Saturday, November 29, 2014

WANACCM RUVUMA WATAKIWA KUACHA MAJUNGU NA FITINA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, aliyevaa skafu shingoni akiangalia mganda ngoma ya asili, wakati alipowasili juzi katika ofisi kuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Songea mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano na kuacha vitendo vya majungu na fitina ndani ya chama, huku ikielezwa kuwa endapo kama wataendeleza mambo hayo yatawafanya wagawanyike katika makundi na kusababisha hata wanachama wa chama hicho wakose imani nao.

Aidha walielezwa kuwa CCM ni chama ambacho kipo madarakani kwa miaka mingi tokea nchi hii ipate uhuru, mikononi mwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, hivyo wanapaswa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa katiba husika ili wananchi wasiweze kujengeka na dhana potofu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM, kwenye ukumbi wa Songea Club uliopo mjini hapa.

Sunday, November 23, 2014

AFISA USALAMA WA TAIFA WILAYA YA MBINGA AMTISHIA MWANDISHI WA HABARI KWA BASTOLA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Na Gideon Mwakanosya,


Mbinga.

MWANDISHI wa habari Kampuni ya Businesstimes Limited, Kassian Nyandindi anayeandikia gazeti la Majira wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ameshushiwa kipigo na kutishiwa kuuawa kwa silaha na Afisa usalama wa taifa (DSO) wa wilaya hiyo (Jina tunalo) katika hoteli ya Gold Farm ya Mbinga mjini.

Habari zilizopatikana mjini hapa, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 22 mwaka huu, majira ya saa 5 usiku kwenye hoteli hiyo wakati mwandishi huyo alipokuwa anaaga kurudi nyumbani kwake.

Taarifa zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa, Nyandindi ambaye alikuwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, alishushiwa kipigo na kigogo huyo wa usalama wa taifa ambapo baadhi ya wajumbe wa UVCCM wakiwemo maafisa wa umoja huo toka makao makuu ya chama hicho, walishuhudia tukio hilo.

Aidha wajumbe hao walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walishitushwa na kufikia hatua ya kwenda karibu na tukio hilo na kuingilia kati ili kuweza kumnusuru mwandishi huyo asiweze kudhurika, licha ya kuwa wakati huo tayari alikuwa anapigwa mateke na ngumi huku kigogo huyo akiporomosha lugha chafu akimtukana mwandishi huyo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida inadaiwa kwamba afisa usalama huyo wa taifa, baada ya kuona mwandishi Nyandindi amebebwa na kuingizwa kwenye gari ili apelekwe nyumbani kwake, ghafla alitoka kwenye eneo la tukio na kwenda kuchukua silaha aina ya bastola, aliyokuwa ameihifadhi kwenye gari lake ambalo alikuwa ameliegesha  nje ya hoteli hiyo.

Habari zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa wakati silaha hiyo akiwa ameishika mkononi tayari kwa kutaka kumfyatulia risasi mwandishi wa habari, baadhi ya wajumbe wa UVCCM waliokuwepo kwenye eneo hilo la tukio walimdhibiti afisa usalama huyo na kufanikiwa kumnyang’anya silaha hiyo, ambayo baadae ilidondoka chini na kuokotwa na mmoja wa viongozi hao wa chama huku wakimuuliza kwa nini unataka kufanya mauaji kwa mwandishi wa habari huyu, ambapo alishindwa kuwa na majibu zaidi aliendelea kufoka kwa hasira huku akiporomosha matusi.

Saturday, November 22, 2014

KATIBU MKUU UVCCM TAIFA AENDELEA NA ZIARA YAKE WILAYANI MBINGA, SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA VIONGOZI WENYE MATENDO YA HOVYO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, akipokelewa na Vijana wakiwemo pia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi leo asubuhi, katika eneo la Tanki la maji mjini hapa wakati anawasili wilayani Mbinga akitokea wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda akiwasili katika ofisi kuu ya CCM wilayani Mbinga.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda akizungumza na wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIBU wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda amesema, serikali nchini ipo tayari kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi yeyote aliyekuwa madarakani, ambaye anaonesha kuwa na matendo ya hovyo kwa wananchi wake na yenye  kurudisha nyuma maendeleo husika.

“Ndugu zangu wananchi hatupo tayari mahali popote pale, kumvumilia Mkuu wa wilaya au Mkurugenzi mtendaji mwenye matendo ya hovyo na yenye kukatisha tama wananchi, tukisikia tunamwondoa haraka tunahitaji kiongozi mwenye kujali maisha na maendeleo ya watu wake”, alisema.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu huyo leo, alipokuwa akihutubia wananchi wa kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mpepai wilayani humo.   

Mapunda alisema kuwa itakuwa ni ajabu kwa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumkalia kimya bila kumwajibisha kiongozi ambaye hana nia njema na taifa hili, huku akiwaacha wananchi wakiteseka kutokana na mambo yake binafsi ambayo hayana tija katika jamii.

Friday, November 21, 2014

KATIBU MKUU UVCCM TAIFA KUFANYA ZIARA MBINGA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini kinaendelea kuwa imara na kuwajali wananchi wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa chama hicho, Sixtus Mapunda atafanya ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo pia na taratibu za kuimarisha chama na umoja huo kwa ujumla.

Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa Katibu huyo atapokelewa mjini hapa kesho, Novemba 22 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwasili kwenye viwanja vya ofisi kuu ya CCM wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akitokea wilaya ya Nyasa mkoani humo.

Wananchi wa wilaya hiyo wameombwa kujitokeza kwa wingi, katika kushiriki zoezi hilo muhimu  la mapokezi.

Aidha Mapunda katika ziara yake baada ya kuwasili kwenye ofisi za chama hicho, atafanya ziara fupi akielekea kata ya mpepai kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata hiyo.

Baadaye atarudi Mbinga mjini kwa lengo pia la kuzungumza na wananchi mnamo majira ya mchana, hivyo wadau wanaombwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara ambao atahutubia kwenye viwanja vya soko kuu vilivyopo mjini hapa.

Kwa ujumla Mapunda sio mtu mgeni kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga, wengi wao wamekuwa wakimfahamu akiwa mzaliwa wa wilaya hii, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kumsikiliza.

Pamoja na mambo mengine, Katibu huyo wa vijana mnamo Novema 23 mwaka huu wakati anamaliza ziara yake ya kikazi wilayani humo, atazungumza na wakazi wa kijiji cha Kigonsera hatimaye kuelekea Songea mjini.


Monday, November 17, 2014

KWA MAMBO HAYA YANAYOFANYWA NA MKURUGENZI HUYU WA MBINGA, HAKIKA SEKTA YA ELIMU HUENDA IKADOROLA WILAYANI HUMO


Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akisisitiza jambo wakati akiwa katika vikao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JINAMIZI linalodaiwa kutengenezwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga katika kuhakikisha linaendelea kumsakama Afisa elimu msingi Mathias Mkali na walimu wake, imeelezwa kuwa ni dalili tosha zinazoashiria kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu msingi wilayani humo, ambapo hivi sasa limeingia katika sura mpya kwa walimu wakuu wa shule hizo likitaka taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za TSM. 9 na Capitation zinazopelekwa mashuleni.

Mkurugenzi huyo amewaandikia barua walimu hao ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba MDCC/F. 10/20/43 ya Novemba 10 mwaka huu, ikiwataka waandae taarifa hiyo ya kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi sasa 2014/2015.

Baadhi ya walimu waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo kuwaandikia barua hiyo ambayo ameichelewesha kuwafikia walimu hao, ikiwataka kufanya kazi hiyo   jambo ambalo ni vigumu huku wengine wakibeza na kusema huenda anatafuta sababu kwa mwalimu atakayekosea na kushindwa kukamilisha kwa wakati apate cha kusemea.

Walisema wamechoshwa na mambo yake tokea aingie katika wilaya ya Mbinga, amekuwa ni mtu wa kuongoza wenzake kwa njia ya migogoro na kuwatafutia sababu zisizo na msingi badala ya kukaa na kubuni mipango ya kimaendeleo, huku wakiongeza kuwa kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi wake wa ndani, Laston Kilembe alipokuwa akipita hivi karibuni kuhoji mashuleni kwa walimu wakati anafanya ukaguzi wake juu ya fedha hizo, lakini mkaguzi huyo hakufanya hivyo ndio maana hivi sasa walimu hao wanasumbuliwa akiwataka watekeleze hilo.

Sunday, November 16, 2014

CHEMBA YA WAFANYABIASHARA MBINGA YAITAKA SERIKALI ULIPAJI KODI UFANYIKE MAHALI BIDHAA INAPOZALISHWA, GAUDENCE KAYOMBO LAWAMANI


Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

UMOJA wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, umepanga mikakati na kuitaka serikali iweke taratibu zake ambazo zitahakikisha kwamba, kila jambo la ulipaji wa kodi lifanyike pale mahali ambapo bidhaa inazalishwa kwa lengo la kukuza uchumi wa eneo husika na Taifa kwa ujumla. 

Aidha kodi za makampuni yanayofanya kazi au biashara yoyote wilayani humo, malipo yafanyike Mbinga ikiwa ni lengo la kumfanya mfanyabiashara mkubwa na mdogo, asiweze kuumizwa kwa kutozwa kodi kubwa.

Hayo yalisemwa katika kikao cha Wafanyabiashara hao kilichoketi ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) mjini hapa, ambapo walieleza kwamba wafanyabiashara wa wilaya hiyo hutozwa kodi kubwa ya mapato kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, ambapo walitolea mfano kwa wale ambao hujishughulisha na ununuzi wa zao la kahawa wilayani humo, kwenda makao makuu ya kampuni zao yaliyopo nje ya Mbinga kulipia kodi zao. 

Vilevile mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Menlick Sanga, aliongeza kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa na mwekezaji mkubwa wa mgodi wa makaa ya mawe Ngaka, ambayo uchimbaji wake hufanyika katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Rwanda wilayani humo, bado amekuwa halipi kodi hapa wilayani na wilaya kutonufaika na chochote hivyo ni vyema serikali ikaliangalia hilo ili malipo husika kwa mwekezaji huyo aweze kuyafanya hapa hapa wilayani.

Saturday, November 15, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA MBINGA KATIKA HILI UMEKENGEUKA



Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WASOMAJI wetu wa mtandao huu mara ya mwisho tuliwaeleza kwamba tutaendelea kuwaletea tuhuma zingine ambazo zinaonesha kuleta mashaka dhidi ya Afisa elimu msingi Mathias Mkali wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambazo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo Hussein Ngaga anamtuhumu huku akijua fika kwamba anamuonea na hazina ukweli wowote ambapo binafsi haziningii akilini kwa mtu mwenye akili zake timamu, endelea kufuatilia sakata hili kupitia mtandao huu.............

Awali tuliwafafanulia juu ya chanzo cha mgogoro huu kwamba kuhusiana na tuhuma inayojieleza kwamba Afisa elimu huyo ameunda NGO yake inayofahamika kwa jina la UWEKAMBI ambapo kirefu chake ni Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga.

Sasa nachukua safu hii kutaka kuelezea tuhuma zingine ambazo Mkurugenzi huyo amemtuhumu Afisa elimu huyo na inanilazimu niziweke bayana juu ya ukweli wake.

Nikiachana na tuhuma hiyo ya Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga, naingia katika tuhuma ya Ununuzi na matumizi ya mafuta ambapo Hussein Ngaga anamtuhumu Mkali kwamba ameiba mafuta na kuyatumia yenye thamani ya shilingi milioni 25,547,500 yakiwemo Petroli lita 5,500 na Diesel lita 5,500 yaliyoagizwa Mei 26 mwaka huu na mafuta ya nyongeza Petroli lita 4,500 na Diesel lita 4,500 ikiwemo na vilainisho vyenye thamani ya shilingi milioni 22,250,000 yaliyoagizwa Agosti 12 mwaka huu ambapo ukweli ni kwamba;

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa mafuta haya yote yaliombwa kwa Mkurugenzi huyo, ili kuwezesha uendeshaji wa mitihani 11 ya Mock kata, Mock mkoa ambapo ulifanyika mtihani mmoja na shughuli za kujisomea watoto wakati wa likizo yaani Makambi kwa darasa la saba.

Aidha mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa darasa la saba, mtihani wa ufundi na matumizi ya ofisi kama dharula za misiba na uhamisho kwa shule 227 na kata za kielimu 38 ikiwemo pia na vituo vya makambi 42 mafuta hayo yalitumika katika shughuli hizo.

Katika mahitaji hayo ni mtihani pekee wa kumaliza elimu ya msingi ndio Mkurugenzi Hussein Ngaga, alinunua mafuta Petroli lita 1,000 na Diesel lita 5,000 mnamo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo mafuta hayo yalitumika kusambaza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na yalitumika ndani ya siku tatu na yakaisha.

Mahitaji ya mafuta hayo hapo juu yaliombwa kwa kuzingatia kuwa toka mwezi Machi 2014, idara ya elimu msingi wilayani Mbinga haikupewa mafuta ya uendeshaji mitihani ya mock kata, wilaya na mock mkoa ambapo pamoja na idara kutopewa mafuta haikusimamisha utekelezaji wa shughuli zake za kila siku yaani matokeo makubwa sasa (BRN).

NGAGA KIBULI HIKI KWA MAMBO UNAYOYAFANYA UNAKIPATA WAPI, MBINGA UNAIPELEKA WAPI?


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TAARIFA zilizotufikia hivi punde Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga ameitisha kikao na Waratibu elimu kata wakiwemo pia Watendaji wa kata wa wilaya hiyo kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ya maendeleo husika, ikiwemo suala la waratibu hao na watendaji kwa lengo la kutaka kuwarubuni kwa namna moja au nyingine juu ya kukubalina naye katika mgogoro ambao unaendelea sasa kati yake na Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Mathias Mkali. 

Kikao hicho ambacho kinafanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza kuwa kukutana na watu hao kunatokana na Mkurugenzi huyo kuendelea kupanga njama na kutangaza kwamba Afisa elimu huyo ni mwizi, ili watendaji hao na waratibu wamkubali kwa kile anachokitaka yeye jambo ambalo wengi wao wamekuwa wakishangazwa nalo, huku wengine wakieleza kuwa ni vyema Ngaga akaachana na mambo hayo badala yake awe mbunifu wa mambo ya kimaendeleo na sio kuendekeza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii.

Walisema, Mkurugenzi huyo tokea afike wilayani hapa ni mtu wa kuendekeza majungu na migogoro isiyokuwa na msingi kwa wananchi wa Mbinga, huku wakihofia kwamba endapo ataendeleza mambo hayo huenda wilaya hiyo ikarudi nyuma kimaendeleo.

Katika hatua nyingine wengi wao walieleza kuwa tokea afike katika wilaya hii ni mwaka mmoja sasa umepita, lakini amekuwa ni mtu wa kupenda migogoro na kupanga safu katika idara mbalimbali kwa lengo la kutaka kuweka wakuu wa idara ambao yeye anawataka kwa maslahi yake binafsi.

Friday, November 14, 2014

GAUDENCE KAYOMBO: KATIKA HILI MKURUGENZI WAKO WA MBINGA AMEKENGEUKA

Gaudence Kayombo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SIRI imefichuka juu ya mgogoro ambao unaendelea kufukuta, kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, na Afisa wake wa elimu ya msingi Mathias Mkali kwamba baadhi ya Madiwani wa kata ya Mkako na Mkumbi wilayani humo ndio wanaohusika kwa kiasi kikubwa kuuendeleza mgogoro huo, ambao sasa unahatarisha kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu msingi wilayani humo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo walimtaja diwani wa kata ya Mkako Ambrose Nchimbi na Bruno Kapinga kutoka Mkumbi, ndio wanaohusika kwa karibu zaidi katika kuufanya mgogoro huu uendelee kufukuta na baadhi ya watendaji wa serikali kujengeana chuki.

Walisema kitendo hicho wanachokifanya Madiwani hao kwa kushirikiana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga kutaka kumng’oa Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga, wamekuwa wakitengeneza mambo yasiyokuwa na ukweli na ni dhambi ambayo itakuja kuwatafuna baadae.

Aidha walieleza kuwa kitendo cha Nchimbi na Kapinga kujiingiza katika mgogoro huu, ni sawa na kuwasaliti madiwani wenzao na wananchi wa Mbinga kwa ujumla hivyo wanachotakiwa waachane na mambo hayo badala yake, wajikite katika kupigania maendeleo ya wanambinga na sio kuendekeza mambo ambayo hayana manufaa kwa jamii.

Awali ya yote chanzo cha mgogoro huo ni kwamba Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga amemtengenezea Bw. Mkali tuhuma kadhaa ikiwemo kuwa Afisa elimu huyo ameunda NGO inayofahamika kwa jina la (UWEKAMBI) na kutumia fedha za Capitation, michango ya wananchi na TSM 9 ambazo zote ni fedha za serikali bila idhini ya miamala husika ambapo ukweli ni kwamba umoja huo, uliundwa kisheria kupitia ofisi ya Mkurugenzi huyo Aprili 24 mwaka 2012 na kupewa baraka katika vikao vya baraza la madiwani.

Wednesday, November 12, 2014

BUNDI AENDELEA KUMSAKAMA MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA


 Jumanne Sagini Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-TAMISEMI)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TUHUMA nzito ambayo inaendelea kufukuta juu ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Hussein Ngaga, kudaiwa kutopeleka fedha za Capitation kwa wakati mashuleni wilayani humo kadiri ya miongozo ya Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM) unavyosema, umeibua mapya ambapo taarifa zilizotufikia hivi punde Mkurugenzi huyo anahaha hapa na pale kwa kuwatumia wahasibu wake wa halmashauri hiyo, kuhakikisha kwamba fedha hizo zinarejeshwa kwenye akaunti husika haraka iwezekanavyo.

Vyanzo vya uhakika kutoka katika halmashauri ya wilaya hiyo vimeeleza kuwa shilingi milioni 54,725,000 ndizo anazodaiwa Ngaga kutozipeleka kwa wakati na hivi sasa zimekaa zaidi ya mwaka bila kupelekwa mashuleni.

Walisema licha ya wakaguzi wa mkoa huo kukagua katika kipindi kilichopita na kutoa hoja hiyo Novemba 11 mwaka 2013,  pamoja na kikao cha kamati ya mipango na fedha kilichoketi Julai 10 mwaka huu kupitia hoja hiyo hakuna utekelezaji uliofanyika hadi sasa.

“Hivi ninavyo kuambia dokezo juu ya fedha hizi linakimbizwa kwa haraka sana ili kuweza kuziba pengo hili ambalo linaleta doa kwake, na hatujui hizi pesa kwa nini zimekaa muda mrefu bila kupelekwa kwa wahusika kwa muda muafaka”, kilisema chanzo chetu ambacho kiliomba jina lake lisitajwe.

Monday, November 10, 2014

OFISI YA MKAGUZI WA NDANI MBINGA KUNA MATATIZO NI VYEMA YAKAFANYIWA KAZI

Rais Jakaya Kikwete, wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


OFISI ya Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imeshushiwa shutuma nzito kwamba inashindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa, badala yake inatoa taarifa zenye mapungufu na kuleta migogoro isiyokuwa na tija, mtandao huu umeambiwa.

Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo Laston Kilembe, ndiye anayeshushiwa shutuma hizo na baadhi ya madiwani wa wilaya hiyo, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti.

Walisema hata Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, alimuagiza mkaguzi huyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Julai 26 mwaka huu mjini hapa, kwamba ahakikishe anatoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Sunday, November 9, 2014

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA APOKELEWA KWA MABANGO, VIGOGO WILAYA YA MBINGA MATUMBO JOTO

Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Hussein Mwinyi akisalimiana na wana CCM wakati alipowasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho wilayani Mbinga.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho akisistiza jambo ndani ya kikao cha Halmashauri kuu ya mkoa wa Ruvuma kilichofanyika ukumbi wa Jumba la maendeleo wilayani Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Dokta Hussein Mwinyi, ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, amepokelewa kwa mabango wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yakiwatuhumu baadhi ya vigogo wa ngazi ya juu wilayani humo kufuatia mgogoro mkubwa uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri na Afisa elimu wa shule za msingi wa wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi ambao ni wanachama wa CCM, ndio walioshika mabango hayo ambayo yalikuwa na ujumbe uliosomeka kuwa; Afisa elimu wetu anaonewa, Mkurugenzi wa halmashauri hatumtaki ondoka nae, Afisa usalama wa taifa (DSO) hatufai ondoka nae, Hawa ndio wanaoimaliza CCM Mbinga, Wananchi wanaichukia CCM kupitia hawa watu na mwishoni kabisa yalikuwa yakimalizia kwa kauli ya Tafadhali sikiliza vilio vyetu wanambinga.

Hayo yote yalitokea wakati Waziri Mwinyi anawasili katika viwanja vya makao makuu ya Ofisi za Chama cha mapinduzi wilayani Mbinga, leo majira ya saa 5: 30 ambapo wanachama hao walionekana kujawa jazba huku wakipinga mgogoro huo ambao unaendelea kufukuta mpaka sasa wilayani humo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanachama hao ambao walionekana wameshika mabango hayo ambayo yalisheheni ujumbe huo wa kuwakataa viongozi hao wa wilaya hiyo, ghafla alijitokeza Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani hapa Joseph Mkirikiti ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akiwa ameongozana na Afisa usalama wa taifa wa wilaya ya Mbinga (Jina tunalo) walikwenda mbele ya mabango hayo na kuyanyang’anya na baadae wanachama hao walikamatwa na kufikishwa kituo kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, zinaarifu kuwa wanachama hao walikuwa wakihojiwa na kuchukuliwa maelezo kituoni hapo na kuambiwa kesho Novemba 10 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi wakaripoti tena.

Aidha wanachama hao wanatuhumiwa kuwa ndio waliohusika kusambaza waraka uliosheheni tuhuma mbalimbali, ambazo zinamtuhumu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga kuwa anamuonea Afisa elimu wa shule za msingi wilayani humo Daud Mathias Mkali.

Wednesday, November 5, 2014

HALMASHAURI MBINGA YATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA MAGARI YA ABIRIA

Mkurugenzi mtendaji, Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa onyo kali kwa wamiliki wa magari ya abiria kuhakikisha kuwa vijana wanaowatumia kupiga debe katika eneo la stendi kuu mjini hapa, kuacha kunyanyasa abiria kwani vitendo hivyo vinawadhalilisha na kuwanyima uhuru wa kuchagua basi walipendalo wakati wanaposafiri.

Meneja wa stendi kuu ya magari ya abiria iliyopo mjini hapa, Dustan Mapunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alisema onyo hilo limetolewa baada ya kupokea malalamiko kuwa wapiga debe wamekuwa na kawaida ya kuwadhalilisha na kuwasumbua abiria jambo ambalo wakati mwingine husababisha mizigo yao kupotea.

Mapunda alisema hatua kali zitachukuliwa kwa kampuni au basi lolote ambalo litaonekana kuleta usumbufu kwa abiria na kwamba lazima wafanyakazi wawe na vitambulisho na orodha yao ipelekwe katika kituo kidogo cha Polisi cha stendi.

NKAMIA: VIJANA MSIKUBALI KUTUMIWA NA WANASIASA WENYE UCHU NA MADARAKA

Na Dunstan Ndunguru,
Nyasa.

SERIKALI imewaasa vijana nchini kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka, ambao wamekuwa na kawaida ya kuwahamasisha washiriki maandamano yasiyo na tija jambo ambalo huhatarisha uvunjifu wa amani.

Pia imevitahadharisha vyombo vya habari kutotumiwa vibaya na wale wenye nia ya kukwamisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, ambao kwa sasa unategemewa kupigiwa kura na wananchi.

Hayo  yalisemwa na Naibu waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo Juma Nkamia wakati wa uzinduzi wa mradi wa pikipiki kwa vijana wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, uliofanyika katika kijiji cha Mbamba bay.

CCM YAWATAKA WANACHAMA WAKE KUACHA MIFARAKANO



Na Dunstan Ndunguru,
Songea.

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma Verena Shumbusho, amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kwa ngazi zote mkoani humo kuepuka kujenga mifarakano inayojitokeza nyakati za chaguzi mbalimbali, ili uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu ushindi wa kimbunga uweze kupatikana.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Majira kuhusiana na zoezi zima la upigaji wa kura za maoni ndani ya chama hicho, ambazo hutoa wagombea watakaosimama wakati wa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa.

Verena alisema kuwa uzoefu unaonesha kuwa wakati wa uendeshaji wa kura za maoni ndani ya chama hicho, unapomalizika unaacha makovu ambayo hutumiwa na wapinzani kupata ushindi hivyo jambo hilo ni vyema likaepukwa mapema ili wapinzani hao, wasipate mwanya kama ilivyojitokeza miaka iliyopita.

WANAFUNZI WAANDAMANA KUTOKANA NA CHOO WANACHOKITUMIA KUJAA NA KUSABABISHA HARUFU KALI

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WANAFUNZI wanaosoma katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameandamana kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na choo wanachokitumia kujaa na kusababisha harufu kali katika eneo la chuo hicho.

Tukio hilo lilitokea Novemba 3 mwaka huu majira ya asubuhi, ambapo walieleza kwa nyakati tofauti kuwa walifikia hatua ya kufanya hivyo kutokana na uongozi husika wa chuo hicho, kutochukua hatua za haraka katika kunusuru hali hiyo.

Walisema baada ya kuona tatizo hilo halifanyiwi kazi kwa muda mrefu, waliona ni vyema wapeleke kilio chao kwa Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga, ili tatizo hilo la choo kufurika lifanyiwe kazi haraka.

Tuesday, November 4, 2014

VIONGOZI WA SERIKALI, WANASIASA WATAKIWA KUHESHIMU MIPAKA YA KAZI ZAO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa uelewa mdogo kwa viongozi wa serikali na vyama vya siasa juu ya mipaka ya kazi zao, kumekuwa kukisababisha jamii kukosa haki zao za msingi na kusababisha wengi wao kuwa maskini.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kituo cha wasaidizi wa kisheria na haki za binadamu (WAKIHAMBI) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Daniel Chindengwike alipokuwa akisoma taarifa fupi ya ufunguzi wa kituo hicho wilayani humo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli mjini hapa.

Chindengwike alisema kituo hicho kilianzishwa wilayani humo, kwa lengo la kusaidia jamii katika mambo ya kisheria, ili waweze kupata haki zao ambazo huporwa na wajanja wachache.

Sunday, November 2, 2014

WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUNYWA POMBE KUPITA KIASI



Na Willy Sumia,
Sumbawanga.

WATU wawili wamefariki dunia kutokana na kulewa pombe na kuwa chakari wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, kitendo ambacho kiliwasababishia kuzama katika mto wakati walipokuwa wakirejea nyumbani.

Kitendo cha kuzama mtoni, watu hao wanadaiwa kupoteza maisha baada ya kushindwa kuvuka mto walipokuwa wakirejea kutoka kunywa pombe nyakati za usiku katika tarafa ya Mtowisa wilayani humo.

Waliopoteza maisha wametajwa kuwa ni Leonard Salehe (44) mkazi wa kijiji cha Zimba na Gilbert Machimu (47) mkazi wa kijiji cha Sakalilo.

OPEN DOORS YAPONGEZWA KWA KUTOA MSAADA WA PIKIPIKI TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

UMOJA wa makanisa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, umelipongeza shirika  lisilokuwa la serikali la Open Doors  kwa kufanikisha upatikanaji wa msaada wa pikipiki tano zenye thamani ya shilingi milioni 10 zilizoletwa wilayani humo, kwa ajili ya kuwagawia wachungaji wa makanisa ya kikristo.

Lengo la utoaji wa pikipiki hizo ni sehemu ya msaada wa kuwezesha madhehebu hayo yaweze kutoa huduma za kichungaji kwa waumini wao. 

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa umoja wa makanisa hayo, Mchungaji Mathias Nkoma wa Kanisa la Anglikana mjini hapa, alipokuwa akizungumza katika hafla fupi ya ugawaji wa pikipiki hizo kwa wachungaji wa makanisa hayo iliyofanyika uwanja wa kanisa la Bibilia mjini hapa.