Tuesday, November 4, 2014

VIONGOZI WA SERIKALI, WANASIASA WATAKIWA KUHESHIMU MIPAKA YA KAZI ZAO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa uelewa mdogo kwa viongozi wa serikali na vyama vya siasa juu ya mipaka ya kazi zao, kumekuwa kukisababisha jamii kukosa haki zao za msingi na kusababisha wengi wao kuwa maskini.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kituo cha wasaidizi wa kisheria na haki za binadamu (WAKIHAMBI) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Daniel Chindengwike alipokuwa akisoma taarifa fupi ya ufunguzi wa kituo hicho wilayani humo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku hoteli mjini hapa.

Chindengwike alisema kituo hicho kilianzishwa wilayani humo, kwa lengo la kusaidia jamii katika mambo ya kisheria, ili waweze kupata haki zao ambazo huporwa na wajanja wachache.


Alisema tokea kituo hicho kianze kufanya kazi zake wilayani Mbinga, kimeweza kutatua migogoro ya ndoa, ardhi, kesi za madai, usuluhishi na upatanishi pamoja na matatizo ya ajira kwa watumishi wa serikali ikiwa  ni pamoja na mirathi na viinua mgongo.

Pamoja na mambo mengine, mgeni rasmi katika ufunguzi huo Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alisema jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa wasaidizi hao wa masuala ya kisheria, ili waweze kutekeleza vyema majukumu ya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Ngaga alisema jamii inatakiwa kutambua kuishi katika hali ya ubinadamu na sio kutendeana mabaya, kwani kufanya hivyo ni dhambi na hata vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu kama vile Bibilia na Korani vinakataza kufanya matendo mabaya.

Hata hivyo aliongeza kuwa haki na wajibu ndio miongozo ambayo inaweza jamii kutuongoza duniani, na kutufanya tuwe na maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


1 comment:

Anonymous said...

Msichanganye mambo ya siasa na utendaji WA halmashauri