Saturday, June 27, 2015

ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMBAKA MLEMAVU

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Na Sreven Augustino,
Songea.

NIRU Nyimbi (42) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mwombezi kilichopo kijiji cha Chandarua mkoani Ruvuma, anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mlemavu mwenye mtindio wa ubongo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, mtuhumiwa alinaswa akiwa anafanya unyama huo kijijini humo ambako imeelezwa kwamba, alikwenda kufanya kazi ya kibarua cha kufyatua tofari.

Mihayo Msikhela, Kamanda wa polisi wa mkoa huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo alifumaniwa na mama mzazi wa binti huyo aliyemtaja kwa jina la, Oresta Ndonde.

Mama huyo alifanikiwa kumkamata mtuhumiwa, baada ya kusikia sauti ya binti yake akiwa analia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata wakati anafanyiwa unyama huo.


Baada ya mama huyo kusikia sauti hiyo, ambayo ilikuwa ikitokea choo cha nyumba ya jirani yake, alikwenda haraka na kumkuta mtoto wake akiwa amevuliwa nguo huku akiwa amelaliwa kifuani na mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa baada ya kushuhudia tukio hilo, mama huyo alipiga kelele akiomba msaada ambapo majirani walijitokeza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Nyimbi, kisha walimpeleka kituo cha polisi.

Kamanda Msikhela aliendelea kufafanua kuwa walipofika kituoni hapo, Polisi walimpatia hati namba tatu (PF 3) kwa ajili ya kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake hospitali, ili kuweza kubaini kama amepewa maambukizi ya homa mbalimbali ikiwemo UKIMWI.

Hata hivyo alisema mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani, baada ya kukamilika taratibu husika ili kupisha sheria iweze kuchukua mkondo wake na iwe fundisho kwa wengine, wenye tabia kama hiyo.


No comments: