Saturday, June 13, 2015

MAKAMBA APONGEZA UJENZI WA BARABARA RUVUMA


Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho akiwakaribisha jana mkoani humo Mheshimiwa January Makamba na mkewe Ramona Makamba wakati walipokuwa wamewasili kwenye ofisi za CCM mkoani hapa.
Na Muhidin Amri,
Songea.

NAIBU Waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia January Makamba, amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa  uamuzi wake  wa kujenga barabara za mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami hatua ambayo imewezesha kuharakisha shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo.

Barabara hiyo ni ile ya kutoka Songea hadi Mbinga yenye kilometa 96, Songea kwenda Namtumbo kilometa 76 na  barabara ya Namtumbo hadi Tunduru yenye zaidi ya kilometa 220 ambayo ujenzi wake unaendelea.

Makamba ametoa pongezi hizo jana wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani  humo, baada ya kukamilisha zoezi la kutafuta wadhamini katika jitihada zake za kuomba ridhaa ya chama hicho, kumsimamisha ili  aweze kupeperusha bendera ya kugombea  Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini mgombea huyo.


Makamba sasa ni mgombea wa tatu sasa kwa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi  kufika mkoani Ruvuma, kuomba udhamini akitanguliwa na wagombea wengine ambao ni Makongoro Nyerere na Waziri wa Mambo ya nchi za nje, Bernard Membe.

Makamba alisema kuwa kazi aliyoifanya Rais Kikwete ya kujenga barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami, ni jambo la kupongezwa hasa ikizingatia kuwa mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa michache hapa nchini, inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula ambapo aliahidi kama atapata nafasi ya urais ataendeleza mambo mazuri aliyoacha Rais Kikwete, wakati wa utawala wake.

Aidha alifafanua kuwa endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao na kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha anajenga Reli kutoka Mtwara hadi Mbamba bay na mji wa Songea  kuufanya ndiyo kituo kikubwa cha reli hiyo, kutokana na umuhimu wake kiuchumi.

Kwa mujibu wa mgombea huyo wa chama hicho tawala, alieleza kuwa wakazi wa Ruvuma wamekuwa wakifanya vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara hata hivyo ni jambo la kusikitisha kuona kiasi kikubwa cha mazao  hayo, bado yanaozea shambani au majumbani kwani hakuna soko la uhakika kwa wakulima hao.

Ameahidi kama atabahatika kupata ridhaa ya wananchi kuingia Ikulu basi atajitahidi kuweka mfumo mzuri ambao utamwezesha mkulima anapopeleka mazao yake sokoni, analipwa fedha yake badala ya kukopwa jambo hilo limekuwa likiwaumiza wakulima na kusababisha kuwa masikini.

Aidha amewataka wagombea wengine katika nafasi hiyo kufanya kampeni zao kistaarabu na kuacha tabia ya kuwachafua wengine, kwa sababu kufanya hivyo ni kukichafua CCM kwa kuwa hata yule atakayechaguliwa bado ataonekana ana mapungufu makubwa na hana sifa ya kuwaongoza watanzania.

“Kama kuna jambo linaloniuma ndani ya chama chetu wakati huu wa kutafuta wadhamini ni tabia ya baadhi ya wagombea wenzangu kuchafuana hali hii haileti picha nzuri, mwisho wa siku atapatikana mgombea mmoja ambaye ni lazima wote tutamuunga mkono”, alisema Makamba.

Alisema kati ya wagombea wote waliojitokeza na kuchukua fomu ya kutaka urais kupitia tiketi ya Chama cha mapinduzi ni yeye tu ndiye mwenye sifa ya kuwaongoza watanzania kwani amezaliwa, kukua, kulelewa na kufanya kazi ndani ya chama hicho kwa hiyo ana uzoefu mkubwa katika kuwatumikia wananchi.

Kadhalika aliongeza kuwa Watanzania ni lazima waelewe kwamba hivi sasa nchi inahitaji mabadiliko ya uongozi  utakaokuwa tayari, kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani na nje ya chama na kamwe wasikubali kurubuniwa na watu wanaotaka uongozi kwa kutumia nguvu kubwa ya fedha au kuwakashifu wenzao.

No comments: