Saturday, June 27, 2015

NYALANDU: VIONGOZI WASIOKUWA NA SIFA NI MIZIGO KWA CHAMA

Na Muhidin Amri,
Songea.

WAZIRI wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini ambao wanawania kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya urais, amewatahadharisha viongozi na wanachama wa CCM kuwa makini katika uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, ili kuepuka kuteua watu wasiokuwa na sifa ambao watakuwa mzigo kwa chama wakati utakapofika wa kuwanadi kwa wananchi.

Nyalandu alisema kuwa CCM imara itajengwa na viongozi imara waliopo madarakani, kwa kuzingatia hekima na kusimamia vizuri misingi ya haki na ukweli na kwamba pasipo kufanya hivyo wanaweza kukipeleka chama kubaya na kusababisha baadhi ya wanachama, kushindwa kukiamini tena.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, mara baada ya kukamilisha zoezi la kuwapata wadhamini kwa nafasi hiyo anayogombea.


“Ninawatahadharisha wanaccm wenzangu, muda utakapofika msifanye mchezo kwa kumchagua mtu ambaye atakuwa mzigo kwenu chagueni mtu ambaye licha ya kuwa na uwezo wake wa kiutendaji ndani na nje ya chama, lakini awe muadilifu na anayefahamu vizuri misingi na taratibu za nchi yetu”, alisema.

Alisema kwamba wakati wa kupokezana kijiti cha uongozi katika nchi hii umefika, hivyo ni zamu ya watu wengine kuingia Ikulu kuendeleza yale yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, ambapo katika muda wa utawala wake kipindi cha miaka kumi Rais huyo amefanya mambo mazuri ambayo leo hii Watanzania wanajivunia.

Alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuna baadhi ya Watanzania ambao hawana shukrani, wamekuwa wakibeza mafanikio yalipatikana katika uongozi huu wa awamu ya nne badala yake aliwataka waache kufanya hivyo, kwani hukatisha tamaa.

Endapo atapata nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya urais katika nchi alisema, mambo ya msingi atakayoyaendeleza ni umoja, amani na mshikamano kwa watu wote.


Kwa mujibu wa Nyalandu aliongeza kuwa yeye amekuwa ndani ya CCM tangu akiwa na umri mdogo, ambapo hivi sasa licha ya kuwa waziri lakini ni kati ya wagombea wachache waliozaliwa, kukua ndani ya chama na sio kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine ambao wamekikuta chama njiani.

No comments: