Monday, June 15, 2015

UWT YAWATAKA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Manduzi Tanzania (UWT) mkoa  wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama akizungumza na wananchi wilayani Tunduru mkoani humo, (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya baraza la Idd wilayani humo.
Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANAWAKE mkoani Ruvuma, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi mkoani humo ili kuweza kufikia malengo ya hamsini kwa hamsini, katika kuongoza jamii.

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) mkoani humo imewataka wanawake kufanya hivyo, kwa kuunganisha nguvu pamoja na kuacha tabia ya kubezana au kupakana matope kwamba mtu fulani hatoshi.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Ruvuma, Kuruthum Mhagama katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya baraza la Idd wilayani Tunduru.

Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, kitaibuka na ushindi wa kishindo hivyo wanachama wa UWT wametakiwa kuendelea kukisemea vizuri chama hicho, hasa kwa yale yaliyotekelezwa kupitia ilani yake.


Kadhalika Waasisi wa CCM wilayani humo, Husna Makanjila na Futuma Kalongo walitahadharisha kuwa wajumbe hao wanatakiwa kufanya kazi zao, kwa kuzingatia weledi na kuacha kukigawa chama.

Walisema hivi sasa kumekuwa na utitiri wa vyama vya siasa hapa nchini, ambapo muda mwingi vimekuwa vikikiandama chama tawala kwa kutoa kauli mbaya na matusi, kwamba chama hicho ambacho kimetawala watanzania miaka 50 hakijafanya chochote, jambo ambalo sio kweli.

Waasisi hao walieleza kuwa wanawake ambayo ndiyo nguzo kuu ya familia katika taifa hili, endapo wataunganisha nguvu zao katika ushawishi kwa chama cha mapinduzi kutakuwa na uhakika kuwa chama hicho kitaibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Awali akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Tunduru, Mariam Mchongea aliwaeleza wapenzi na wakereketwa wa CCM kuwa wanawake kupitia Jumuiya hiyo wamejipanga na kuhakikisha kwamba, hapatakuwa na mpasuko wa aina yoyote ile ambao utasababisha chama tawala kumeguka katika makundi mbalimbali.

No comments: