Tuesday, June 23, 2015

HOSPITALI LITEMBO YAZINDUA SACCOS YAKE WANACHAMA WATAKIWA KUWEKA AKIBA

Katikati ni Meneja mkuu wa benki ya CRDB tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, Efrosina Mwanja akimpongeza kwa kupeana mkono na Mwenyekiti wa Chama cha ushirika Litembo SACCOS, Joseph Komba katika sherehe ya uzinduzi wa chama hicho iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Litembo iliyopo wilayani humo.


Vikundi mbalimbali vya ngoma za asili (kioda na mganda) navyo havikuwa mbali siku hiyo ya uzinduzi rasmi wa SACCOS hiyo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo, Litembo SACCOS wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuweka akiba kwa wingi jambo ambalo litawafanya waweze kukidhi mahitaji husika ndani ya chama hicho na kuepukana na tabia ya kuingia mikataba ya mikopo na taasisi za kifedha, ambazo hazijapewa dhamana ya kutoa mikopo.

Aidha wameshauriwa kwamba, endapo watahitaji kupewa mikopo hiyo ni vyema wakaingia mkataba na benki ili waweze kupewa fedha ambazo hatimaye wataweza kutoa mikopo kwa wanachama wake, na kuwafanya kusonga mbele kimaendeleo.

Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa benki ya CRDB tawi la Mbinga, Efrosina Mwanja alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya uzinduzi wa SACCOS hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Litembo, katika kata ya Litembo wilayani humo.


“Ndugu zangu haki ya chombo hiki ni kuingia mikataba katika mabenki na kuweza kupata huduma za kifedha ambazo mtakopeshana, lakini natoa rai kwenu viongozi kuweni waaminifu ndani ya chama baadaye chama kiweze kusonga mbele”, alisisitiza Mwanja.

Meneja huyo aliutaka uongozi wa bodi ya Litembo SACCOS kuacha tabia ya kujilimbikizia mali kwa kujikopesha fedha wenyewe, badala yake wawe makini na wasimame imara ili chombo hicho kiweze kuleta manufaa kwa wanachama wote na jamii kwa ujumla.

Naye Meneja biashara wa CRDB wilayani hapa, Hando Matley alifafanua kuwa benki hiyo ipo tayari kutoa elimu ya ujasiriamali na mikopo kwa wanachama wa ushirika huo kwa masharti nafuu, huku akiwasisitiza kuongeza juhudi katika kuweka akiba.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ushirika huo Makamu Mwenyekiti, Stella Ndomba alisema kuwa wanachama wa SACCOS hiyo ni watumishi wa Hospitali ya Litembo, ambapo mpaka sasa ina jumla ya wanachama 145 na wengine wanaendelea kujitokeza ili waweze kujiunga ndani ya chama hicho.

Ndomba alieleza kuwa mnamo Oktoba 7 mwaka 2014 mchakato wa kuunda chama ulianza, ikiwa ni lengo la watumishi wa Hospitali hiyo waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Hata hivyo alibainisha kuwa chama hicho, kimefungua akaunti yake katika benki ya CRDB tawi la Mbinga na kukusanya fedha kutoka kwa wanachama kwa kiingilio, hisa na amana na kufanya chama mpaka sasa kuwa na akiba ya shilingi milioni 19,650,000.

No comments: