Monday, June 1, 2015

MWENYEKITI UWT AWATAKA WAANDISHI KUZINGATIA MAADILI YA KAZI ZAO

Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

WANAHABARI mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya taaluma yao, kwa kujenga ukweli katika kazi zao za kila siku ambazo huripoti katika vyombo vya habari, ikiwemo kufichua watu wanaojihusisha na vitendo vya kuomba, kupokea na kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka huu.

Licha ya kufanya hivyo, wamehimizwa kujiendeleza kielimu jambo ambalo litawafanya waweze kuwa na uwezo mkubwa wa kuandika habari hasa zile za uchunguzi, ambazo husaidia jamii kuleta chachu ya kimaendeleo.

Pendo Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wilayani Mbinga, alisema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku mbili kwa akina mama wa umoja huo waliotoka katika kata zote za wilaya hiyo, yenye kulenga kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wanawake hao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.


Ndumbaro alisema ni jambo la kushangaza kumuona mwandishi wa habari, anaacha majukumu yake ya kazi na kugeuka kuwa mpiga debe wa mgombea fulani, huku akitambua fika kufanya hivyo ni kuvunja maadili ya kazi.

Aidha Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo, kuwakumbusha waandishi wa habari kutangaza fursa zilizopo ndani ya mkoa wa Ruvuma, ambazo kwa kiasi kikubwa zitasaidia kuvutia watalii wa ndani na nje.


“Mbali na hili vita dhidi ya vitendo vya rushwa ni lazima muelimisha jamii kila kukicha katika vyombo vyenu vya habari, kwani kalamu zenu zina nguvu kubwa kuliko upanga na huwafikia idadi kubwa ya watu kwa haraka zaidi”, alisema.

No comments: