Thursday, June 18, 2015

FUNDI MITAMBO YA KAHAWA KUGOMBEA UDIWANI KATA YA MBAMBI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MICHAEL Ndomba ambaye amebobea katika ufundi wa mitambo ya kukoboa kahawa mbichi na kavu, ametangaza nia ya kugombea udiwani wa kata ya Mbambi iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akiahidi kuwaletea neema wananchi wa kata hiyo.

Ndomba ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa kiwanda cha serikali cha kukoboa kahawa wilayani Mbinga (MCCCO) tokea mwaka 1988 na baadaye amestaafu mwaka huu, hivi sasa anafanya kazi ya mizani na ufundi wa kuunda mitambo ya kati ya kukoboa kahawa mbichi.

“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kujipatia maendeleo hasa katika viwanda, kilimo na ufugaji wananchi wakizalisha kwa wingi katika eneo hili wataweza kuondokana na umasikini”, alisema Ndomba.


Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ambapo alieleza kuwa kata ya Mbambi inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maji na barabara za uhakika hivyo endapo wananchi watampatia ridhaa ya kuwaongoza, atahitaji ushirikiano wa kutosha na usimamizi mzuri wa pamoja katika kusimamia maendeleo ya wananchi ili kuleta ufanisi wenye tija katika jamii.

Vilevile alifafanua kuwa kuhusiana na tatizo la maji na barabara, atashirikiana na serikali kuhakikisha kwamba visima vya maji vinachimbwa katika kata hiyo ili akina mama, waweze kuondokana na adha ya kutafuta maji umbali mrefu na kwa upande wa barabara atahakikisha zinajengwa kwa viwango vinavyokubalika ili ziweze kupitika wakati wote masika na kiangazi.

Kadhalika alibainisha kuwa kutokana na taaluma yake ya ufundi aliyonayo atawaunganisha pia vijana na akina mama kwa kuwapa mbinu za kuunda vikundi vya ujasiriamali, baadaye waweze kukopesheka na taasisi za kifedha hatimaye waweze kusonga mbele na kuepukana na tabia ya kuwa tegemezi.

Alisisitiza kusimamia na kuboresha sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari, kwa kuwataka wazazi kupeleka watoto wao shule na kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma vizuri.


Hata hivyo alisema katika safari hiyo anaimani peke yake hawezi kufika, lakini wana CCM wanachotakiwa wamuunge mkono ili aweze kuingia madarakani na kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo, katika kata ya Mbambi.

No comments: