Wednesday, June 10, 2015

MGOGORO WA WAFUGAJI WANUKIA TUNDURU


Baadhi ya wafugaji wakiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, walikwenda huko kwa lengo la kupinga tukio la kufukuzwa na kuhamishwa katika maeneo wanayofugia. 


Mfugaji wa jamii ya kisukuma ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake, akiwa na mifugo yake katika kijiji cha Masonya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. (Picha zote na Steven Augustino)
Na Mwandishi wetu,

Tunduru.

SERIKALI imeombwa kutengeneza utaratibu wa kudumu, wa kuijengea sekta ya ufugaji miundombinu ya uhakika jambo ambalo litaifanya iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa, tofauti na ilivyo sasa sekta hiyo imekuwa ikichangia wastani wa asilimia 6 tu, kiasi ambacho  imeelezwa kuwa  ni kidogo.

Hayo yalibainishwa na wafugaji waliopo katika maeneo mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakati walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho pamoja na Mkurugenzi mtendaji, Tina Sekambo wakati wakipinga amri ya kuondolewa katika maeneo ya vijiji wanavyoishi na kufanyia shughuli za ufugaji.

Wafugaji hao walisema, ni jambo la muhimu kwa serikali kutilia mkazo juu ya maoni yao, ikiwemo kuacha tabia ya kunyanyasa wafugaji ili kuweza kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.
                    
Rugwashi Mtegwambuli na Leleshi Latu ni miongoni mwa wazee wafugaji, ambao walivunja ukimya na kuilalamikia serikali kuwa hali hiyo inatokana na kutotekeleza makubaliano husika, huku akisema kuwa serikali imewasahau wafugaji na kuwafanya kama sio watanzania ambao wanapaswa kuishi na kupewa haki zao za msingi, kama ilivyo kwa watu wengine.


Walisema wao ni watanzania ambao ni miongoni mwa wafugaji walioondolewa katika bonde la Ihefu kutokana na kuwa na makundi makubwa ya ng’ombe, lakini walipofika maeneo ya Tunduru lilitolewa tamko kwamba waweke makazi yao huko, hali ambayo iliwafanya wajisajili katika vijiji vya wilaya hiyo na kusomesha watoto wao hivyo sasa wanashangaa pale wanapoambiwa tena kwamba wahame bila kupewa maelekezo wanakwenda kuishi wapi na watoto hao watasoma wapi.

“Sisi ni watanzania na kazi ya ufugaji tunayofanya ni halali kama zilivyo kazi zingine, hatukatai kuondoka kwenye maeneo haya lakini tunaiomba serikali inapotoa amri ya kututaka tuondoke, itoe maelekeo wapi tunakwenda”, alisisitiza mzee Leleshi.

Mzee huyo aliendelea kufafanua kuwa, msimamo wao umetokana na kuchoshwa na utaratibu mbovu wa serikali kuwaonea mara kwa mara wafugaji na kuonekana ni watu wa kuhama hama.

Wafugaji wengine ambao nao walizungumzia juu ya hali hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji (CCW) wilayani Tunduru, Othuman Marhaja kutokana na wao kutii mamlaka husika walikubali kuondoka kwenye bonde la Ihefu mkoani Mbeya, kupitia tamko lililotolewa na serikali mwaka 2006/2007 na kutakiwa kwenda katika mikoa ya Lindi na Mtwara lakini wakiwa njiani mifugo yao ilianza kufa kutokana na homa ya bonde la ufa, hali ambayo serikali ilitoa tena tamko jipya la kusitisha zoezi hilo la kusafirisha mifugo ili ugonjwa huo usiweze kusambaa.

Naye Nandala Samwel alieleza kuwa kinachowashangaza ni utaratibu wa serikali, kuendelea kuwanyanyasa na kuwafukuza kwenye maeneo ambayo tayari walikwisha jisajili katika vijiji, huku wakiwachangisha michango na kuwatoza ushuru wa aina mbalimbali ambao sasa imekuwa ni kero kwao.

Akizungumzia juu ya tamko hilo la kuwaondoa wafugaji hao, Mwenyekiti wa Halmashauri wilaya ya Tunduru, Faridu Khamis alisema maamuzi hayo yametokana na uwepo wa uvamizi mkubwa unaofanywa na wafugaji hao ikiwa ni tofauti na maelekezo yaliyotolewa katika vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Khamis alisema wakati wafugaji hao wanaingia wilayani humo, hawakuzidi 10 lakini tawimu alizonazo sasa zinaonesha makundi ya wafugaji ni zaidi ya 52 yameonekana yakifanya shughuli za ufugaji ndani ya wilaya.

Mwenyekiuti huyo alivitaja vijiji ambavyo vimevamiwa na makundi hayo kuwa ni Misechela, Sauti moja, Mkowela, Tulieni, Nakapanya, Songambele, Mchangani, Machemba, Liwangula, Mbuyuni, Twendembele, Kindamba na Jakika kwa kile alichodai kuwa maeneo hayo ni maalumu kwa ajili ya hifadhi ya misitu.

Alisema kumbukumbu zilizopo katika ofisi yake zinafafanua kuwa wafugaji hao waliruhusiwa kukaa katika vijiji vya Musonya, Muhuwesi na Ngapa lakini kutokana na wafugaji kuwa na tabia ya kuwaita wenzao kutoka maeneo mengine nje ya wilaya, wameendelea kuongezeka hali ambayo sasa inahatarisha usalama na amani ndani ya wilaya ya Tunduru.

1 comment:

Anonymous said...

Kuna kila sababu kwa serikali kumaliza mgogoro huu, kabla haujafikia mahali pabaya.