji husika ndani ya chama hicho na kuepukana na tabia ya kuingia mikataba ya mikopo na taasisi za kifedha, ambazo hazijapewa dhamana ya kutoa mikopo.

Aidha wameshauriwa kwamba, endapo watahitaji kupewa mikopo hiyo ni vyema wakaingia mkataba na benki ili waweze kupewa fedha ambazo hatimaye wataweza kutoa mikopo kwa wanachama wake, na kuwafanya kusonga mbele kimaendeleo.

Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa benki ya CRDB tawi la Mbinga, Efrosina Mwanja alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya uzinduzi wa SACCOS hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Litembo, katika kata ya Litembo wilayani humo.

Thursday, June 18, 2015

MBESA TUNDURU WAPO HATARINI KUUGUA HOMA ZA MATUMBO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

UKOSEFU huduma ya uhakika ya upatikanaji wa maji safi na salama, katika kijiji cha Mbesa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kuna hatarisha wakazi wa kijiji hicho kuugua homa ya matumbo, kipindupindu na kuhara kutokana na kunywa maji machafu.

Zaidi ya wakazi 7,000 wanaoishi huko, wapo hatarini kukumbwa na madhara hayo ambapo licha ya serikali kuweka katika mpango wa ujenzi wa mradi wa maji ambao utagharimu shilingi milioni 700, utekelezaji wake mpaka sasa unaonekana ukisuasua na kuwafanya wananchi wajenge hofu juu ya usalama wa maisha yao.

Wananchi wa kijiji cha Mbesa, walipozungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti walisema kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo wamekuwa wakinywa maji machafu yaliyopo kwenye vyanzo ambavyo hata wanyama wakali kama vile simba, tembo, chuwi na nyoka wakubwa wamekuwa wakinywa maji hayo jambo ambalo linawafanya waishi kwa hofu kubwa.

Awanda Yusuph na Zuhura Said walisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 walianza kupata matumaini baada ya serikali kupitia mradi mkubwa, ambao unatekelezwa kwa ufadhili wa benki ya dunia na kumpatia kazi hiyo mkandarasi wa kampuni ya Nyakile Investment Company Limited, lakini utekelezaji wake mpaka sasa haujazaa matunda.

FUNDI MITAMBO YA KAHAWA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MBAMBI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MICHAEL Ndomba ambaye amebobea katika ufundi wa mitambo ya kukoboa kahawa mbichi na kavu, ametangaza nia ya kugombea udiwani wa kata ya Mbambi iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akiahidi kuwaletea neema wananchi wa kata hiyo.

Ndomba ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa kiwanda cha serikali cha kukoboa kahawa wilayani Mbinga (MCCCO) tokea mwaka 1988 na baadaye amestaafu mwaka huu, hivi sasa anafanya kazi ya mizani na ufundi wa kuunda mitambo ya kati ya kukoboa kahawa mbichi.

“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kujipatia maendeleo hasa katika viwanda, kilimo na ufugaji wananchi wakizalisha kwa wingi katika eneo hili wataweza kuondokana na umasikini”, alisema Ndomba.

Wednesday, June 17, 2015

UWT TUNDURU YAVUNA WANACHAMA WAPYA

Mmoja kati ya wanachama wapya wa UWT wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Winfrida Chibwana akipokea kadi ya kujiunga na Jumuiya hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wake wa mkoa wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama. (Picha Steven Augustino)
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANACHAMA wapya 200 wamejitokeza wilayani Tunduru, mkoa wa Ruvuma na kujiunga na Jumuiya ya Umoja Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wilayani humo.

Fatuma Mandingo ambaye ni Katibu wa Jumuiya hiyo wilayani humo, alisema huo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha umoja wao hasa katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mandingo alisema kuwa UWT itagawa kadi kwa wanachama wapya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru, ili kuendelea kuimarisha na kujihakikishia ushindi katika uchaguzi huo ujao ambao wanachama wa CCM watamchagua Rais, Mbunge na Diwani.

Tuesday, June 16, 2015

MANJOLO KUPEPERUSHA BENDERA JIMBO LA TUNDURU KASKAZINI

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika mkutano wa pamoja kumchagua mgombea atakayepeperusha bendera ya kuwania nafasi ya ubunge, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

CHAMA cha Wananchi CUF jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma, kimemteua Manjolo Dastan Kambili kupeperusha bendera ya chama hicho katika kuwania nafasi ya ubunge, kwenye jimbo hilo.

Maamuzi hayo yalifanywa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, katika uteuzi uliofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu, tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo kutoka makao makuu ya CUF taifa, Abudrahaman Lugone alisema Kambili ameshinda baada ya kupata kura 147 kati ya kura 396 zilizopigwa na kuwabwaga, washindani wake.

Alisema katika kinyang’anyiro hicho jumla ya wagombea watano, walijitokeza kuwania nafasi hiyo ambapo nafasi ya pili ilichukuliwa na Kindamba Mamlia ambaye alipata kura 102, Mohamed Abdallah kura 73, Issa Mtuwa kura 68 na Issa Kapukusu aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kupata kura 2.

Monday, June 15, 2015

UWT YAWATAKA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Manduzi Tanzania (UWT) mkoa  wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama akizungumza na wananchi wilayani Tunduru mkoani humo, (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya baraza la Idd wilayani humo.
Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANAWAKE mkoani Ruvuma, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi mkoani humo ili kuweza kufikia malengo ya hamsini kwa hamsini, katika kuongoza jamii.

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) mkoani humo imewataka wanawake kufanya hivyo, kwa kuunganisha nguvu pamoja na kuacha tabia ya kubezana au kupakana matope kwamba mtu fulani hatoshi.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Ruvuma, Kuruthum Mhagama katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya baraza la Idd wilayani Tunduru.

Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, kitaibuka na ushindi wa kishindo hivyo wanachama wa UWT wametakiwa kuendelea kukisemea vizuri chama hicho, hasa kwa yale yaliyotekelezwa kupitia ilani yake.

Sunday, June 14, 2015

FUNDIMBANGA TUNDURU WAIOMBA SERIKALI KUWAONGEZEA MRADI


Afisa mifugo wa kata ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Tatu Omary Tururu akisoma risala ya wanakikundi cha ufugaji ng'ombe wa maziwa katika hafla ya kuwapongeza wanakikundi hao kwa kufanya vizuri katika mradi wao, iliyofanyika kijiji cha Fundimbanga wilayani humo. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

KIKUNDI cha ufugaji ng’ombe wa maziwa kilichopo katika kijiji cha Fundimbanga Tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kujenga ubunifu juu ya taratibu za ufugaji huo, ambao umeweza kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na waweze kuondokana na umasikini.

Pamoja na pongezi hizo, wanachama wa kikundi hicho wameiomba pia serikali kuangalia uwezekano wa kuwapelekea miradi mingine kama vile ufugaji wa samaki na kuku, huku wakiitaka Halmashauri ya wilaya hiyo iwasaidie kuwajengea josho litakalosaidia kuogeshea mifugo yao.

Hayo yalisemwa kupitia risala yao ambayo ilisomwa na afisa mifugo wa kata ya Matemanga, Tatu Tururu na kuongeza kuwa kijiji cha Fundimbanga kilipokea mradi wa ng’ombe wa maziwa 20 wenye thamani ya shilingi milioni 16 uliotolewa kwa ufadhili wa mpango wa DADPs, kupitia Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mwaka 2012.

Saturday, June 13, 2015

MAKAMBA APONGEZA UJENZI WA BARABARA RUVUMA


Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho akiwakaribisha jana mkoani humo Mheshimiwa January Makamba na mkewe Ramona Makamba wakati walipokuwa wamewasili kwenye ofisi za CCM mkoani hapa.
Na Muhidin Amri,
Songea.

NAIBU Waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia January Makamba, amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa  uamuzi wake  wa kujenga barabara za mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami hatua ambayo imewezesha kuharakisha shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo.

Barabara hiyo ni ile ya kutoka Songea hadi Mbinga yenye kilometa 96, Songea kwenda Namtumbo kilometa 76 na  barabara ya Namtumbo hadi Tunduru yenye zaidi ya kilometa 220 ambayo ujenzi wake unaendelea.

Makamba ametoa pongezi hizo jana wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani  humo, baada ya kukamilisha zoezi la kutafuta wadhamini katika jitihada zake za kuomba ridhaa ya chama hicho, kumsimamisha ili  aweze kupeperusha bendera ya kugombea  Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini mgombea huyo.

Friday, June 12, 2015

JANUARY MAKAMBA: KUPAKANA MATOPE TUNAJIWEKA KATIKA WAKATI MGUMU


January Makamba akiwa katika taswira tofauti za mapokezi na mkewe Ramona Makamba, leo mjini Songea mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JANUARY Makamba, ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli amewataka makada wote wlioomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais hapa nchini, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) endapo kama hawana dhamira ya dhati waache kugombea nafasi hiyo, badala yake wakiache chama kikiwa salama baada ya kukamilika kwa mchakato huo.

Makamba alisema hayo leo mjini Songea mkoani Ruvuma, mara baada ya kupokea orodha ya wanachama wa chama hicho ambao walijitokeza kumdhamini ambapo jumla ya wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini, katika nafasi hiyo.

Alieleza kuwa kuna watu wameomba kugombea nafasi hiyo nyeti, huku akidai kuwa baadhi yao hawana sifa na endapo hawatateuliwa, kuna hatari ya kukisambaratisha chama hicho.

Mbunge huyo alifafanua kuwa CCM kinahitaji kupata mgombea ambaye atahakikisha chama hicho kinabaki salama na kuwaongoza Watanzania, bila kujali itikadi ya dini, rangi au kabila huku akijisifia kuwa yeye ndiye mwenye uwezo wa kushika nafasi hiyo.

MAJERUHI ALIYEPATA AJALI KIGONSERA GARI KUTEKETEA KWA MOTO AFARIKI DUNIA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MWANAFUNZI wa shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) Regoberthy Mahay (16) ambaye ni mmoja kati ya majeruhi wanne waliolazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, baada ya kupata ajali na wanafunzi wenzake katika gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye korongo kisha kuteketea kwa moto, kitongoji cha Minazi kata ya Kigonsera wilayani humo, amefariki dunia.

Marehemu Regoberthy amefariki Juni 10 mwaka huu, majira ya saa 9 usiku baada ya kuzidiwa ghafla na kwamba mwili wake umesafirishwa kwenda kijiji cha Mpepo wilayani humo, kwa ajili ya mazishi.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Roberth Elisha alithibitisha kufariki kwa mtoto huyo na kueleza kuwa hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri, lakini kufikia majira hayo ya usiku alizidiwa ghafla kutokana na kushindwa kupumua ipasavyo.

MWANAFUNZI AGONGWA NA GARI AFARIKI DUNIA

Na Steven Augustino,
Songea.

MWANAFUNZI Vicent Baisi (13) anayesoma katika shule ya sekondari Ruhila, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari.

Gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili SM 8685 mali ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, mkoani humo ndilo lilimgonga mtoto huyo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, marehemu huyo aligongwa na gari hilo wakati alipokuwa akijaribu kuvuka barabara ambapo tukio hilo, lilitokea Juni 9 mwaka huu majira ya jioni.

MGAWO WA UMEME WAENDELEA KULETA KERO SONGEA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Muhidin Amri,
Songea.

WAKATI serikali ikiendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme katika baadhi ya maeneo hapa nchini, wakazi na wafanyabiashara waishio katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamesema tatizo hilo limekuwa sugu kwao kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo muhimu, hivyo serikali inapaswa kulitatua kwa haraka iwezekanavyo, ili kuweza kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, mmoja wa wafanyabiashara ambaye alijitambulisha kwa jina la Said Athuman alisema kwamba kutokana na kutokuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Manispaa hiyo wananchi wanaendelea kuteseka, juu ya uzalishaji wa bidhaa pamoja na shughuli mbalimbali za kimaendeleo zimeanza kushuka.

Alisema kuwa tatizo hilo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu sasa, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua madhubuti ambayo itasaidia kumaliza kero hiyo.

Wednesday, June 10, 2015

MWENYEKITI CCM MKOA WA RUVUMA AVAMIWA NA CHADEMA KATIKA KATA YAKE

Mathayo Kaimaima.
Na Stephano Mango,
Nyasa.

KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Mathayo Kaimaima ametangaza nia yake ya kuchukua fomu ya kugombea udiwani katika kata ya Chiwanda wilayani humo, ambayo kata hiyo kwa sasa inaongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Oddo Mwisho.

Mwisho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, ameeleza kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka kufanya mabadiliko ya kweli kwa kumpata kiongozi mwingine wa kutoka chama cha upinzani, ambaye ataweza kuleta ushirikiano wa karibu katika kusukuma mbele maendeleo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimaima alisema kuwa amechukua maamuzi hayo baada ya kuona kwamba wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo diwani aliyekuwa madarakani na ambaye anaelekea kumaliza muda wake, ameshindwa kutatua kero husika na kuwafanya wananchi waendelee kuwa maskini.

MKUU WA SHULE SEKONDARI NANUNGU ADAIWA KUKWAMISHA UJENZI WA MAABARA

Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.

MOHAMED Ngonyani, ambaye ni Mkuu wa shule ya sekondari Nanungu kata ya Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, analalamikiwa akidaiwa kukwamisha ujenzi wa jengo la maabara kutokana na kuzuia kiasi cha shilingi milioni 1,330,000 ambacho alipaswa kulipa mafundi wanaojenga jengo hilo, licha ya kamati husika ya ujenzi kuidhinisha malipo hayo.

Fedha hizo ni kati ya shilingi milioni 3,500,000 zilizopo katika mkataba wa ujenzi kati ya Mkuu wa shule na fundi mkuu anayesimamia ujenzi huo, George Mbeya akisaidiana na watu wengine ambapo jengo hilo kwa ujenzi wake umesimama kutokana na kuwepo kwacmgogoro huo na limefikia katika hatua ya kuezeka.

Kufuatia hali hiyo Ngonyani ametishia kuchukua hatua dhidi ya kamati husika ya ujenzi, ili kuondoa adha anayoendelea kuipata na kumfanya ashindwe kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

NAMTUMBO WAJIVUNIA MAFANIKIO KATIKA KILIMO

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amesema wakulima waliopo katika wilaya hiyo wanatarajia kupata mavuno mengi ambayo wameyazalisha katika mashamba yao, katika msimu wa mwaka huu 2015/2016 kufuatia wakulima hao kutumia vyema mvua zilizonyesha na kuzingatia maelekezo waliyopewa na wataalamu wa ugani wilayani humo.

Nalicho alifafanua kuwa matunda ya kuwa na wataalamu wa kutosha na wenye kuwajibika kwa wananchi ipasavyo, ndiyo njia pekee iliyochangia wakulima kuwa na hamasa ya kuzalisha mazao ya biashara na chakula kwa wingi huku akiwataka watendaji wengine wa idara za Halmashauri wilaya ya Namtumbo, kuiga mfano huo kutoka kwa wenzao wa idara ya kilimo wilayani humo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, tangu mpango huo wa kilimo uanze kuboreshwa hapa nchini, wilaya ilijiwekea mikakati madhubuti ambayo inatekelezwa na maafisa kilimo kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba mazao yanazalishwa kwa wingi na yenye ubora.

UTEKELEZAJI WA TASAF TUNDURU WADAIWA KUWA MWIBA KWA WANUFAIKA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

TAARIFA potofu kuhusu utekelezaji wa mpango wa uhawilishaji fedha ili kuziwezesha kaya maskini kujikimu kiuchumi, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, unadaiwa kuendelea kuwa mwiba kwa wanufaika hali ambayo inawafanywa kushindwa kubuni mikakati ya kujiendeleza, kupitia mfuko huo.

“Ingawa wataalamu wetu wamekuwa wakitupatia elimu ya kujikwamua na umaskini kupitia vikundi vyetu vya ujasiriamali, ambavyo tunawekeza katika vikundi vya Mpeano miongoni mwetu wamekuwa wakiogopa kujiunga na vikundi hivi kutokana na kuhofia kuwa huenda mpango huo, utakwisha kabla hawajamaliza mzunguko wa mpeano wao kwa sababu chanzo ni uwepo wa taarifa potofu hivyo familia zao kukosa uwezeshaji huo”, walisema.

Hayo na mengine mengi yalibainika kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu, wakati waratibu husika wa mpango huo wilayani humo wakiwajibika kuelimisha wananchi wakati wa malipo ya fedha, kwa walengwa waliokuwemo kwenye mpango huo katika vijiji vilivyomo wilayani humo.

WAZIRI MEMBE AVUNA WADHAMINI MKOANI RUVUMA, AZUNGUMZIA VIPAUMBELE VYAKE ATAKAPOINGIA IKULU

Waziri Bernad Membe akipokelewa jana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wakati alipowasili katika Ofisi za makao makuu ya CCM mkoani humo zilizopo katika Manispaa ya Songea.

Upande wa kushoto, Waziri Bernad Membe akikabidhiwa fomu ya watu ambao wamemdhamini mkoani Ruvuma katika harakati zake za kutaka kugombea Urais. Anayemkabidhi fomu hiyo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Oddo Mwisho.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernad Membe amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitampa ridhaa ya kugombea nafasi ya Urais na kushinda katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu jambo la kwanza atakalolifanya kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, ni kujenga viwanda vingi vitakavyosaidia kusindika vyakula kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa mkoani humo, ili wakulima wake waweze kukua kiuchumi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri Membe alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa CCM, alipokuwa katika harakati zake za kutafuta wadhamini ndani ya chama hicho mkoani hapa, ambapo zaidi ya wanachama 5600 walijitokeza kumdhamini mgombea huyo wa Urais.

“Namuomba sana Mungu endapo chama changu kitanipa ridhaa ya kupeperusha bendera na hatimaye kushinda nafasi hii mwezi Oktoba, basi jambo la kwanza nitakalowafanyia ndugu zangu wanaruvuma ni kujenga viwanda ili vyakula vinavyolimwa hapa kwetu, viweze kusindikwa katika ubora unaokubalika”, alisema Waziri Membe.

Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kutowaogopa wagombea wengine, ambao wameonesha dhamira ya kugombea urais kupitia tiketi ya CCM.

Waziri Membe alisema wanachopaswa ni kuwauliza maswali juu ya uadilifu na uwajibikaji wao, kwa wananchi hatua itakayowawezesha kutambua nani anafaa kusimamishwa na kugombea katika kinyang’anyiro hicho.

HOKORORO AWATAKA VIONGOZI TUNDURU KUSAIDIA WANANCHI

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo amewataka wakuu wa idara waliopo katika wilaya hiyo kujipanga na kuanza kufanya kazi kwa weledi, ili waweze kuwasaidia wananchi wasonge mbele kimaendeleo.

Alisema kiongozi yoyote aliyepewa dhamana ya kuwaongoza wananchi wake, endapo kama anakuwa ni mtu wa kufanya kazi kwa mazoea bila kushirikisha jamii, ni hatari kwa ustawi wa maendeleo katika eneo husika.

Hokororo alisema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi hao, katika makabidhiano kati yake na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho ambaye anahamia wilaya ya Namtumbo, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza kujenga ushirikiano hasa pale atakapohitaji ushauri na maelekezo wakati akitekeleza majukumu yake.

MGOGORO WA WAFUGAJI WANUKIA TUNDURU


Baadhi ya wafugaji wakiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, walikwenda huko kwa lengo la kupinga tukio la kufukuzwa na kuhamishwa katika maeneo wanayofugia. 


Mfugaji wa jamii ya kisukuma ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake, akiwa na mifugo yake katika kijiji cha Masonya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. (Picha zote na Steven Augustino)
Na Mwandishi wetu,

Tunduru.

SERIKALI imeombwa kutengeneza utaratibu wa kudumu, wa kuijengea sekta ya ufugaji miundombinu ya uhakika jambo ambalo litaifanya iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa, tofauti na ilivyo sasa sekta hiyo imekuwa ikichangia wastani wa asilimia 6 tu, kiasi ambacho  imeelezwa kuwa  ni kidogo.

Hayo yalibainishwa na wafugaji waliopo katika maeneo mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakati walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho pamoja na Mkurugenzi mtendaji, Tina Sekambo wakati wakipinga amri ya kuondolewa katika maeneo ya vijiji wanavyoishi na kufanyia shughuli za ufugaji.

Wafugaji hao walisema, ni jambo la muhimu kwa serikali kutilia mkazo juu ya maoni yao, ikiwemo kuacha tabia ya kunyanyasa wafugaji ili kuweza kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.
                    
Rugwashi Mtegwambuli na Leleshi Latu ni miongoni mwa wazee wafugaji, ambao walivunja ukimya na kuilalamikia serikali kuwa hali hiyo inatokana na kutotekeleza makubaliano husika, huku akisema kuwa serikali imewasahau wafugaji na kuwafanya kama sio watanzania ambao wanapaswa kuishi na kupewa haki zao za msingi, kama ilivyo kwa watu wengine.

MWANDISHI WA HABARI MAJIRA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UDIWANI

Cresensia Kapinga.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

CRESENSIA Kapinga (42) ambaye ni mwandishi wa habari, gazeti la Majira mkoani Ruvuma ametangaza nia yake ya kugombea nafasi ya udiwani, katika kata ya Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani humo, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kapinga ameweka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa ya kuwaongoza, kwamba atahakikisha huduma zifuatazo zinaboreshwa kwa wananchi wake ambavyo ni elimu, afya, maji na miundombinu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, Kapinga alieleza kuwa dhamira ya kugombea katika kata hiyo alikuwa nayo tokea muda mrefu, ambapo katika uchaguzi mkuu uliyopita mwaka 2010 aliwahi kugombea nafasi hiyo kupitia viti maalum, lakini kura hazikutosha na sasa amerudi tena.

Tuesday, June 9, 2015

PADRI ALIYEFARIKI AJALINI AZIKWA

Gari hili ndilo walilopata nalo ajali Wanafunzi na Padri wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAUMINI wa madhehebu mbalimbali ya dini wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, kufuatia ajali ya gari lililoteketea kwa moto na kusababisha baadhi ya wanafunzi na Padri wa kanisa katoliki wilayani humo, kufariki dunia.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, John Ndimbo wakati alipokuwa akiongoza ibada ya mazishi ya Padri Hyasint Kawonga ambaye alifariki dunia, kwenye ajali hiyo na kusababisha vifo vya watu saba wakiwemo wanafunzi sita, Padri huyo na majeruhi 24.

Wanafunzi wanaosoma katika shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) iliyopo katika kata ya Kigonsera, akiwemo na Padri Kawonga ambaye ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Parokia ya Kigonsera katika jimbo hilo walipoteza maisha baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kutumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto.

Saturday, June 6, 2015

TUWEMACHO TUNDURU KUJENGEWA ZAHANATI NA TASAF

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MFUKO wa maendeleo ya jamii (TASAF) awamu ya tatu ambao kwa sasa unatekeleza mradi wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini hapa nchini, umeridhia ombi la kugharimia ujenzi wa zahanati, katika kijiji cha Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Hayo yamefuatia baada ya makubaliano yaliyofanyika, kati ya viongozi wa mfuko huo na wananchi walioshiriki kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, ambao ulilenga kuibua mradi huo na ujenzi wake kugharimu zaidi ya shilingi milioni 75.

Kwa mujibu wa wananchi waliokuwepo katika mkutano huo, kwa nyakati tofauti walipendekeza pia wajengewe mradi wa maji, nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, matundu ya choo na ghala la kuhifadhia mazao.

Thursday, June 4, 2015

PADRI KANISA KATOLIKI NA WANAFUNZI SABA WAFARIKI DUNIA BAADA YA GARI WALILOKUWA WAKISAFIRIA KUTEKETEA KWA MOTO

 
Gari likiwa limetumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) iliyopo katika kata ya Kigonsera, akiwemo na Padri wa Parokia ya Kigonsera kanisa katoliki jimbo la Mbinga, mkoani Ruvuma wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kutumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto.

Wanafunzi sita na Padri Hyasint Kawonga ndiyo waliopoteza maisha katika ajali hiyo, wakati wakitoka shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo.

Padri Kawonga ndiye Mkurugenzi wa shule hiyo, ambapo gari lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya Land rover ndilo walilopata nalo ajali, baada ya gari hilo kushindwa kupanda mlima wakati wanatoka huko shambani.

Tukio hilo lilitokea katika eneo la Minazi kata ya Kigonsera wilayani humo, Juni 4 mwaka huu majira ya jioni ambapo baada ya kushindwa kupanda mlima katika eneo hilo, lilirudi nyuma na kutumbukia kwenye korongo kisha kuwaka moto huku ndani ya gari wakiwa wanafunzi na padri huyo.

WAFUASI WA CHADEMA MBINGA WAFIKISHWA POLISI KWA KULETA VURUGU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imewataka wanachama wa umoja huo kutojihusisha na vitendo vya vurugu hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu, badala yake watumie muda mwingi kuelezea utekelezaji wa ilani wa chama hicho, ulivyofanikiwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Hayo yalisemwa na Mhamasishaji na chipukizi wa UVCCM wa wilaya hiyo, Emmanuel Mapunda kufuatia vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye mkutano wa hadhara, eneo la Soko kuu Mbinga mjini Mei 31 mwaka huu.

Mapunda alisema kuwa vurugu za wafuasi hao, ambazo walizifanya wakati mkutano huo ukiendelea zilisababisha madhara ya kuumizwa kwa baadhi ya wanachama wa CCM.

WANANCHI TUNDURU WAUKATAA MRADI VIONGOZI WAZOMEWA

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANANCHI wa kijiji cha Misechela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamekataa kuupokea mradi wa Uhifadhi Shirikishi wa Misitu (USM) ambao ulipangwa kutekelezwa kati yao na shirika la WWF, kutokana na madai waliyoyatoa kwamba wanahofia kunyimwa uhuru endapo mradi huo utakuwa umeanzishwa katika misitu yao.

Sambamba na kuukataa huko, wananchi hao walieleza kuwa endapo wataendela kuwalazimisha kuanzisha mradi huo kwa mabavu, wapo tayari kuchangishana fedha kwa ajili ya kupata nauli na kuteuana miongoni mwao kwenda kufikisha malalamiko yao kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Hayo yalisemwa na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kijiji hicho ambapo waliyasema mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho.

Walimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa, hawapo tayari kuupokea kwa kile walichodai kuwa uzoefu unaonesha kwamba wafadhili wa miradi ya aina hiyo wamekuwa wakienda kwa wananchi na maneno mazuri, lakini mwisho wa siku baada ya kuwapokea kwa mikono miwili, huwageuka na kuanza kuwanyanyasa wenyeji wao.