Wednesday, November 5, 2014

NKAMIA: VIJANA MSIKUBALI KUTUMIWA NA WANASIASA WENYE UCHU NA MADARAKA

Na Dunstan Ndunguru,
Nyasa.

SERIKALI imewaasa vijana nchini kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka, ambao wamekuwa na kawaida ya kuwahamasisha washiriki maandamano yasiyo na tija jambo ambalo huhatarisha uvunjifu wa amani.

Pia imevitahadharisha vyombo vya habari kutotumiwa vibaya na wale wenye nia ya kukwamisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, ambao kwa sasa unategemewa kupigiwa kura na wananchi.

Hayo  yalisemwa na Naibu waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo Juma Nkamia wakati wa uzinduzi wa mradi wa pikipiki kwa vijana wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, uliofanyika katika kijiji cha Mbamba bay.


Nkamia alisema mara nyingi baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa na tabia ya kuwarubuni vijana, ili wavunje sheria za nchi huku wao wenyewe wakibaki nyuma na kwamba pamoja na hamasa zao hizo pindi vijana hao wanapopatwa na matatizo baada ya kukumbana na vyombo vya dola, viongozi hao waliowahamasisha hushindwa kuwasaidia.

Alisema dhamira ya serikali ni kuona vijana wanaondokana na umasikini na ndio maana Wizara hiyo, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa ajili ya kusaidia vikundi mbalimbali vya ujasiriamali hapa nchini ambavyo vimeibuliwa na vijana.

“Ninyi vijana ni tegemeo kubwa katika kufanikisha maendeleo ya taifa letu, hivyo kamwe msikubali kutumiwa na mtu kwa maslahi yake bali kinachotakiwa jikiteni moja kwa moja, katika shughuli za uzalishaji mali na sio vionginevyo”, alisema Nkamia.

Nkamia aliwataka vijana waliobahatika kupata mkopo wa pikipiki hizo kurejesha mkopo kwa wakati, ili hatimaye wale ambao hawakupata waweze kukopeshwa hapo baadae na kwamba wazingatie sheria za usalama barabarani, jambo ambalo litasaidia waepukane na ajali zinazojitokeza mara kwa mara.

Kuhusu  vyombo vya habari alisema kamwe serikali haitasita kuchukua hatua kwa chombo cha habari kitakachokiuka maadili kwa kuchapisha taarifa zinazolenga kuhatarisha amani na utulivu,   wakati huu ambao wananchi wanapaswa kujiandaa kuipigia kura katiba inayopendekezwa, hivyo wanahabari washiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa jambo hilo.

Awali Mbunge wa jimbo la Nyasa Kapteni mstaafu John Komba alisema mradi wa vijana wa pikipiki unalenga kuwafikia vijana 300 kwa awamu ya kwanza, ambapo kwa sasa umetoa pikipiki 120 zenye thamani ya shilingi milioni 261.3.

Mkopo wa pikipiki hizo umetolewa na benki ya wanawake nchini na kwamba pikipiki hizo kwa vijana zitachangia kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii katika wilaya hiyo yenye vijana 50,038 wenye umri kati ya miaka 14 hadi 35.


Komba alisema pamoja na mkopo huo wa pikipiki lengo lingine la benki hiyo ni kuhakikisha inawakopesha vijana kupitia vikundi vyao boti za kisasa kwa ajili ya uvuvi, hivyo aliwataka vijana ambao hawajajiunga katika vikundi wajiunge ili waweze kunufaika na mikopo.

No comments: