Wednesday, November 12, 2014

BUNDI AENDELEA KUMSAKAMA MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA


 Jumanne Sagini Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-TAMISEMI)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TUHUMA nzito ambayo inaendelea kufukuta juu ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Hussein Ngaga, kudaiwa kutopeleka fedha za Capitation kwa wakati mashuleni wilayani humo kadiri ya miongozo ya Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM) unavyosema, umeibua mapya ambapo taarifa zilizotufikia hivi punde Mkurugenzi huyo anahaha hapa na pale kwa kuwatumia wahasibu wake wa halmashauri hiyo, kuhakikisha kwamba fedha hizo zinarejeshwa kwenye akaunti husika haraka iwezekanavyo.

Vyanzo vya uhakika kutoka katika halmashauri ya wilaya hiyo vimeeleza kuwa shilingi milioni 54,725,000 ndizo anazodaiwa Ngaga kutozipeleka kwa wakati na hivi sasa zimekaa zaidi ya mwaka bila kupelekwa mashuleni.

Walisema licha ya wakaguzi wa mkoa huo kukagua katika kipindi kilichopita na kutoa hoja hiyo Novemba 11 mwaka 2013,  pamoja na kikao cha kamati ya mipango na fedha kilichoketi Julai 10 mwaka huu kupitia hoja hiyo hakuna utekelezaji uliofanyika hadi sasa.

“Hivi ninavyo kuambia dokezo juu ya fedha hizi linakimbizwa kwa haraka sana ili kuweza kuziba pengo hili ambalo linaleta doa kwake, na hatujui hizi pesa kwa nini zimekaa muda mrefu bila kupelekwa kwa wahusika kwa muda muafaka”, kilisema chanzo chetu ambacho kiliomba jina lake lisitajwe.


Katika hatua nyingine Ngaga analalamikiwa na baadhi ya walimu wa shule za msingi wilayani hapa kwamba hajawalipa fedha zao za kazi waliyoifanya ya kufundisha muda wa ziada wakati walikizo.

Walifafanua kuwa fedha wanazozidai ni za Desemba mwaka 2013 na kwamba baada ya idara husika kuandaaa malipo na fedha hizo kutoka, aliamua kuzichukua yeye mwenyewe kwa mtindo kwamba anaziazima lakini cha ajabu hadi leo hii walimu hao hawajalipwa. 

Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo ambayo hayaleti picha nzuri kwa mtendaji wa serikali ambaye umewekwa madarakani kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, hakuweza kupatikana ofisini kwake.

Hata hivyo taarifa za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali zinasema kuwa kamati ya siasa ya wilaya hiyo leo Novemba 12 mwaka huu imechukua maamuzi ya kuketi na kujadili jambo hilo kufuatia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Dokta Hussein Mwinyi alipokuwa wilayani hapa Novemba 9 mwaka huu, kumuagiza Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga kwamba mgogoro huo unapaswa kumalizwa mapema na sio viongozi kuendelea kulumbana badala ya kufikiria kufanya shughuli za maendeleo kwa manufaa ya wananchi na kizazi kijacho.

Hata hivyo Mwinyi alimuagiza Mkuu wa wilaya Ngaga, kuhakikisha Afisa elimu msingi wilayani humo Bw. Mkali, anarejeshwa ofisini haraka iwezekanavyo huku tuhuma ambazo anatuhumiwa akiendelea kuzijibu wakati akiwa ofisini.

No comments: