Wednesday, November 5, 2014

CCM YAWATAKA WANACHAMA WAKE KUACHA MIFARAKANO



Na Dunstan Ndunguru,
Songea.

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma Verena Shumbusho, amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kwa ngazi zote mkoani humo kuepuka kujenga mifarakano inayojitokeza nyakati za chaguzi mbalimbali, ili uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu ushindi wa kimbunga uweze kupatikana.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Majira kuhusiana na zoezi zima la upigaji wa kura za maoni ndani ya chama hicho, ambazo hutoa wagombea watakaosimama wakati wa uchaguzi ujao wa serikali za mitaa katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa.

Verena alisema kuwa uzoefu unaonesha kuwa wakati wa uendeshaji wa kura za maoni ndani ya chama hicho, unapomalizika unaacha makovu ambayo hutumiwa na wapinzani kupata ushindi hivyo jambo hilo ni vyema likaepukwa mapema ili wapinzani hao, wasipate mwanya kama ilivyojitokeza miaka iliyopita.


Alisema ana imani kuwa kura za maoni zilizofanyika mkoani humo zitasaidia chama kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi huo, kutokana na wagombea wake kukubalika na wananchi wenyewe na kwamba kinachotakiwa sasa ni kuangalia wapi kuna kasoro kwa lengo la kutafuta suluhisho litakalokinufaisha CCM.

“Mpaka sasa hakuna malalamiko yaliyonifikia kuhusiana na zoezi hili muhimu kwa chama chetu, ila tu niwaombe sana viongozi na wanachama wenzangu wawe makini katika uchujaji wa majina ya wagombea kwani uzoefu unaonesha hiki ni kipindi ambacho wenzetu wapinzani, wanatusubiri wasikie wapi tunagombana ili wapate na wenyewe nafasi ya kusema”, alisema Verena.

Alisema wananchi wa mkoa wa Ruvuma, wana imani kubwa na chama cha mapinduzi kutokana na jinsi ambavyo ilani yake ya  uchaguzi ilivyotekelezwa kwa vitendo, hivyo wajitokeze kwa wingi  siku ya uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa kuwapigia kura za kutosha wagombea wa CCM ambapo kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa mwelekeo wa kushinda katika uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani.

Verena alisema kwa maeneo yale ambayo yanaongozwa na wapinzani mikakati kabambe imewekwa, ili kuyarejesha nyumbani kwake ambako ni CCM hivyo kinachotakiwa ni kuwepo kwa ushiriano wa dhati baina ya wanachama wa chama hicho, viongozi na wananchi kwa ujumla.

No comments: