Friday, June 12, 2015

MAJERUHI ALIYEPATA AJALI KIGONSERA GARI KUTEKETEA KWA MOTO AFARIKI DUNIA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MWANAFUNZI wa shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) Regoberthy Mahay (16) ambaye ni mmoja kati ya majeruhi wanne waliolazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, baada ya kupata ajali na wanafunzi wenzake katika gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye korongo kisha kuteketea kwa moto, kitongoji cha Minazi kata ya Kigonsera wilayani humo, amefariki dunia.

Marehemu Regoberthy amefariki Juni 10 mwaka huu, majira ya saa 9 usiku baada ya kuzidiwa ghafla na kwamba mwili wake umesafirishwa kwenda kijiji cha Mpepo wilayani humo, kwa ajili ya mazishi.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Roberth Elisha alithibitisha kufariki kwa mtoto huyo na kueleza kuwa hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri, lakini kufikia majira hayo ya usiku alizidiwa ghafla kutokana na kushindwa kupumua ipasavyo.


“Ni kweli amefariki dunia, tatizo kubwa wakati analetwa hospitali kwa ajili ya matibabu alikuwa ameungua mwili mzima, madaktari tulifanya jitihada ya kuokoa maisha yake lakini kufikia siku hiyo alikata roho”, alisema Elisha.

Elisha alieleza kuwa majeruhi wenzake waliobakia hospitalini hapo, hali zao zinaendelea vizuri na kupatiwa huduma za matibabu.

Ajali ya kuteketea gari hilo ilitokea Juni 4 mwaka huu majira ya saa 11 jioni, wakati wanafunzi hao na Padri Hyasint Kawonga wa Parokia ya Kigonsera jimbo la Mbinga mkoani humo, walipokuwa wakitoka shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa ajili ya chakula cha watoto hao shuleni hapo.

Padri Kawonga ambaye ni Mkurugenzi wa shule hiyo, ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo ambalo lilipata ajali lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya Landrover One ten, baada kushindwa kupanda mlima ambapo lilirudi nyuma na kutumbukia kwenye korongo kisha kuwaka moto, huku ndani ya gari wakiwa wanafunzi na Padri huyo ambapo baadhi yao waliteketea kwa moto.


Tukio hilo lilisababisha kifo cha Padri Kawonga na wanafunzi saba, wakiwemo majeruhi 24 na kwamba kati ya majeruhi hao, 20 waliruhusiwa makwao na wanne walilazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga.

No comments: