Friday, June 12, 2015

MWANAFUNZI AGONGWA NA GARI AFARIKI DUNIA

Na Steven Augustino,
Songea.

MWANAFUNZI Vicent Baisi (13) anayesoma katika shule ya sekondari Ruhila, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari.

Gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili SM 8685 mali ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, mkoani humo ndilo lilimgonga mtoto huyo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, marehemu huyo aligongwa na gari hilo wakati alipokuwa akijaribu kuvuka barabara ambapo tukio hilo, lilitokea Juni 9 mwaka huu majira ya jioni.


Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alimweleza mwandishi wetu kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, aliokuwa akiendesha dereva wa gari hilo.

Baada ya tukio hilo dereva aliyefahamika kwa jina la Seleman Hamidu, alijisalimisha Polisi na hadi sasa anaendelea kushikiliwa huko, akisubiri sheria ifuate mkondo wake.

Msikhela alifafanua kuwa mwili wa marehemu huyo, umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya mkoa Songea, ukisubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.


Hata hivyo aliongeza kwa kuwataka madereva wanaoendesha magari, wanapokuwa barabarani wawe waangalifu na sio kuendesha kwa mwendo kasi kutokana na wakati mwingine hata walemavu, watoto na wazee wamekuwa wakitembea na kuvuka katika barabara hizo.

No comments: