Friday, June 12, 2015

JANUARY MAKAMBA: KUPAKANA MATOPE TUNAJIWEKA KATIKA WAKATI MGUMU


January Makamba akiwa katika taswira tofauti za mapokezi na mkewe Ramona Makamba, leo mjini Songea mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JANUARY Makamba, ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli amewataka makada wote wlioomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais hapa nchini, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) endapo kama hawana dhamira ya dhati waache kugombea nafasi hiyo, badala yake wakiache chama kikiwa salama baada ya kukamilika kwa mchakato huo.

Makamba alisema hayo leo mjini Songea mkoani Ruvuma, mara baada ya kupokea orodha ya wanachama wa chama hicho ambao walijitokeza kumdhamini ambapo jumla ya wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini, katika nafasi hiyo.

Alieleza kuwa kuna watu wameomba kugombea nafasi hiyo nyeti, huku akidai kuwa baadhi yao hawana sifa na endapo hawatateuliwa, kuna hatari ya kukisambaratisha chama hicho.

Mbunge huyo alifafanua kuwa CCM kinahitaji kupata mgombea ambaye atahakikisha chama hicho kinabaki salama na kuwaongoza Watanzania, bila kujali itikadi ya dini, rangi au kabila huku akijisifia kuwa yeye ndiye mwenye uwezo wa kushika nafasi hiyo.


“Mimi siamini kwamba siasa za kupakana matope ndio zinaweza kutujenga, sisi sote ni wanachama wa chama kimoja mwisho wa siku, tutapata mgombea mmoja na tutahitajika kumpigia kura”, alisema Makamba.

Alisema kuwa endapo wagombea wataendelea kupakana matope katika mchakato huu wa kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo ya urais, anaamini wakati ukifika kumpata mteule kutakuwa na wakati mgumu kwa kile alichodai kuwa itakuwa sio rahisi kumfanyia kampeni, mtu ambaye tayari amepakwa matope kwa wananchi.

Kadhalika alieleza kuwa kuna kila sababu wananchi, kuwapima wagombea ambao wanaonekana wakiomba nafasi hiyo kwa mbwembwe, kwani hata wakiipata itakuwa ni tatizo katika kuliongoza taifa hili.

Makamba alisema kuwa CCM ni chama makini na kamwe hakitaweza kumteua mgombea kwa uwoga, kama inavyodaiwa na baadhi ya wagombea wengine kwamba wasipochaguliwa chama kitaingia katika hali ambaya, jambo ambalo sio sahihi.

“Nina imani kubwa kwamba chama changu kitamteua mgombea ambaye ni mwadilifu, na ni rahisi kumnadi wakati kampeni zitakapoanza”, alisema.

Akizungumzia juu ya mkoa wa Ruvuma, alisema mkoa huo hivi sasa unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la upatikanaji umeme wa uhakika na upande wa huduma za matibabu katika Hospitali ya mkoa, Songea.

Alibainisha kuwa kutokana na matatizo hayo yeye binafsi anayatambua, endapo wananchi na chama kwa ujumla kitampatia ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais atahakikisha mkoa, unaingizwa kwenye gridi ya taifa kama ilivyo kwa mikoa mingine.


Hata aliongeza kuwa atakapoingia Ikulu, atakuwa na uwezo wa kuamua mambo makubwa yanayolihusu taifa hili tofauti na nafasi aliyonayo sasa ya ubunge, ambayo inampaka wake katika kushughulikia matatizo ya wananchi.

No comments: