Tuesday, June 16, 2015

MANJOLO KUPEPERUSHA BENDERA JIMBO LA TUNDURU KASKAZINI

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika mkutano wa pamoja kumchagua mgombea atakayepeperusha bendera ya kuwania nafasi ya ubunge, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

CHAMA cha Wananchi CUF jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma, kimemteua Manjolo Dastan Kambili kupeperusha bendera ya chama hicho katika kuwania nafasi ya ubunge, kwenye jimbo hilo.

Maamuzi hayo yalifanywa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, katika uteuzi uliofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu, tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo kutoka makao makuu ya CUF taifa, Abudrahaman Lugone alisema Kambili ameshinda baada ya kupata kura 147 kati ya kura 396 zilizopigwa na kuwabwaga, washindani wake.

Alisema katika kinyang’anyiro hicho jumla ya wagombea watano, walijitokeza kuwania nafasi hiyo ambapo nafasi ya pili ilichukuliwa na Kindamba Mamlia ambaye alipata kura 102, Mohamed Abdallah kura 73, Issa Mtuwa kura 68 na Issa Kapukusu aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kupata kura 2.


Mkutano huo pia ulipitisha jina la Zuhura Kanduru kuwa mgombea mwenza katika nafasi hiyo, na endapo Manjolo ataibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi mkuu ujao basi Chipola, atakuwa Mbunge wa viti maalum katika jimbo hilo.

Alipozungumza na waandishi wa habari, Manjolo aliwaomba wananchi wa jimbo la Tunduru Kaskazini kumpatia ridhaa ya kuwaongoza ili aweze kusimamia maendeleo ya wananchi katika nyanja ya elimu, afya, barabara na maji.

Mgombea huyo, pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wapinzani wake walioshindwa katika uteuzi huo kuvunja makundi na kumuunga mkono ili kukiwezesha chama chao kuibuka na ushindi, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.


Awali akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa chama hicho cha wananchi CUF wilaya ya Tunduru, Abdalah Mtalika aliwataka wajumbe kuacha maneno yenye ushabiki kwani kiongozi waliyemchagua wanapaswa kujenga ushirikiano naye, ili kuweza kufikia malengo husika.

No comments: