Wednesday, June 10, 2015

MWANDISHI WA HABARI MAJIRA ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UDIWANI

Cresensia Kapinga.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

CRESENSIA Kapinga (42) ambaye ni mwandishi wa habari, gazeti la Majira mkoani Ruvuma ametangaza nia yake ya kugombea nafasi ya udiwani, katika kata ya Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani humo, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kapinga ameweka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa ya kuwaongoza, kwamba atahakikisha huduma zifuatazo zinaboreshwa kwa wananchi wake ambavyo ni elimu, afya, maji na miundombinu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, Kapinga alieleza kuwa dhamira ya kugombea katika kata hiyo alikuwa nayo tokea muda mrefu, ambapo katika uchaguzi mkuu uliyopita mwaka 2010 aliwahi kugombea nafasi hiyo kupitia viti maalum, lakini kura hazikutosha na sasa amerudi tena.


Alisema anaamini kwamba atashinda kwa kishindo kutokana na vijana na wazee wa kata hiy,o kumpatia baraka kuwa wanamuhitaji agombee kwenye kata ili aweze kuwaletea mabadiliko.

Alifafanua kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kugombea nafasi hiyo, ilitokana na maombi ya wananchi wa kata ya Ndilimalitembo ambao kwa muda mrefu wamechoshwa na viongozi waliokuwepo madarakani kutoa ahadi ambazo hawazitekelezi, licha ya ukweli kwamba kata hiyo ni moja kati ya sehemu ambayo inawasomi wengi akiwemo Waziri wa nchi, Sera na Bunge Jenista Mhagama.

“Wananchi wameniomba nigombee katika nafasi hii, ili niweze kuwa mwakilishi wao katika baraza la madiwani Manispaa ya Songea kwa kuwazungumzia matatizo yao ya kimaendeleo ndani ya kata, ili niweze kusaidia kuyasukuma mbele na mwisho wa siku waondokane na adha wanazoendelea kuteseka nazo”, alisema Kapinga.

Alisema hivi sasa wananchi wa kata hiyo wanachohitaji ni kuona mabadiliko makubwa ya kiuongozi ambayo wanaimani kufanya hivyo itasaidia kuboresha maisha yao, kwa kile walichoeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona licha ya wao kuwa wachapakazi lakini tokea kata hiyo ianzishwe hawajajengewa hata zahanati au soko jambo ambalo lingewafanya wapige hatua.


Kukosekana kwa huduma hizo muhimu, kunasababisha wananchi hao wateseke kwa kuzifuata umbali mrefu na endapo zingekuwa jirani nao wangeweza kuondokana na kero hiyo.

No comments: