Tuesday, June 23, 2015

NCHIMBI ATANGAZA RASMI KUTOGOMBEA JIMBO LA SONGEA MJINI

Dokta Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa CCM jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma.
Na Julius Konala,
Songea.

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Wananchi wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiangua kilio baada ya Mbunge wa jimbo hilo, Dokta Emmanuel Nchimbi kuwatamkia rasmi kuwa hatagombea tena nafasi ya kiti cha ubunge katika jimbo hilo. 

Tukio hilo lilitokea wakati Mbunge huyo, alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM kuanzia ngazi ya mashina hadi kata, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majimaji mjini hapa.

Dokta Nchimbi aliwaambia wanachama hao kuwa ameamua kuachia jimbo hilo, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka kumi jambo ambalo wanachama hao wa chama tawala, walilipokea kwa mshituko mkubwa.


Baada ya tamko hilo kutolewa na Mbunge huyo wa Songea mjini, simanzi na majonzi vilitawala katika eneo hilo la uwanja wa Majimaji, huku wengine wakibubujika machozi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutoamini na maamuzi hayo magumu, ambayo yaliyotolewa na Mbunge wao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanachama hao wa Chama Cha Mapinduzi walisema kuwa kuachia ngazi kwa Dokta Nchimbi, kutogombea kupitia jimbo hilo kunatoa fursa kubwa kwa vyama vya upinzani kuchukua jimbo hilo, jambo ambalo waliongeza kuwa hawatakubaliana nalo.

Wanachama hao wamemwomba Dokta Nchimbi kutengua msimamo wake, na kumtaka arejee tena kugombea kwenye jimbo la Songea mjini ambapo Mbunge huyo baada ya kupokea ombi hilo, aliwaeleza wanachama hao kuwa wamwachie nafasi ya kufikiri kwanza na ifikapo Juni 28 mwaka huu, atawapatia majibu.


Awali Dokta Nchimbi katika kulitumikia jimbo lake kwa kipindi cha miaka kumi, alielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho cha uongozi wake ni pamoja na ujenzi wa barabara, zahanati, miundombinu ya maji na shule za sekondari.

No comments: