Saturday, June 27, 2015

VETA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Na Mwandishi wetu,
Songea.

ZAIDI ya vijana 60 mkoani Ruvuma, ambao hujishughulisha na kazi mbalimbali ya kuwahudumia wateja katika maeneo yao ya kazi, wamepata mafunzo ya kuwaongezea uelewa ambayo yametolewa na Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kanda ya nyanda za juu kusini, jambo ambalo litawasaidia kuleta ufanisi mzuri katika majukumu ya kazi zao za kila siku.

Kaimu Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu kusini, Suzan Magani alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao kukabiliana na changamoto mbalimbali mahali pa kazi, ambapo pia yanawaongezea uwezo wa namna ya kuwakaribisha na kuwahudumia wateja wao.

Magani alisema kuwa Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kutoa mafunzo ili kuweza kukidhi mahitaji ya sekta rasmi na isiyo rasmi, kwa lengo la kuwaongezea uwezo wadau waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na sio kwa kubahatisha, jambo ambalo linaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.


Alisema katika kutoa mafunzo hayo kwenye sekta isiyo rasmi, wamekuwa wakijenga ushirikiano na wadau hao kwa lengo la kutambua mahitaji kwa kundi husika, kisha kuwapa mafunzo ikiwemo kozi ya kuwahudumia wateja wao.

Kozi hizo zinazotolewa hulipiwa na VETA yenyewe na washiriki hulazimika kulipa kiasi kidogo cha gharama, ikiwa ni lengo la kutoa nafasi ya kuweza kuwapata washiriki wengi na kuisaidia serikali katika kupunguza tatizo la ajira hapa nchini.

Mbali na hayo, lengo lingine ni kutaka kuwawezesha wanaofanya kazi kupata stadi wanazohitaji kwa kuboresha huduma wanazozitoa katika jamii, ili kuongeza kipato chao.

Kwa upande wake mkufunzi, Gosbert Kakiziba alifafanua kuwa mafunzo hayo ya kuwawezesha wadau wa huduma kwa wateja ndani ya Mamlaka hiyo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara ambapo sasa ni takribani miaka miwili imepita, yalikwisha fanyika katika mkoa wa Njombe na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.


“Lengo halisi la kutoa mafunzo haya, ni kuwawezesha watu wa kawaida kutambua fursa ya kukuza biashara na kuwafanya wakue kiuchumi na hatimaye taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo”, alisema Gosbert.

No comments: