Saturday, November 15, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA MBINGA KATIKA HILI UMEKENGEUKA



Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WASOMAJI wetu wa mtandao huu mara ya mwisho tuliwaeleza kwamba tutaendelea kuwaletea tuhuma zingine ambazo zinaonesha kuleta mashaka dhidi ya Afisa elimu msingi Mathias Mkali wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambazo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo Hussein Ngaga anamtuhumu huku akijua fika kwamba anamuonea na hazina ukweli wowote ambapo binafsi haziningii akilini kwa mtu mwenye akili zake timamu, endelea kufuatilia sakata hili kupitia mtandao huu.............

Awali tuliwafafanulia juu ya chanzo cha mgogoro huu kwamba kuhusiana na tuhuma inayojieleza kwamba Afisa elimu huyo ameunda NGO yake inayofahamika kwa jina la UWEKAMBI ambapo kirefu chake ni Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga.

Sasa nachukua safu hii kutaka kuelezea tuhuma zingine ambazo Mkurugenzi huyo amemtuhumu Afisa elimu huyo na inanilazimu niziweke bayana juu ya ukweli wake.

Nikiachana na tuhuma hiyo ya Umoja wa Waratibu Elimu Kata wilaya ya Mbinga, naingia katika tuhuma ya Ununuzi na matumizi ya mafuta ambapo Hussein Ngaga anamtuhumu Mkali kwamba ameiba mafuta na kuyatumia yenye thamani ya shilingi milioni 25,547,500 yakiwemo Petroli lita 5,500 na Diesel lita 5,500 yaliyoagizwa Mei 26 mwaka huu na mafuta ya nyongeza Petroli lita 4,500 na Diesel lita 4,500 ikiwemo na vilainisho vyenye thamani ya shilingi milioni 22,250,000 yaliyoagizwa Agosti 12 mwaka huu ambapo ukweli ni kwamba;

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa mafuta haya yote yaliombwa kwa Mkurugenzi huyo, ili kuwezesha uendeshaji wa mitihani 11 ya Mock kata, Mock mkoa ambapo ulifanyika mtihani mmoja na shughuli za kujisomea watoto wakati wa likizo yaani Makambi kwa darasa la saba.

Aidha mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa darasa la saba, mtihani wa ufundi na matumizi ya ofisi kama dharula za misiba na uhamisho kwa shule 227 na kata za kielimu 38 ikiwemo pia na vituo vya makambi 42 mafuta hayo yalitumika katika shughuli hizo.

Katika mahitaji hayo ni mtihani pekee wa kumaliza elimu ya msingi ndio Mkurugenzi Hussein Ngaga, alinunua mafuta Petroli lita 1,000 na Diesel lita 5,000 mnamo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo mafuta hayo yalitumika kusambaza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na yalitumika ndani ya siku tatu na yakaisha.

Mahitaji ya mafuta hayo hapo juu yaliombwa kwa kuzingatia kuwa toka mwezi Machi 2014, idara ya elimu msingi wilayani Mbinga haikupewa mafuta ya uendeshaji mitihani ya mock kata, wilaya na mock mkoa ambapo pamoja na idara kutopewa mafuta haikusimamisha utekelezaji wa shughuli zake za kila siku yaani matokeo makubwa sasa (BRN).


Aidha kutokana na Mkurugenzi huyo kutotaka kuipatia idara hiyo mafuta kwa sababu anazozijua yeye na matakwa yake binafsi, ililazimika kukopa na kununua mafuta kwa fedha taslimu kuanzia mwezi Machi hadi Septemba mwaka huu hadi wakati Dokezo la kwanza la lita 5,500 petroli na 5,500 diesel na Dokezo la pili la lita 4,500 petroli na lita 4,500 diesel yanaandikwa idara haikuwa na mafuta.

Hivyo idara ya elimu ya msingi baada ya kuona shughuli zake inashindwa kuendesha ipasavyo iliamua kufanya hivyo, huku ikitegemea kwamba mafuta iliyoomba endapo ingeyapata kutoka kwa Mwajiri wake, ingeweza kulipia deni la mafuta yaliyonunuliwa kwa fedha taslimu kwa kazi husika.

Wakati mafuta hayo yananunuliwa kwa fedha taslimu idara ilitumia mtindo wa kuwasilisha risiti na hati iliyosainiwa na Waratibu elimu kata ambao walipokea mafuta hayo ikiwa ni kumbukumbu na kuiwasilisha kwa boharia ili mafuta yaliyoombwa kwa madokezo yaliyotajwa hapo juu yakinunuliwa yatumike kama ushahidi kwa Mwajiri.

Uchunguzi umebaini kuwa pamoja na ukweli kuwepo kwa kazi zinazoonekana ambazo zimefanyika na idara ya elimu msingi wilayani Mbinga, lakini Mkurugenzi wa wilaya hiyo Ngaga alikataa kuyalipa mafuta hayo huku akitumia kigezo cha makosa yaliyofanywa na boharia wake kwa makusudi, ambapo badala ya kutunza kumbukumbu alizopewa boharia huyo aliamua kutumia issue voucher, ledger na nyaraka zingine za kiboharia kwa kuwasainisha madereva.

Katika hili inadhihirisha kuwa kulikuwa na mpango uliosukwa kati ya boharia husika (Jina tunalo) na Mkurugenzi huyo wa halmashauri hiyo, kwani cha kushangaza baada ya tukio hilo Hussein Ngaga aliamua kuchukua jukumu la kumhamisha mtumishi huyo kwenda idara nyingine wilayani hapa, na kuanza kutengeneza madai kwamba Afisa elimu msingi Bw. Mkali alikusudia kuiba mafuta kwa nyaraka alizoziandika boharia huyo, mpango ambao ulikuwa ukiimarishwa na Mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya hiyo Laston Kilembe.

Kwa ujumla mafuta yote yaliyotajwa hapo juu, imebainika kuwa kwenye madokezo hayakununuliwa kama ilivyodaiwa kwamba Afisa elimu msingi ameiba, na mpaka sasa hayajaidhinishwa na kununuliwa na Mkurugenzi huyo na kwa ushahidi hakuna Voucher wala Check iliyotoa mafuta hayo.

Badala yake Mkurugenzi Hussein Ngaga yeye mwenyewe aliagiza lita 6,000 tu kwa ajili ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ambayo imefanyika hivi karibuni, na yalitumika kwa siku tatu za mitihani iliyokuwa ikifanyika, ambapo idara haikubaki na mafuta badala yake imebaki na madeni ambayo Mkurugenzi ameyakataa kuyalipa.

Utafiti umeendelea kubaini kuwa katika kipindi cha mwezi Septemba mwaka 2014 idara elimu ya msingi wilayani humo, haikupewa mafuta ilikuwa ikilazimika kununua mafuta kwa fedha taslimu na kupata risiti toka kwa muuzaji ambapo mafuta yaliyonunuliwa kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali za idara ni kama ifuatavyo;

  • Mitihani ya Mock mkoa na kata mitihani 12 zilitumika petrol lita 6,745.

  • Masomo ya ziada yaani Makambi wakati wa likizo kwa vituo 42 zilitumika petroli lita 1,260 kwa ajili ya shughuli za kuendeshea umeme kwa njia ya Jenereta.

  •  Matumizi ya lita 2,103 za diesel yalitumika kwa ajili ya usafirishaji mitihani na matumizi ya ofisi katika idara.

Kwa ujumla katika kufanikisha maendeleo yasiweze kudorola katika sekta ya elimu msingi wilayani Mbinga, idara ililazimika kukopa fedha na huduma mbalimbali kutoka kwa mchapaji wa mitihani, fedha za UMITASHUMTA na posho za Waratibu elimu kata walizolipwa kupitia kusimamia mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2014 baada ya mwajiri kukataa kulipa fedha hizo kila mratibu alilazimika kulipia deni la mafuta aliyoyatumia kwa mitihani ya mock mkoa na kata.

Imeelezwa kuwa mafuta haya yote yalitarajiwa yalipwe kupitia madokezo yaliyozuiliwa na huyo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, baada ya kumtuhumu Afisa elimu msingi kwa madai ya kuyanunua mafuta hewa jambo ambalo sio kweli.

Jambo hili limekuwa likielezwa kuwa Waratibu elimu kata wakati wote wa utendaji wa kazi za idara hiyo ya elimu ya msingi, katika shughuli za uendeshaji wa mitihani wilayani humo, wamekuwa wakitumia fedha zao binafsi kutoka mifukoni mwao na sehemu ya fedha za UMITASHUMTA hali ambayo wengi wao wanasema inawavunja moyo na kukatisha tamaa ya kujitoa kufanya kazi.

Pamoja na mambo mengine katika tuhuma hii ya mafuta, pia Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga anamtuhumu Afisa elimu msingi wilaya hiyo Mathias Mkali, kuwa ametoa mafuta kwa pikipiki za Waratibu elimu kata kinyume na miongozo ya fedha.

Katika tuhuma hii mtandao huu umebaini kuwa jambo hili sio kweli ambapo kikao cha kamati ya mipango na fedha cha Desemba 20 mwaka 2013, ndicho kilichoridhia pikipiki binafsi za waratibu elimu kata kupewa mafuta kwa kazi za serikali lengo kufanikisha ukuaji wa taaluma wilayani humo.

Tumebaini kuwa kwa tuhuma hiyo inaonesha wazi kuwa mwajiri yaani Mkurugenzi huyo, hana nia ya kuwawezesha mafuta watendaji wake (Waratibu elimu kata) licha ya kujitolea pikipiki zao binafsi kufanyia kazi za serikali.

Kwa ujumla shughuli za uendeshaji wa mitihani ya mock kata zimeanza tangu mwezi Januari 2013 hadi sasa, na kuna miaka miwili taratibu zilizokuwa zinatumika ni hizi hizi na hakuna malalamiko yaliyojitokeza kutoka kwa wazazi, wananchi na hata walimu wilayani humo kama anavyodai mkurugenzi huyo. 

Badala yake haijawahi kutokea kwa Mkurugenzi Hussein Ngaga kutoa ushauri wowote kwa lengo la kurekebisha na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa mitihani wilayani Mbinga, ambapo mfumo uliopo sasa umeonekana kuleta matunda mazuri ya ufaulu cha kushangaza badala ya kusimamia misingi ya maendeleo katika sekta hiyo muhimu ya elimu, muda mwingi amekuwa akielekeza tuhuma dhidi ya Afisa elimu msingi Bw. Mkali na kufikia hatua ya kumsimamisha kazi jambo ambalo sasa limekuwa likizua mgogoro mkubwa na kuwagawa viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo kuwa katika makundi mawili ambayo hayana tija kwa wananchi wa Mbinga.


No comments: