Wednesday, June 17, 2015

UWT TUNDURU YAVUNA WANACHAMA WAPYA

Mmoja kati ya wanachama wapya wa UWT wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Winfrida Chibwana akipokea kadi ya kujiunga na Jumuiya hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wake wa mkoa wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama. (Picha Steven Augustino)
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANACHAMA wapya 200 wamejitokeza wilayani Tunduru, mkoa wa Ruvuma na kujiunga na Jumuiya ya Umoja Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wilayani humo.

Fatuma Mandingo ambaye ni Katibu wa Jumuiya hiyo wilayani humo, alisema huo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha umoja wao hasa katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mandingo alisema kuwa UWT itagawa kadi kwa wanachama wapya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru, ili kuendelea kuimarisha na kujihakikishia ushindi katika uchaguzi huo ujao ambao wanachama wa CCM watamchagua Rais, Mbunge na Diwani.


Katibu huyo alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa, kwenye viwanja vya baraza la Idd ambao ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama ambaye ndiye alihusika katika kugawa kadi hizo kwa wanachama wake.

Alisema kuwa wanachama hao wamepatikana kupitia hamasa iliyofanywa kupitia vikao vyao mbalimbali, na kwamba zoezi hilo ni endelevu.

“Tatizo kubwa tunalokabiliana nalo hapa ni upungufu wa kadi, hivyo tunawaomba viongozi wetu wa UWT mkoa wafanye utaratibu wa kutuletea kadi ili wanachama wengi waliopo ndani ya wilaya hii, waweze kuwa na kadi”, alisema Mandingo.


No comments: