Thursday, June 4, 2015

ASKARI JKT ATAFUTWA NA JESHI LA POLISI KWA UNYANYASAJI

Na Steven Augustino,
Songea.

ROBERT Mkika (26) ambaye ni askari wa kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale mkoani Ruvuma, anatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani humo ili aweze kujibu tuhuma ya kumtesa mtoto wa ndugu yake, ambaye alikuwa akiishi naye.

Mtoto huyo ambaye anafahamika kwa jina la Frank Kiria (9) anasoma darasa la tatu katika shule ya msingi mkombozi, Manispaa ya Songea mkoani hapa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kuwa katika kuhakikisha mtoto huyo anapata uangalizi salama hivi sasa wapo katika mchakato wa kufanya mawasiliano na vituo vya kulea watoto yatima, ili waweze kumkabidhi huko hadi taratibu za kumrejesha kwao Bukoba kwa wazazi wake zitakapokamilika.

Msikhela alifafanua kuwa Frank alikimbia nyumbani kwa askari huyo wa JKT Mei 27 mwaka huu, na kwenda kwa rafiki yake Jackson Malekela kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata.


Alisema rafiki yake huyo wote wanasoma darasa la tatu katika shule hiyo, na kwamba Mama mzazi wa Jackson, Bi Bupe Mlawa baada ya kumpikia chakula na kumaliza kula alipomtaka mtoto huyo arudi kwao, alikataa na kudai kuwa hatarajii kurudi tena kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata.

Mama huyo alipofanya mahojiano naye, Frank alisema kwamba amekuwa akinyanyaswa kwa kunyimwa chakula, mavazi na kulazwa chini mambo ambayo askari polisi baada ya kupewa taarifa na mama Mlawa walijionea kipindi walipokwenda kufanya uchunguzi, nyumbani alikokuwa akiishi mtoto huyo.


Taarifa za awali zinaonesha kuwa askari huyo wa Jeshi la kujenga taifa, alikwenda kumchukua mtoto huyo huko Bukoba mwaka 2014, kwa madai kuwa anakwenda kumlea.

No comments: