Wednesday, June 10, 2015

MWENYEKITI CCM MKOA WA RUVUMA AVAMIWA NA CHADEMA KATIKA KATA YAKE

Mathayo Kaimaima.
Na Stephano Mango,
Nyasa.

KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Mathayo Kaimaima ametangaza nia yake ya kuchukua fomu ya kugombea udiwani katika kata ya Chiwanda wilayani humo, ambayo kata hiyo kwa sasa inaongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Oddo Mwisho.

Mwisho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, ameeleza kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka kufanya mabadiliko ya kweli kwa kumpata kiongozi mwingine wa kutoka chama cha upinzani, ambaye ataweza kuleta ushirikiano wa karibu katika kusukuma mbele maendeleo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimaima alisema kuwa amechukua maamuzi hayo baada ya kuona kwamba wananchi wake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo diwani aliyekuwa madarakani na ambaye anaelekea kumaliza muda wake, ameshindwa kutatua kero husika na kuwafanya wananchi waendelee kuwa maskini.


Kaimaima alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kumuona Mwisho ambaye amebeba vyeo vingi akiwa pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, ameshindwa kutetea ujenzi wa barabara ya kutoka Mbamba bay kwenda mpakani mwa nchi jirani ya Msumbiji ambako ndipo kata hiyo ipo mpakani humo, na haipitiki na kuwafanya wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla kushindwa kufanya shughuli zao ipasavyo.

“Barabara hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa kata ya Chiwanda kutokana na kuwa mpakani, akina mama wajawazito wamekuwa wakijifungulia njiani kutokana na vyombo vya usafiri kama vile magari hasa nyakati za masika kukwama wakati mgonjwa anapopelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu”, alisema Kaimaima.

Kada huyo wa CHADEMA ameendelea kumrushia kombora Oddo Mwisho akisema kuwa, ameshindwa hata kuwaunganisha wananchi ambapo muda mwingi amekuwa akiwagawa na kujenga makundi, ambayo hayana tija katika jamii kwa manufaa yake binafsi.

Alisema umefika wakati sasa, viongozi wa CCM kuwapumzisha na kukipatia nafasi CHADEMA kiweze kuwaongoza wananchi wake kikamilifu, ili waweze kunufaika na rasilimali zao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA wilaya ya Nyasa, Jacob Beniwes alisema chama hicho kimejipanga kuwasimamisha wagombea wa udiwani katika kata zote 21 zilizopo wilayani Nyasa, ikiwemo hata kumsimamisha mgombea wa ubunge ndani ya wilaya hiyo ambayo ina jimbo moja la uchaguzi.


Katibu huyo alisisitiza kuwa chama kitahakikisha kwamba kinafanya kampeni zake kwa ustaarabu, usiku na mchana ili kuweza kupata ushindi mnono ambao utakiwezesha kuongoza wananchi wake wilayani humo na kuwaletea maendeleo.

No comments: