Monday, November 17, 2014

KWA MAMBO HAYA YANAYOFANYWA NA MKURUGENZI HUYU WA MBINGA, HAKIKA SEKTA YA ELIMU HUENDA IKADOROLA WILAYANI HUMO


Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akisisitiza jambo wakati akiwa katika vikao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahy na Mkurugenzi wake Hussein Ngaga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JINAMIZI linalodaiwa kutengenezwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga katika kuhakikisha linaendelea kumsakama Afisa elimu msingi Mathias Mkali na walimu wake, imeelezwa kuwa ni dalili tosha zinazoashiria kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu msingi wilayani humo, ambapo hivi sasa limeingia katika sura mpya kwa walimu wakuu wa shule hizo likitaka taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za TSM. 9 na Capitation zinazopelekwa mashuleni.

Mkurugenzi huyo amewaandikia barua walimu hao ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba MDCC/F. 10/20/43 ya Novemba 10 mwaka huu, ikiwataka waandae taarifa hiyo ya kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi sasa 2014/2015.

Baadhi ya walimu waliokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, wanamshangaa Mkurugenzi huyo kuwaandikia barua hiyo ambayo ameichelewesha kuwafikia walimu hao, ikiwataka kufanya kazi hiyo   jambo ambalo ni vigumu huku wengine wakibeza na kusema huenda anatafuta sababu kwa mwalimu atakayekosea na kushindwa kukamilisha kwa wakati apate cha kusemea.

Walisema wamechoshwa na mambo yake tokea aingie katika wilaya ya Mbinga, amekuwa ni mtu wa kuongoza wenzake kwa njia ya migogoro na kuwatafutia sababu zisizo na msingi badala ya kukaa na kubuni mipango ya kimaendeleo, huku wakiongeza kuwa kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi wake wa ndani, Laston Kilembe alipokuwa akipita hivi karibuni kuhoji mashuleni kwa walimu wakati anafanya ukaguzi wake juu ya fedha hizo, lakini mkaguzi huyo hakufanya hivyo ndio maana hivi sasa walimu hao wanasumbuliwa akiwataka watekeleze hilo.


“Kitendo cha Mkurugenzi huyu kutaka taarifa hizi za mapato na matumizi kwa kutupeleka kwa uharaka wa siku chache namna hii, sio taratibu nzuri tukiwa sisi watumishi wa serikali kama alivyo yeye”, walisema.

Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa hayo yote yanajitokeza baada ya Hussein Ngaga kumsimamisha kazi Afisa elimu msingi Mathias Mkali akisema kuwa ni mwizi wa fedha za serikali na michango husika ya wananchi, huku wazazi, walimu na wananchi wa wilaya ya Mbinga wakipata taharuki na mshangao juu ya mambo anayoyafanya mkurugenzi huyo dhidi ya mtumishi mwenzake.

Kadhalika wazazi na wananchi kwa ujumla wanahoji kwamba, endapo kama Afisa elimu huyo ni mwizi, inakuwaje ameweza kufanikisha utendaji wa kazi zake kwa kufaulisha vizuri watoto wao tokea alipohamia Mbinga, kupitia michango yao waliyokuwa wakichanga na ile inayotolewa na shule kwa ajili ya mitihani ya kila mwezi kwa wanafunzi?

Tafiti zinaeleza kuwa Mkurugenzi huyo katika barua yake aliyowaandikia walimu wakuu mashuleni ambazo walimu hao wanalalamika zimechelewa kuwafikia, na kuwataka wawasilishe taarifa hiyo Novemba 19 mwaka huu wanatakiwa kuandaa na kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya fedha, walizopokea kutoka kwa wananchi (Wazazi) na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011 hadi 2014/ 2015.

Barua hiyo inasema anawataka wawasilishe taarifa ya; michango ya fedha za TSM. 9, michango ya fedha za mitihani, fedha za Capitation, ongezeko la fedha za mitihani darasa la saba kwa mwaka 2014 pamoja na fedha zingine tofauti na zilizotajwa katika barua yake aliyowaandikia walimu hao kitendo ambacho kinawashangaza walimu hao wakisema, kazi hiyo ilibidi aikamilishe Mkaguzi wake wa ndani wa halmashauri hiyo pale alipomtuma hivi karibuni apite mashuleni kufanya ukaguzi.

Aidha Ngaga katika barua yake amewataka walimu hao katika taarifa zao waonyeshe fedha zote zilizopokelewa na shule, na baadaye kuhamishiwa kwenye akaunti ya Umoja Waratibu Elimu Kata Wilaya ya Mbinga (UWEKAMBI) huku akijua fika fedha zinazopelekwa kwenye umoja huo ni mpango ambao ulibarikiwa katika vikao halali vya halmashauri hiyo, ikiwemo baraza la madiwani na kamati za shule mashuleni.

Vilevile pamoja na maagizo hayo Mkurugenzi huyo amewapa barua za kuwataka pia watendaji wa kata kufuatilia suala hilo, huku wengi wao wakilalamika wakisema kazi hiyo ni jukumu la Waratibu elimu kata, kamati za shule na walimu wake hivyo wao ni sawa na kuwatwisha mzigo wa kazi ambayo sio jukumu lao.

Mwandishi wa habari hizi baada ya kufuatilia sera, sheria na kanuni za Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi namba 25 ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 1995 inatamka wazi kuwa jukumu hilo ni la kamati za shule, mashuleni yenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za shule na kuitisha vikao vya wazazi, walezi na jamii pale inapotakiwa kutoa taarifa husika na sio kuwatuma watendaji wa kata kusimamia zoezi hili, hivyo kufanya hivyo ni kukiuka miongozo ya wizara. 

Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga Hussein Ngaga alipotafutwa ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana hadi pale habari hizi zilipokuwa zinaingia mitamboni.

No comments: