Wednesday, June 10, 2015

WAZIRI MEMBE AVUNA WADHAMINI MKOANI RUVUMA, AZUNGUMZIA VIPAUMBELE VYAKE ATAKAPOINGIA IKULU

Waziri Bernad Membe akipokelewa jana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wakati alipowasili katika Ofisi za makao makuu ya CCM mkoani humo zilizopo katika Manispaa ya Songea.

Upande wa kushoto, Waziri Bernad Membe akikabidhiwa fomu ya watu ambao wamemdhamini mkoani Ruvuma katika harakati zake za kutaka kugombea Urais. Anayemkabidhi fomu hiyo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Oddo Mwisho.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAZIRI wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernad Membe amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitampa ridhaa ya kugombea nafasi ya Urais na kushinda katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu jambo la kwanza atakalolifanya kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, ni kujenga viwanda vingi vitakavyosaidia kusindika vyakula kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa mkoani humo, ili wakulima wake waweze kukua kiuchumi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri Membe alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa CCM, alipokuwa katika harakati zake za kutafuta wadhamini ndani ya chama hicho mkoani hapa, ambapo zaidi ya wanachama 5600 walijitokeza kumdhamini mgombea huyo wa Urais.

“Namuomba sana Mungu endapo chama changu kitanipa ridhaa ya kupeperusha bendera na hatimaye kushinda nafasi hii mwezi Oktoba, basi jambo la kwanza nitakalowafanyia ndugu zangu wanaruvuma ni kujenga viwanda ili vyakula vinavyolimwa hapa kwetu, viweze kusindikwa katika ubora unaokubalika”, alisema Waziri Membe.

Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kutowaogopa wagombea wengine, ambao wameonesha dhamira ya kugombea urais kupitia tiketi ya CCM.

Waziri Membe alisema wanachopaswa ni kuwauliza maswali juu ya uadilifu na uwajibikaji wao, kwa wananchi hatua itakayowawezesha kutambua nani anafaa kusimamishwa na kugombea katika kinyang’anyiro hicho.


Kwa mujibu wa kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi, alisema nafasi hiyo ya urais ni kubwa kuliko nafasi nyingine za uongozi hivyo sio ya kuifanyia majaribio hasa pale linapokuja suala la mahusiano ya kimataifa, ambapo wagombea wote wanaotaka kuchaguliwa na chama hicho na hata wale watakaochaguliwa na vyama vya upinzani ni yeye tu ndiye mwenye sifa hiyo, ikilinganishwa na wenzake waliotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.

Alisema baadhi ya wagombea wamekuwa mabingwa wa kuzungumza na kutoa kauli zenye maneno matamu, yenye kuwavutia wanachama na wananchi kwa ujumla ili wa wachague huku akisema wananchi wanapaswa kuwapuuza kwani hawana jipya kutokana na utendaji wao mbovu walipokuwa watendaji wa umma, huku akiongeza kuwa itakuwa sio vyema kuwapa ridhaa ya kuongoza nchi hii inayobeba maisha ya Watanzania karibu milioni 48.

Akizungumza na umati wa wananchi nje ya ukumbi wa makao makuu ya CCM mkoani Ruvuma uliopo mjini Songea, ambao walikusanyika kumpokea mara baada ya kumaliza zoezi la kutafuta wadhamini katika mkoa huo, Waziri Membe alisema endapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha pia nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote wa utawala wake, ili kutoa nafasi kwa wananchi waweze kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo bila usumbufu wa aina yoyote ile katika maeneo yao wanayoishi.

Waziri huyo ameahidi kupunguza matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi, badala yake atazielekeza katika kujenga uchumi imara, huku wananchi wake wakipewa kipaumbele katika kumiliki fursa za kiuchumi.

Mbali na hilo amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na kutokubali kuvurugwa na baadhi ya watu, wanaotaka nafasi hiyo nyeti ambao wengine hawana sifa na uwezo wa kuwaongoza wananchi.

Kadhalika aliwataka pia kuacha kumshabikia mtu kwa misingi ya dini au ukabila badala yake watumie utashi wao, unaotokana na uadilifu na uwajibikaji wao walipokuwa serikalini wakiwahudumia wananchi.

“Nitakapoingia madarakani nitaanza kushughulikia mambo ya msingi nayo ni wakulima wa mazao ya chakula na biashara, natambua maisha yao yanategemea sana kilimo hivyo nitahakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje waweze kuuza mazao yao”, alisisitiza.

Alitaja pia kipaumbele kingine ni ujenzi wa viwanda huku akitolea mfano kilimo cha zao la korosho, suluhisho lake ni kuwajengea wakulima viwanda vya kubangulia zao hilo ili kuongeza ubora wa zao hilo na kuifanya jamii, iweze kupata ajira katika viwanda hivyo.

Vilevile alisema atatumia gesi iliyopatikana kwa wingi katika mkoa wa Mtwara na baadhi ya maeneo mengine ya nchi, kusukuma mbele uchumi wa nchi yote ya Tanzania bila kubagua na akaongeza kuwa suala hili linahitaji kiongozi aliyekuwa makini kutokana na kiasi kikubwa cha gesi tuliyonayo hapa nchini.


Pamoja na mambo mengine Waziri Membe amewaahidi wafanyabiashara kuwa atakapoingia Ikulu ataunda kamati ya wataalamu mbalimbali, kufuatilia mfumo wa mashine ya EFD’S kama zinamnufaisha mfanyabiashara hasa kwa wale wadogo wadogo ambao wengi wao licha ya kutumia mashine hizo, bado inaonekana ni tatizo kwao na kuendelea kuwafanya kuwa maskini.

No comments: