Sunday, June 14, 2015

FUNDIMBANGA TUNDURU WAIOMBA SERIKALI KUWAONGEZEA MRADI


Afisa mifugo wa kata ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Tatu Omary Tururu akisoma risala ya wanakikundi cha ufugaji ng'ombe wa maziwa katika hafla ya kuwapongeza wanakikundi hao kwa kufanya vizuri katika mradi wao, iliyofanyika kijiji cha Fundimbanga wilayani humo. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

KIKUNDI cha ufugaji ng’ombe wa maziwa kilichopo katika kijiji cha Fundimbanga Tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kujenga ubunifu juu ya taratibu za ufugaji huo, ambao umeweza kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na waweze kuondokana na umasikini.

Pamoja na pongezi hizo, wanachama wa kikundi hicho wameiomba pia serikali kuangalia uwezekano wa kuwapelekea miradi mingine kama vile ufugaji wa samaki na kuku, huku wakiitaka Halmashauri ya wilaya hiyo iwasaidie kuwajengea josho litakalosaidia kuogeshea mifugo yao.

Hayo yalisemwa kupitia risala yao ambayo ilisomwa na afisa mifugo wa kata ya Matemanga, Tatu Tururu na kuongeza kuwa kijiji cha Fundimbanga kilipokea mradi wa ng’ombe wa maziwa 20 wenye thamani ya shilingi milioni 16 uliotolewa kwa ufadhili wa mpango wa DADPs, kupitia Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mwaka 2012.


Afisa mifugo huyo alisema kuwa mradi huo, ulipokelewa na wanachama wa kikundi hicho cha ufugaji ng’ombe wa maziwa kupitia kauli mbiu ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe, ambapo kati ya ng’ombe hao kulikuwa na majike 19 na dume mmoja.

Wanachama wa kikundi hicho, hivi sasa wameongezeka na kufikia wanachama 42 ambapo kila mmoja wao, sasa anamiliki ng’ombe mmoja bora wa maziwa.

Akizungumzia juu ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo wafugaji hao, Tururu alisema kutokana na kukosekana kwa huduma za uhakika ikiwemo suala la kuwatibu ng’ombe wao, tatizo hilo linasababisha baadhi ya ng’ombe kupoteza maisha na kuwafanya warudi nyuma kimaendeleo.

Pamoja na mambo mengine akimwakilisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Kaimu afisa tawala wa wilaya hiyo, Manfredy Hyera aliwapongeza wanakikundi hao kwa kujali na kutunza mradi wao, ili uweze kuwa endelevu katika kuwaboreshea maisha yao.

Hyera alitumia nafasi hiyo, kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo kuangalia uwezekano wa kupanga bajeti kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani, ili fedha zitakazopatikana zisaidie ujenzi wa josho hilo na kupeleka mtaalamu atakayeweza kusimamia mifugo hiyo kwa karibu ili isishambuliwe na magonjwa mbalimbali.

No comments: