Friday, November 21, 2014

KATIBU MKUU UVCCM TAIFA KUFANYA ZIARA MBINGA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini kinaendelea kuwa imara na kuwajali wananchi wake, Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa chama hicho, Sixtus Mapunda atafanya ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo pia na taratibu za kuimarisha chama na umoja huo kwa ujumla.

Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa Katibu huyo atapokelewa mjini hapa kesho, Novemba 22 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi na kuwasili kwenye viwanja vya ofisi kuu ya CCM wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akitokea wilaya ya Nyasa mkoani humo.

Wananchi wa wilaya hiyo wameombwa kujitokeza kwa wingi, katika kushiriki zoezi hilo muhimu  la mapokezi.

Aidha Mapunda katika ziara yake baada ya kuwasili kwenye ofisi za chama hicho, atafanya ziara fupi akielekea kata ya mpepai kwa ajili ya kuzungumza na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata hiyo.

Baadaye atarudi Mbinga mjini kwa lengo pia la kuzungumza na wananchi mnamo majira ya mchana, hivyo wadau wanaombwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara ambao atahutubia kwenye viwanja vya soko kuu vilivyopo mjini hapa.

Kwa ujumla Mapunda sio mtu mgeni kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga, wengi wao wamekuwa wakimfahamu akiwa mzaliwa wa wilaya hii, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kumsikiliza.

Pamoja na mambo mengine, Katibu huyo wa vijana mnamo Novema 23 mwaka huu wakati anamaliza ziara yake ya kikazi wilayani humo, atazungumza na wakazi wa kijiji cha Kigonsera hatimaye kuelekea Songea mjini.


No comments: